WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, amemtaka waziri wa ushirikiano wa Afrika Mashariki Samwel Sitta, aweke wazi njia anazotumia kupambana na ufisadi nchini ambazo mawaziri wengine wa serikali ya CCM hawawezi kuzitumia. Wakati Wassira akitaka ufafanuzi huo, Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe kwa upande wake alikataa kuzungumzia mbinu anazotumia Samwel Sitta kwa kile alichoeleza kuwa hawezi kuongelea masuala ya serikali na mtu asiyemjua.
Wassira na Chikawe walitoa kauli hiyo jana wakati gazeti hili lilipotaka maoni yao juu ya kauli ya Sitta iliyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa katika serikali nzima ni mawaziri wanne waliojipambanua kupambana na ufasadi na kutetea wanyonge. Wassira alisema kwa sasa hawezi kuchangia jambo lolote juu ya kauli hiyo ya Sitta kwa kuwa hajaliona katika vyombo vya habari au kumsikia waziri huyo akisema hadharani.Alisema kama kauli hiyo imetolewa na Sitta ni vema angefafanua mbinu anazotumia ili wengine waige.
“Mimi siwezi kuzungumzia hayo; mmeyasema nyie pia ingekuwa ni vema kama angeulizwa Sitta mwenyewe na atueleze mbinu zake tuone na wengine wanafanya nini,” alisema Wassira.Alipoulizwa kama majina yaliyotajwa ni miongoni mwa makundi yanayodaiwa kujipanga ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa ajili ya urais wa 2015; Wassira alisisitiza jambo hilo aulizwe Sitta. Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe, alipopigiwa simu kwa ajili ya ufafanuzi wa kauli hiyo, alikataa kuzungumzia jambo lolote kwa madai kuwa alishajeruhiwa kwa kutoa habari kwa njia ya simu.
“Sitaki na sizungumzi mambo ya serikali na mtu nisiyemjua tena katika simu…siku moja alinipigia mtu akasema anatoka Daily News nilipompa habari akaandika anavyojua na ikaniletea matatizo, kwanza kwa sasa niko Arusha,” alisema Chikawe na kukata simu. Juzi wakati Waziri Sitta, akishiriki harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph katika Parokia ya Igoma jijini Mwanza, aliwataka Watanzania kujihadhari na watu wasio waadilifu katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2015. Alisema watuhumiwa wa kashfa ya ufisadi wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond na Dowans ni hatari na hawastahili kuungwa mkono katika uongozi.
Alisema kutokana na hali hiyo ya ufisadi yeye pamoja na mawaziri wengine watatu wako pamoja katika fikra za kupambana na vitendo vya kifisadi, uonevu na mikataba tata. Aliwataja mawaziri hao kuwa ni Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, pamoja na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli.
Source: Khamis A. (May 2013). Wassira amvaa Sitta. Retrieved from Tanzania Daima

No comments:
Post a Comment