Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewatuhumu viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Jeshi la Polisi kwa kupanga njama ili kuwaunganisha viongozi wa juu wa Chadema kwenye kesi ya kumwagiwa tindikali, Mussa Tesha. Viongozi waliotajwa hadharani kuwa wanapanga mbinu hizo ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba na Ofisa wa Jeshi la Polisi makao makuu, Advocate Nyombi. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Uenezi, John Mnyika alisema mikakati hiyo imesababisha kukamatwa kwa Katibu wa Chadema mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kileo wiki iliyopita na kupelekwa Igunga, mkoani Tabora kuunganishwa kwenye kesi hiyo.
Kileo alikamatwa na kupelekwa makao makuu ya Jeshi la Polisi ambako alihojiwa na jopo la maofisa wa polisi. Kwa mujibu wa Mnyika baada kuhojiwa aliwekwa mahali pasipojulikana na kwamba alizuiwa kuwekewa dhamana. Mnyika alisema siku iliyofuata, walielezwa kwamba Kileo alipelekwa Igunga kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka akituhumiwa kumwagia tindikali Tesha. “Tumepata taarifa kwamba Kileo aliteswa vibaya na polisi ili awataje viongozi waliomtuma lakini alikuwa akibishana nao, lakini baadaye aliandikisha mambo waliyoyataka polisi,” alisema. Akijibu tuhuma hizo, Nchemba alisema hakuna mikakati yoyote inayofanywa kati yake na Nyombi bali hiyo ni hofu yao viongozi wa Chadema kwa sababu wanafahamu kwamba walitenda kitendo hicho.
Source: Kaminyonge R. (June 2013).Chadema yalia hujuma kesi ya tindikali Igunga. Dar. Retrieved from Mwananchi
No comments:
Post a Comment