Ni rahisi mno kuwafahamu wanasiasa makini na wanafiki, kutokana na maneno pamoja na matendo yao. Wanasiasa makini hawapo tayari kupoteza heshima waliyojijengea kwa wapiga kura wao na jamii. Kwa msingi huo wanasiasa makini hawapo tayari kuburuzwa kwa suala lenye maslahi ya wachache au kundi fulani, bali wapo kwa suala lenye maslahi ya wengi kwa maana ya taifa.Wanapojipambanua na wale wanasiasa legelege au wanafiki ambao huburuzwa kwa kujua au kutojua kwa faida ya wachache. Mwishoni wanasiasa hawa legelege huilalamikia Serikali wanapokaliwa vibaya kisiasa popote pale kama vile majimboni mwao au katika maeneo yao kisiasa.
Kitendo cha wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa na tabia ya kuunga mkono bajeti mbalimbali hata zile ambazo zinaonekana wazi kuwa na dosari, ni dhahiri ni unafiki unawasumbua. Unafiki unawasumbua kutokana na tabia yao hiyo ya kuipongeza Serikali kwa kila kitu, hata kwa yale mambo ambayo yanaonekana wazi kuwa na upungufu. Kinachoshangaza zaidi ni tabia yao baada ya kuunga mkono bajeti hiyo, lakini muda mfupi husimama bila hata aibu wakieleza matatizo waliyonayo katika majimbo yao.
Swali la kujiuliza ni wanaona woga gani wa kuipinga bajeti hizo kutokana na matatizo yaliyopo katika majimbo yao? Inatia hasira na inafedhehesha kuwaona wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi bungeni, wakiwageuka wapiga kura wao na kuitetea Serikali hata kwa yale mambo ambayo yanaonekana wazi kuwa na kasoro. Wapo wabunge wa CCM wachache ambao wameonyesha misimamo yao kwa siku za karibuni, kwa kuikosoa Serikali bila woga, huku wakishambuliwa na hao wanafiki kwa kitendo chao cha kuikosoa Serikali yao. Ni ujinga na ulimbukeni wao ndio maana wanafanya hivyo, wao wanadhani kuwa Mbunge wa chama tawala ni lazima kuipongeza Serikali hata kwa uozo unaoonekana wazi mbele ya Watanzania.
Wanaiunga mkono Bajeti na kutoa pongezi za kila aina, lakini baada ya muda kidogo wanasimama bila aibu wakieleza matatizo yaliyopo katika majimbo yao. Wao wanadhani ni sifa kuunga mkono kila bajeti, ili hali wakijua kuna matatizo katika majimbo yao, wanasahau kero za wananchi wao na kuona ni bora kuisifia Serikali. Sina budi kuwapongeza baadhi ya wabunge wa chama hicho, walioonyesha misimamo yao bila woga kuwa wanatoka katika chama tawala, lakini wao wameweza kupinga bajeti mbalimbali ambazo waliona hazina manufaa kwa wananchi wao.
Muda utafika kwa wabunge hawa wanafiki wakiendeleza unafiki wao huo, mwaka 2015 itakuwa mwisho wao wa kuwa mjengoni kwa kuwa wameharibu kwa mikono yao wenyewe nafasi walizopewa na wapiga kura wao. Nasema hivyo kwa sababu Watanzania wa leo wamebadilika si wale wa miaka ya 47, ni waelewa hata kama wabunge wao watarudia maneno matamu kwa kuwalaghai wawapigie kura, huku wakimwaga chakula, fedha, khanga, fulana na vitu vingine vingi kama kawaida yao nadhani hawatadanganyika sasa.
Ninachofurahia ni kutokana na Watanzania wa leo kuwa na uelewa mkubwa, nina imani watapokea hiyo misaada lakini katika sanduku la kura hawataweza kufanya hivyo. Endapo wataendelea kuwachagua kwa kupewa misaada, najua hata Mwenyezi Mungu ataendelea kuwalaani Watanzania kwa kuwapa maisha magumu kama yalivyo hivi sasa.
Ushauri wangu kwa wabunge wanafiki, ni kubadilika kama watahitaji kurudi katika hizo nafasi zao uchaguzi ujao, wasifanye mambo kwa ajili ya kumfurahisha mtu bali wafanye kwa kuwatatulia wananchi kero zao na kuzitekeleza ahadi walizozitoa uchaguzi uliopita. Nina imani endapo wabunge wakiacha unafiki wakaungana na kuwa na msimamo ambao utasababisha taifa kuwa na maendeleo, lakini kama wataendelea kuangalia matumbo yao tu hilo litakuwa ni ndoto.
Source: Hombo E (May 2013). Unafiki huu wa wabunge wa CCM hadi lini?. Retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment