CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inakihujumu kwa kuzuia shughuli za kisiasa kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara. Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, alipozungumza na waandishi wa habari, ambapo alibainisha kuwa ngome ya chama hicho kwa Tanzania Bara ipo kwenye mikoa hiyo. Mtatiro alisema miongoni mwa hujuma hizo ni baadhi ya viongozi wa chama hicho kutishwa kwa namna mbalimbali na kutuhumiwa kuhusika kwenye vurugu za Lindi na Mtwara, jambo ambalo si kweli.
“Ni kweli yapo madai kwamba viongozi wetu wanatishwa… wanatafutiwa sababu waonekane ni chanzo cha vurugu za Lindi na Mtwara. “Viongozi wa CUF waliohojiwa na polisi ni Katani Katani, huyu ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana taifa na Katibu wa CUF wa Wilaya ya Mtwara Mjini,” alisema Mtatiro. Kwa mujibu wa Mtatiro, kwa sababu ya hujuma hizo, uongozi wa CUF taifa umeamua kuzungumza na wananchi wa Mtwara na Lindi wanaoishi Dar es Salaam. Alisema Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, atakutana na wananchi hao kwenye makao makuu ya chama hicho yaliyopo Buguruni jijini Dar es Salaam Juni 2, mwaka huu na kuwaeleza faida na hasara ya kusafirisha gesi iliyogunduliwa kwenye mikoa hiyo.
“Vurugu za kusini ni matokeo ya serikali kuwafungia wananchi wasikutane na wadau ili kupata mawazo ya upande wa pili kuhusu rasilimali hiyo,” alisema Mtatiro. Alisema ni kikao cha wazi kitakachojumuisha watu wa kada na rika mbalimbali kutoka mikoa ya kusini, ambapo Profesa Lipumba atatoa mada, na maazimio yatakayotolewa yatapelekwa kwa viongozi wakuu serikalini.
Source: Mark I. (May 2013). Rufu za CCM zaitesa CUF. Retrieved from Tanzania Daiama
No comments:
Post a Comment