ASEMA KUNDI LAKE NI CCM, AKANA KUMCHANGIA FEDHA
SIKU chache baada ya Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kuwataja mawaziri wenzake watatu akidai kuwa ni marafiki zake wasafi wasio walafi na wanaomuunga mkono katika vita ya ufisadi, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, amemruka. Kwa mujibu wa chanzo chetu, Magufuli amekana madai ya Sitta akisema kuwa hajawahi kuwa na ushirikiano wa kumuunga mkono katika masuala ya kisiasa wala hajawahi kumtuma akaseme chochote. Badala yake Magufuli amesema kuwa habari hizo ameshangaa kuzisoma kwenye vyombo vya habari wakati akiwa hajawahi kufanya makubaliano yoyote na Sitta wala kuunda kundi la mbio za urais mwaka 2015.
Katika kile kinachoonekana kama ilikuwa mbinu ya kujitafutia umaarufu wa kisiasa, Sitta ambaye anatajwa kuwa mmoja wa makada wa CCM watakaowania urais mwaka 2015, aliwataja marafiki zake hao juzi wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki la Josephine Bakita, Parokia ya Igoma, Mwanza. Waliotajwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, akisema wana mikono safi, si kama wengine walafi na waongo wanaowatumbukiza katika mikono ya Dowans na Richmond, ambao si waadilifu na wazalendo. Sitta aliwasilisha zaidi ya sh milioni 25 ambazo alisema kati yake sh milioni tano zilitoka kwa Membe, sh milioni tano nyingine zilichangwa na Dk. Mwakyembe na Dk. Magufuli huku yeye (Sitta) akichangia sh milioni tano.
Hata hivyo, Magufuli kupitia chanzo chetu hicho alikana kuwa fedha hizo zilizotajwa na Sitta hakuwahi kuchangia hata senti moja. “Naapa sijawahi kuzungumza wala kuhudhuria mkutano wa kundi lolote la mgombea urais, naomba Mungu aogopwe, watu wasiwasingizie wengine. Mimi kundi langu ni CCM,” alisema.Kwa mujibu wa chanzo hicho, Magufuli alisema kuwa kwa sasa Rais ni Jakaya Kikwete, ambaye anaiwakilisha CCM, hivyo ni makosa kuanza kampeni za urais kwa mwaka 2015 wakati muda wake bado. Sitta katika hotuba yake hiyo alifafanua kuwa fedha zilizobaki ili kutimia mchango wake sh milioni 25 zilichangwa na wabunge wanaowaunga mkono, ambao ni Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, Waziri wa Uwekezaji na Uwezeshaji, Mary Nagu, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage na Catherine Majige.
Wengine ni Mbunge wa Kahama, James Lembeli, Waziri asiye na wizara maalumu Mark Mwandosya pamoja na Victor Mwambalaswa, ambao wote walimchangia sh 500,000 kila mmoja huku Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alitoa sh milioni moja. Sitta alisema kuwa mafisadi wanapaswa kukataliwa, maana wakipewa madaraka wataweka vibaraka wao na nchi itaelekea pabaya, na hiyo ndiyo inaweza kuzusha vurugu. Hatua hiyo ya Magufuli kumkana Sitta ni dhahiri kuwa itaibua mpasuko mwingine ndani ya CCM baina ya makundi yanayotajwa kujipanga kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu huo. CCM hivi karibuni ilionya vikali makada wake wanaokusudia kugombea nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi Mkuu ukiwamo urais kuwa wasithubutu kufanya kampeni zozote, kwani muda bado na kwamba atakayekiuka atachukuliwa hatua.
Source: Kamukara E. (May 2013). Magufuli amruka Sitta. Dodoma. Tanznia Daima

No comments:
Post a Comment