KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI YA WIZARA YA KAZI NA AJIRA KWA MWAKA 2013/2014
(Inatolewa
chini ya Kanuni ya 99(9) ya kanuni za Bunge toleo la mwaka 2013)
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa spika,
mwaka jana nilianza hotuba yangu kwa kutoa pole kwa ndugu jamaa na
marafiki wa wale wote waliofariki dunia
kwa ajali ya mv skagit, mwaka huu naomba nianze hotuba yangu kwa kutoa pole kwa
ndugu jamaa na marafiki wa wale waliofariki kwa ajali nyingine ya kizembe ya
kuanguka kwa ghorofa la Dar Es Salaam. Aidha, mwaka jana nilianza kwa kutoa
pole kwa Mh. Joseph selasini kwa kufiwa na baba yake na mwaka huu nianze pia
kwa kutoa pole kwa Mh. mchungaji Israel Natse kwa kufiwa na baba yake mzee
Yohana Natse. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake , mahali pema peponi.
Mheshimiwa Spika,
hakuna ubishi wala ushindani kuwa Serikali yoyote makini duniani huweka sera na
mifumo thabiti ya kuhakikisha kuwa ajira za kutosha zinatengenezwa, mazingira
ya kazi yanaboreshwa na wafanyakazi wanalipwa ujira na mishahara yenye staha,
si tu kwaajili ya kuwawezesha kumudu gharama za maisha, bali pia kuwapa morali
wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi kwa maendeleo ya taifa.
Mheshimiwa Spika,
napenda kusisitiza kuwa Taifa lolote
duniani ambalo haliwezi kutengeneza ajira na hivyo kuwafanya vijana wake wengi
wenye uwezo wa kuajiriwa kuzurura mitaani, na wale walio vyuoni wanashindwa
kusoma kwa sababu ya Serikali kushindwa au kupuuza kugharamia masomo yao; sote
tunatambua kuwa Taifa hili limejaliwa
rasilimali nyingi za utalii na madini ya thamani, lenye vyanzo vingi vya kodi
na mapato, lakini limegubikwa na migogoro mingi, ya mara kwa mara na
isiyokwisha, ya wafanyakazi wanaodai haki na mafao yao halali, huku wakiishia
kunyamazishwa kwa kauli laini zenye matumaini hewa; Kwa namna yoyote ile taifa
hilo, ni kielelezo cha nchi inayoongozwa na Serikali isiyo na vipaumbele, yenye
viongozi wasiojali na wanaotekeleza sera wasizozijua au zilizoshindwa.
2.0 MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII
Mheshimiwa Spika,
katika Maoni yetu ya mwaka jana, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilituhumu
kwamba Serikali hii ya CCM haiijatekeleza ahadi zake kwa Watanzania kuhusu
mifuko ya hifadhi ya jamii kama zilivyotajwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2010 – 2015. Katika
Maoni hayo tulidai kwamba ahadi ya “… kurekebisha viwango vya mafao ili
visipishane mno haijatekelezwa hadi sasa kwani viwango vya mafao vinavyotolewa
na Mifuko mbali mbali ya Hifadhi ya Jamii ni vile vile vya kabla ya Uchaguzi
Mkuu wa 2010.” Aidha, tulifafanua jinsi ambavyo ahadi ya “… ya kupanua wigo wa
kinga ya hifadhi ya jamii ili Watanzania wengi zaidi wafaidike na huduma hiyo
nayo haijatekelezwa.” Vile vile, tulionyesha jinsi ambavyo ahadi ya “kuelimisha jamii … juu ya umuhimu wa
hifadhi ya jamii kwa maendeleo ya wafanyakazi na ya nchi kwa ujumla”, nayo
haikutekelezwa kwa sababu Serikali yenyewe imekiri kwamba ‘“… bado kuna uelewa mdogo wa masuala ya hifadhi
ya jamii kwa watunga sera, waajiri, waajiriwa, wanachama na wananchi kwa
ujumla.”’
Mheshimiwa Spika,
katika Maoni yetu hayo tulionyesha kwamba ahadi pekee ambayo Serikali hii ya
CCM imeitekeleza ni “… kuendelea kutumia
fedha za wafanyakazi zilizomo katika Mifuko mbali mbali ya Hifadhi ya Jamii
kuwekeza katika miradi ambayo haina manufaa yoyote kwa wafanyakazi wenyewe.”
Tulifanya rejea pana ya Taarifa Kuu ya
Mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Kuhusu Hesabu za
Mashirika ya Umma na Taasisi Zingine kwa Mwaka 2010/2011, iliyoonyesha
kwamba “… kuna udhaifu mkubwa katika vitega uchumi vinavyosimamiwa na Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii.” Hivyo,
kwa mfano, ukaguzi wa vitega uchumi vya NSSF ulionyesha kwamba licha ya Mfuko
huo kuwekeza zaidi shilingi bilioni 269.272 za wafanyakazi katika ujenzi wa
Awamu ya Kwanza na ya Pili ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), sio tu Mfuko huo
‘“… ulikuwa haujasaini mkataba na Serikali juu ya fedha za mradi huo”’, bali
pia ulikuwa ‘“… haujapokea fedha ya
pango, au malipo ya mkopo kutoka Serikalini ambao tayari umelimbikiza riba ya
shilingi bilioni 14.157.”’
Mheshimiwa Spika,
kwa kutumia Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu tulionyesha kwamba sio fedha za
NSSF tu ambazo zimetumiwa na Serikali hii ya CCM kwenye UDOM. Kama tulivyosema,
“… PPF imekwishazamisha jumla ya shilingi bilioni 39.987; PSPF imechakachuliwa
shilingi bilioni 105.921; LAPF imepoteza shilingi bilioni 22.030; wakati ambapo
NHIF imekwishaunguza shilingi bilioni 13.403 za wanachama wake. Jumla ya fedha
za wafanyakazi wanachama wa Mifuko hii mitano ambazo zimeunguzwa katika ujenzi
wa UDOM ni shilingi bilioni 450.615…. Vitega uchumi vyote hivi katika UDOM …
havirudishi fedha za mikopo ya Mifuko
husika.” Hali kadhalika, tulionyesha
jinsi ambavyo ujenzi wa Jengo la Idara ya Usalama wa Taifa ulivyotafuna
shilingi bilioni 11.83 za NSSF na PSPF ambazo hadi tunaandika Maoni yetu ya
mwaka jana zilikuwa hazijaanza kulipwa pamoja na riba yake! Vile vile,
tulionyesha kwamba jumla ya shilingi bilioni 19.77 zilitolewa kama mikopo na
NSSF, PPF na LAPF kwa ajili ya ujenzi wa Ukumbi huu wa Bunge lako tukufu “…
hazijalipwa hadi sasa.” Aidha, zaidi ya shilingi bilioni 152.6 zilizotolewa
kama mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Jeshi la Polisi, Machinga Complex,
Continental Venture Tanzania Ltd., Meditech Industrial Co. Ltd., General Tyre,
Dar es Salaam Cement Co. Ltd., Kagera Sugar, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu (HESLB) na Kiwira Power Ltd. haikuwa imelipwa. Kwa sababu hizo,
tulimnukuu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali akisema “… ukubwa wa biashara inayofanywa baina ya
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na taasisi za Serikali na malipo yasiyokuwa na
uhakika ya mikopo hiyo yanatia shaka juu ya uendelevu wa Mifuko husika katika
siku chache zijazo.”
Mheshimiwa Spika,
licha ya kuwa yalitokana na Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali ambaye ni mteuliwa wa mhe. Rais Mheshimiwa Dokta Jakaya Mrisho
Kikwete, Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni yalishambuliwa sana na
Wabunge wa CCM na wawakilishi wa Serikali yake humu bungeni. Hata hivyo, facts are very stubborn things, kama
mwanamapinduzi mmoja wa karne iliyopita alivyokuwa anapenda kusema. ‘Ukweli ni
vitu vikorofi sana’! Na ukweli juu ya afya ya Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii
ni vitu vikorofi kweli kweli, ambavyo haviwezi kuzimwa na propaganda nyepesi
nyepesi za watawala na wawezeshaji wao ndani na nje ya Bunge hili tukufu.
Mheshimiwa Spika,
katika hotuba yake wakati wa Sherehe za Mei Mosi mwaka huu kule Mbeya, Rais
Kikwete alielezea ‘tathmini ya afya ya kifedha’ ya Mifuko yote ya Hifadhi ya
Jamii nchini kama sehemu ya ‘maboresho’ ya sekta hiyo. Tunaomba kumnukuu Rais in extenso: “Tathmini hiyo imeonesha kuwa mifuko yetu ya hifadhi ya jamii ipo kwenye
hali nzuri kifedha na ni endelevu. Kwa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma
(PSPF), Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya malipo ya michango ya
watumishi waliokuwepo kabla ya mwezi Julai 1999 mfuko ulipoanzishwa rasmi. Kwa
hiyo, katika mwaka ujao wa fedha, Serikali italipa shilingi bilioni 50 ikiwa ni
sehemu ya malipo hayo. Napenda kuwatoa hofu wanachama wa Mfuko huo kuwa mafao
yao yako salama. Hakuna atakayestaafu akakosa kulipwa mafao yake.
“Vile vile Mamlaka ya Udhibiti
na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa kushirikiana na Benki Kuu
wameandaa na kutoa miongozo … yenye lengo la kuiwezesha mifuko ya hifadhi ya
jamii kufanya uwekezaji ulio bora na wenye tija unaomnufaisha mwanachama na
taifa kwa ujumla. Tangu kuanza kutumika kwa miongozo hiyo Mei 2012, uwekezaji
wa mifuko hiyo umeongezeka kutoka shilingi trilioni 3.38 mpaka shilingi
trilioni 4.24. Pia mali za mifuko hiyo zimeongezeka kutoka shilingi trilioni
3.74 hadi kufikia shilingi trilioni 4.73.”
Mheshimiwa Spika,
matrilioni haya ya Rais Kikwete yanahitaji kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa na
Bunge lako tukufu. Hii ni kwa sababu takwimu hizi zimetiliwa na shaka na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali Kuhusu Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012
iliyowasilishwa kwa Rais tarehe 28 Machi, 2013. Tunaomba kuiacha Ripoti ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu ijisemee yenyewe: “Ukaguzi
wa Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali Kuu (PSPF) ulibaini kwamba
‘actuarial valuation’ iliyofanyika … tarehe 30 Juni, 2010 … ilionyesha kuwa
hali ya kifedha ya Mfuko iliendelea kuwa mbaya. Ukadiriaji thamani ulibaini
hasara halisi ya shilingi trilioni 6.487 kwa mwaka unaoishia tarehe 30 Juni,
2010.
“Pia nilibaini kwamba katika
mwaka wa fedha 2011, Serikali ilikubali kuanza kurejesha mafao yaliyolipwa na
Mfuko kuanzia mwaka 2004 hadi 2010 kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni
716. Kiasi hiki kilipaswa kurejeshwa kidogo kidogo na Serikali kila mwaka
katika mgawanyo wa shilingi bilioni 71.6 kwa muda wa miaka kumi kuanzia mwaka
2010. Kufikia mwaka unaoishia tarehe 30 Juni, 2012 kulikuwa na malimbikizo ya
marejesho katika kipindi cha mwaka 2011 hadi 2012 na kufikia kiasi cha shilingi
bilioni 133. Vile vile, ilibainika kwamba, Serikali ya Tanzania haikuweza kutoa
fedha za kuziba pengo la upungufu uliojitokeza … ikiashiria kuwepo kwa shaka
kuhusiana na uwezo wa Mfuko kuendelea kulipa madeni yake yanapokuwa tayari kwa
kulipwa.”
Mheshimiwa Spika,
ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kwa mwaka wa fedha uliopita inafichua
‘ukweli korofi’ zaidi kuhusu afya ya kifedha ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii hapa
nchini. Hivyo basi, Ripoti hiyo inaonyesha kwamba PSPF imetoa mikopo
‘isiyolipika’ ya jumla ya shilingi bilioni 67. 179 kwa Serikali na taasisi
zisizo za kiserikali “… na hakuna malipo
yoyote yalifanywa kwa Mfuko katika kipindi chote cha mwaka. Hii inaweza
kuharibu mtiririko wa fedha za Mfuko na matokeo yake kushindwa kulipa mafao
yanapofika wakati wa kulipwa.” Taasisi zisizokuwa za kiserikali
zilizofaidika na mikopo ‘isiyolipika’ ya fedha za watumishi wa Serikali hii ya
CCM ni pamoja na Tan Power Resources, kampuni iliyokuwa inamilikiwa na familia
ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa na ya swahiba wake Daniel Yona ambayo iliwahi
kumilikishwa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira kwa njia za kifisadi. Kwa mujibu
wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, Tan Power Resources ina ‘madeni
yasiyolipika’ kwa PSPF ya jumla ya shilingi bilioni 5.421! Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu inaeleza
kwamba PSPF imeingia mkataba na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutoa
fedha za kujenga Chuo Kikuu cha Elimu Dodoma. Hata hivyo, “mapitio ya mkataba
yalibaini mkanganyiko wa tafsiri ambao unahitaji kutatuliwa mapema. Kutokuwa na
mkataba sahihi kunafanya kuwa na tafsiri mbali mbali ambazo matokeo yake ni
hasara kwa Mfuko iwapo mgogoro utajitokeza.”
Mheshimiwa Spika, PSPF
sio Mfuko wa Hifadhi ya Jamii pekee ambao afya yake ya kifedha ni ya
mashaka. Kwa mujibu wa Ripoti ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, PPF imetoa shilingi bilioni 71 katika ujenzi wa UDOM
“… ingawa mkataba wa kutoa fedha kwa ajili ya mradi huu kati ya Mfuko na Serikali
… bado haujakamilika hadi ripoti hii inaandaliwa.” Kwingineko katika Ripoti
hiyo, inasemekana kwamba majengo ya UDOM yenye thamani shilingi bilioni 452
‘zilizofadhiliwa’ na Mifuko ya Jamii ‘chini ya maelekezo ya Serikali’ “… hayajakabidhiwa
rasmi kwa Chuo Kikuu Dodoma na Serikali ambayo ilisaini mkataba na Mifuko ya
Jamii ya NSSF, PSPF, LAPF na PPF.”
Kwa
kuhofia kwenda kinyume na matakwa ya kanuni ya 64(1)(d) na (e) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inachelea kumwita Rais Kikwete
muongo kutokana na kauli yake juu ya afya ya kifedha ya Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii. Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua, na Watanzania
wanataka kujua, kati ya Rais na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
ni yupi anayesema ukweli kuhusu hali ya kifedha ya Mifuko ya Hifadhi ya Afya ya
Jamii katika nchi yetu? Ni nani aaminiwe na Watanzania kati ya Rais Kikwete
anayesema kwamba “… mifuko yetu ya
hifadhi ya jamii ipo kwenye hali nzuri kifedha na ni endelevu”; na Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anayesema kwamba “… hali ya mfuko wa hifadhi ya jamii uko katika hatari ya kutoendelea
kama hatua madhubuti hazitachukuliwa na pande zinazohusika”? Aidha,
wafanyakazi wa Serikali ya Tanzania wampuuze yupi kati ya Rais ‘anayewatoa
hofu’ kwamba “hakuna atakayestaafu
akakosa kulipwa mafao yake”; na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu anayedai kuwa kuna “… shaka kuhusiana na uwezo wa Mfuko kuendelea kulipa madeni yake
yanapokuwa tayari kwa kulipwa.”
Mwisho,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM iwaambie
Watanzania nani ni mkweli kati ya Rais Kikwete anayedai kuwa mali za Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii imefikia shilingi trilioni 4.73; na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
anayetuambia kwamba ukaguzi wake wa PSPF pekee unaonyesha ‘hasara halisi’ ya
shilingi trilioni 6.487!
Mheshimiwa Spika,
katika mazingira ya kiza na utatanishi kama haya, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inarudia wito wake wa mwaka jana kwa Serikali “… kusitisha mara moja matumizi haya makubwa ya fedha za wafanyakazi
katika miradi ambayo inaelekea kuifilisi Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na hivyo
kuhatarisha maslahi ya moja kwa moja ya wafanyakazi wa Tanzania.”
Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia kauli yake ya mwaka jana: “… Ni wazi kwamba Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
ya Tanzania inaongozwa, kuendeshwa na kusimamiwa na watu ambao hawana uwezo wa
kutekeleza majukumu yao kwa ujuzi na uadilifu unaohitajika kwa maslahi ya
wafanyakazi wanachama wa Mifuko hiyo. Ni wazi, kwa ushahidi huu, kwamba
mabadiliko makubwa ya kimfumo na kiutendaji katika Mifuko hii yanahitajika na
kwa haraka kabla mifuko hii haijafilisika kabisa.” Vile vile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inawataka wastaafu na wafanyakazi wa Tanzania sasa waelewe chanzo halisi cha
mafao yao ya uzeeni kucheleweshwa ama kutokuongezeka ama kutokulipwa kabisa na
Serikali hii ya CCM! Na wakishafahamu sababu halisi za mateso yao, wastaafu na
wafanyakazi wa Tanzania wachukue hatua stahiki dhidi ya wale wote ambao kwa
sera zao na utekelezaji wao wa sera hizo, wamesababisha mateso hayo kwa
wastaafu na wafanyakazi wetu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba
bila wafanyakazi kuchukua hatua hizo, maneno ya ibara ya 11(1) ya Katiba yetu
kwamba “mamlaka ya nchi itaweka utaratibu
unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa haki ya mtu … kupata msaada
kutoka kwa jamii wakati wa uzee, maradhi au hali ya ulemavu, na katika hali
nyinginezo za mtu kuwa hajiwezi …” yatabaki dhihaka ya kikatili kwa
wastaafu na wafanyakazi wetu.
Mheshimiwa
Spika, aidha Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kurejea pendekezo letu tuliloishauri katika
bajeti ya Wizara hii ya mwaka 2011/2012 katika kuona umuhimu wa kuiunganisha
mifuko yote ya hifadhi za jamii na kubaki katika wizara moja ambayo ni ya Kazi
na Ajira. Kambi rasmi ya Upinzani inasisitiza kuwa lengo kuu la kuunganisha
mifuko hii ya hifadhi za jamii ni katika kuirahisishia Mamlaka ya Usimamizi na
Udhibiti wa Hifadhi za Jamii (SSRA) katika kutekeleza Sheria moja na kuunda
vifungu sawa vya kisheria vitakavyosimamia utekelezaji na uendeshaji wa mifuko
hii ambapo kwa sasa mifuko hii imekuwa chini ya wizara tofauti na hivyo hata
utekelezaji wake unakua mgumu na kuleta ukinzani kwa Mamlaka ya Usimamizi na
Udhibiti wa Hifadhi za Jamii. Tunasisitiza kuwa pendekezo letu ni kuifanya PPF
na NSSF iunganishwe na kuwa mfuko mmoja kwaajili ya Sekta Binafsi vilevile
LAPF, PSPF na GEPF iunganishwe na kuwa mfuko mmoja kwaajili ya Sekta ya Umma.
Pia, kambi ya Upinzani inapendekeza mifuko yote isimamiwe chini ya Wizara ya
Kazi na Ajira.
3.0 NYONGEZA YA MISHAHARA YA
WAFANYAKAZI NCHINI
Mheshimiwa Spika,
Katika hotuba yake ya Mei Mosi mwaka huu, Raisi Kikwete alisema kuwa "
........Kwa upande wa makusanyo ya kodi kwa mfano,mapato
yameongezeka kutoka wastani wa shilingi
bilioni 541 kwa mwezi mwaka 2011/12 hadi kufikia shilingi bilioni 637
kwa mwezi mwaka 2012/13, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18. Mapato yanapoimarika kama hivi, Serikali inakuwa na uwezo mkubwa wa kuwahudumia
wananchi wake, kutekeleza miradi ya maendeleo na wakati huo huo kuboresha zaidi maslahi ya wafanyakazi........
Pamoja na mafanikio hayo, lakini bado
hatujafikia mahali ambapo tunaweza kuongeza mishahara kama vile ambavyo tungependa sote tupate. Hata kwa
kiwango cha sasa ambacho sote tunakubaliana hakitoshi bado mishahara inachukua sehemu kubwa ya mapato ya
Serikali."
Mheshimiwa Spika, kitendo
cha Raisi kusema kuwa mishahara itaongezwa bila ya kutaja kiwango kama ilivyo
desturi ya mei mosi haitoshi. Ni lazima Serikali iseme kiwango cha nyongeza
ya mshahara kwa wafanyakazi nchini kwa
mwaka ujao wa fedha wa 2013/2014 ni kiasi gani, na je nyongeza hiyo itatatua
matatizo ya wafanyakazi kwa kiwango gani? Aidha, kambi rasmi ya Upinzani
Bungeni, inaiona kauli ya Mheshimiwa Raisi kuwa, Serikali imedhibiti ubadhirifu
wa umma, ni lazima ionekane katika mishahara ya wafanyakazi wa sekta zote za
umma na za binafsi.
4.0 PUNGUZO LA KODI YA MAPATO KWA WAFANYAKAZI PAYE)
Mheshimiwa Spika,Pamoja
na ugumu wa mazingira ya kazi, mishahara duni na hali ngumu ya maisha nchini,
bado mfanyakazi anaendelea kunyonywa kwa kiwango kikubwa cha PAYE , ambacho ni
moja ya vyanzo vya Serikali katika mapato, huku Serikali ikishindwa kutafuta
njia nyingine mbadala za kukusanya kodi ikiwemo
kufuta misamaha ya kodi isiyo na tija kwenye uchumi wa taifa letu.
Mheshimiwa Spika, katika maoni
yetu ya mwaka jana, tulipendekeza kwamba kiwango cha PAYE ishuke kutoka
asilimia 14 za sasa hadi asilimia 9 kwa kiwango cha chini kinachotozwa na
asilimia 27 kwa kiwango cha juu kinachotozwa.Katika hotuba yake ya mei mosi,
zaidi ya kusema kwamba serikali imekamilisha uchambuzi wa maombi ya wafanyakazi
na kwamba waziri wa fedha atayafafanua zaidi katika hotuba yake ya bajeti,
Raisi Kikwete hakusema kodi ya pato la mfanyakazi itapungua kwa kiasi gani. Kwa
kuzingatia mapendekezo ya TUCTA kwamba kima cha chini cha mfanyakazi wa
Tanzania kiwe 350,000, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba
kiwango cha chini cha mshahara kitakachotozwa PAYE kiwe shilingi 350,000. Hii
itawezesha wafanyakazi wote wanaopata kiwango hicho cha mshahara au pungufu
yake kuwa na mapato zaidi na kukabiliana na mfumuko wa bei wa mara kwa mara na
kupanda kwa gharama za maisha.
Mheshimiwa Spika,wakati Serikali
hii ya CCM ikisita kupunguza mzigo wa maisha magumu unaowakabili wafanyakazi,
kwa kuwaongezea mshahara au kuwapunguzia PAYE , Serikali hiyohiyo haijawahi
kusita kutoa misamaha ya kodi kwa waajiri matajiri wa wafanyakazi. Ukweli ni
kwamba katika baadhi ya sekta
zinazoongoza kwa mauzo ya fedha za nje waajiri wamelipa kodi ya mapato
ya chini kuliko kodi ya PAYE wanayolipa wafanyakazi wao licha ya waajiri hao
kuwa na vipato vikubwa kutokana na mauzo ya bidhaa zao nje ya nchi. Kwa mfano,
kwa mujibu wa hotuba ya bajeti waziri wa nishati na madini iliyowasilishwa
na waziri mwenye dhdamana, Mh. Prof. Muhongo, katika kipindi cha miaka 14
(1992-2012), makampuni ya madini yalilipa jumla ya shilingi bilioni 468 kama
kodi ya mapato. Katika kipindi hicho hicho, wafanyakazi wao walilipa jumla ya
shilingi bilioni 506 kama PAYE na tozo ya kuendeleza ujuzi (Skills Development Levy) inayolipwa
VETA. Takwimu hizo zinaonesha kwamba, katika miaka sita ya kwanza (1999-2004)
makampuni ya madini yalilipa shilingi 0 kama kodi ya mapato, wakati waajiriwa
wao wa kitanzania walilipa shilingi bilioni 52 kama PAYE na SDL (Skills
Development Levy).Aidha,katika miaka 8 iliyofuata ,makampuni ya madini
yalilipa kodi ya mapato ya shilingi bilioni 468 wakati waajiriwa wao walilipa
shilingi bilioni 454. Kwa kipindi chote hicho kwa mujibu wa takwimu hizo za Mh. Prof Muhongo,thamani ya madini
yaliyouzwa nje ya Tanzania na makampuni hayo ilikua ni shilingi Trilioni
19.278. Kwa takwimu hizi, sio tu kwamba Serikali hii ya CCM imeruhusu utajiri
wa nchi hii kutajirisha makampuni ya kigeni bali pia imewanyonya waajiriwa wa
kitanzania wa makampuni hayo kwa kuwatoza kodi kubwa ya mapato kuliko
inayolipwa na waajiri wao wa kigeni.
4.1 Serikali na kima cha chini cha mishahara sekta
binafsi
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013 katika kifungu
2001 wizara ilitenga jumla ya shilingi 60,000,000
kwa ajili ya kuratibu na kuwezesha utafiti wa kima cha chini cha mshahara
katika sekta binafsi , na pia zilitengwa shilingi 55,000,000 kwa ajili ya vikao vya bodi 12 za kisekta za kima cha
chini cha mshahara katika seka binafsi na mwaka huu wa fedha 2013/2014 katika fungu hilo hilo zimetengwa kiasi cha
shilingi 60,600,000 kwa ajili ya
‘kuratibu na kuwezesha utafiti wa kima cha chini cha mshahara katika sekta
binafsi’, vile vile zimetengwa tena shilingi 22,325,000 kwa ajili ya ‘kuwezesha vikao vya Bodi 12 za kisekta za
kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi’. Yaani kwa miaka 2 tumetumia
jumla ya shilingi 197,925,000 kwa
ajili ya kufanya kinachoitwa utafiti na vikao kwa ajili ya kujua kama sekta
binafsi inahitaji kuongezewa mishahara ama laa na kama ipo haja iwe ni kiasi
gani.
Kambi rasmi ya upinzani
, inasikitishwa sana na mtindo wa serikali hii sikivu ya CCM ambayo inasema
kuwa inasikia lakini inaendelea kutenga fedha za kufanya utafiti kuhusiana na
kima cha chini cha mishahara ya wafanya kazi, hivi ni kweli kuwa serikali hii
haijui wafanyakazi wanastahili kulipwa nini , hivi ni kweli kuwa hamkuwasikia
TUCTA tangu mwaka 2010 walipopendekeza kuwa kima cha chini cha mshahara kiwe
kiasi gani? Hivi hamjui kuwa gharama za maisha zimepanda sana na hivyo huhitaji
kufanya utafiti kujua kama wafanyakazi wa sekta binafsi wanahitaji kuongezewa
mishahara?
Aidha
kwa maombi mapya ya kutengwa kwa kiasi hiki cha fedha kinatoa taswira kuwa,
hata kauli aliyoitoa Mhe. Raisi kwenye maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu kwa
kusema nanukuu " Katika kikao chetu
tulichokutana na viongozi wa TUCTA tarehe 27 Februari, 2013 tulijadili suala
hili na kukubaliana kwamba Serikali iendelee kulichambua zaidi ili kutoa unafuu
zaidi kwa wafanyakazi kila mwanya unapopatikana. Nafurahi kuwaarifu kuwa
kazi ya uchambuzi imekamilika na maombi yenu yamesikilizwa." Hii
ni fedheha kwa Serikali makini na sikivu
ya CCM, ambayo utendaji wake na kauli za viongozi wake wakuu ni wazi zinalenga
kuwalaghai wafanyakazi na kuwanyonya kupitia matumizi mabaya ya kodi zao!
5.0 TATIZO LA UKOSEFU WA AJIRA
NCHINI
Mheshimiwa Spika,
Tatizo la ukosefu wa ajira limeendelea kukua kila kukicha huku likiambatana na
ugumu wa maisha. Upatikanaji wa ajira katika soko la ajira nchini ni wa
kusikitisha na jambo la kushangaza ni kuwa Serikali haitaki kukubali kuwa
tatizo hili ni kubwa sana na lina athari kubwa si kwenye jamii ya kitanzania
bali hata kwenye uchumi wa taifa hili.
Leo
hii tukiwa tumefungua milango ya ushirikiano baina ya nchi wanachama wa Jumuia
ya Afrika Mashariki, kama taifa hatujaweka mikakati ya jumla ya kukabiliana na
changamoto za soko la ajira katika Jumuia. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,
inajiuliza kuwa wakati leo mfumo wa elimu wa Tanzania ukiwa katika hali tete
yenye kuzalisha kizazi kisichoweza kushindana na nchi za Kenya, Rwanda, Uganda
ambapo wazazi wengi wenye uwezo wanapeleka watoto wao huko, je nchi ipo tayari
kukabiliana na vigezo takwa vya soko la ajira la ujumla? Ndio maana leo hii si
ajabu kukuta katika soko la ajira, hasa katika utalii kwenye mikoa ya kaskazini
kama Kilimanjaro na Arusha, wakenya wameweza kuliteka soko la ajira ya utalii
kama waongoza watalii, wafanyakazi wa mahoteli makubwa ya kitalii huku
watanzania wakishindwa kutumia fursa hizo kutokana na changamoto za kitaaluma
ambazo zimesababishwa na mfumo duni wa elimu nchini.
Mheshimiwa Spika, Ili
nchi iweze kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya ajira, lazima Serikali
ikubali kuwa mfumo wa elimu uliopo sasa haukidhi matakwa ya soko la ajira
duniani. Mfumo wa elimu uliopo hauzalishi wataalamu wa kutosha wa fani
mbalimbali wanaoweza kufanya kazi kwa weledi katika sekta mbalimbali ndio maana
hata kwenye sekta ya madini nchini, leo hii asilimia kubwa ya kazi zenye
kuhitaji ujuzi na sifa za juu, zimeendelea kufanywa na wageni na bila kufuata
sheria za nchi.
Mheshimiwa
Spika, Ili tufanikiwe katika soko la ajira hatuna budi kufumua mfumo mzima wa
elimu yetu. Hakuna mabadiliko magumu duniani, kama madadiliko ya mfumo wa elimu
kwa kuwa unahusisha gharama kubwa, wakati na hata kuleta mtikisiko kwa kuwa utaathiri
hata ajira za wale waliopo; lakini pia wataalamu wanakiri kuwa mabadiliko ya
mfumo wa elimu ndio njia pekee ya kuweza kukabiliana na changamoto kubwa za
kiuchumi, kijamii, kisiasa na hata kiutamaduni. Lazima kama taifa , tukubali
kufanya maamuzi magumu ili kuokoa nchi yetu ambayo sasa imekosa mikakati
endelevu ya kukabiliana na tatizo la ajira. Kambi rasmi ya Upinzani inajua kuwa
jibu la Serikali katika kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira litakua
"mtikisiko wa uchumi duniani umeathiri nchi nyingi hata zilizoendelea nazo
lina tatizo la ukosefu wa ajira".
Mheshimiwa Spika,
tumekuwa tukishuhudia serikali ikiwatimua wafanya biashara wadogo walioamua
kujiajiri wenyewe na hivyo kuwakosesha amani na kuwakatisha tamaa.Cha
kusikitisha zaidi ni kwamba; Serikali imekuwa ya kwanza kuzikimbia bidhaa
zinazozalishwa na watanzania hawa wanaojitahidi kutatua tatizo (la ukosefu wa
ajira kwa kujiajiri wenyewe), na kukimbilia bidhaa za nje licha ya kuwa bidhaa
zinazozalishwa na watanzania zipo za kutosha na zenye hadhi na ubora wa
kutosha.Hivi serikali haioni tunawakatisha tamaa hawa watanzania ambao wameamua
kujiajiri?
6.0 UKOSEFU WA AJIRA KWA VIJANA
NCHINI
Mheshimiwa Spika, Tanzania,
tumebarikiwa kwa kuwa na rasilimali nyingi, lakini asilimia kubwa ya watanzania
imeendelea kuishi katika umasikini mkubwa , huku soko la ajira kila mwaka
likikua katika upande wa sekta ya kilimo na sekta isiyo rasmi ambapo kuna
kiwango kidogo cha ujira na uzalishaji.
Mheshimiwa Spika,tatizo
la ajira nchini limeendelea kukua, huku viongozi wa Serikali wakiendelea kupoza
wananchi kuwa tatizo la ajira si kubwa na kuwa Serikali imefanya jitihada katia
kuongeza ajira nchini. Leo hii, tunashuhudia ongezeko la ajira , lakini ajira
zisizo na tija kwa taifa, ajira zisizo za staha kwa watanzania na ajira zisizo
na ujira wa kuridhisha kwa watanzania, Je tuendelee kujisifia kuwa tunajenga
jamii yenye usawa na kuheshimu utu na thamani ya mtanzania?
Mheshimiwa Spika,
Serikali ya CCM iliahidi mambo mengi kwa mbwembwe ili kupata kura mwaka 2010,
wakati ahadi zake kwa wananchi walizotoa kwa mwaka 2005 zikiwa zimetekelezwa
kwa kiwango kidogo. Mojawapo ya ahadi hizo ni pamoja na ajira milioni moja za
Raisi Kikwete alizowaahidi wapiga kura. Serikali inayoongozwa na CCM haina budi
kutambua kuwa ari na mwamko wa watanzania leo hii si kama wa wakati ule wa
"Ndiyo mzee", kwa kuwa watanzania sasa wamenguka na wanaelewa wajibu
wao katika kuisimamia Serikali.
Mheshimiwa Spika,
tatizo la ajira nchini ni kubwa sana na Serikali isipokubali wazi kuwa hali ni
mbaya na kuamua kuweka mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na tatizo hili, ni
wazi kuwa, tunajichimbia kaburi , kwa kuwa uchumi wetu utaendelea kuporomoka
huku asilimia kubwa ya watanzania wakiishi katika maisha magumu yanayoambatana
na maumivu ya kupanda kwa gharama za maisha. Leo hii, tunasema zamani mtu
akiokota chupa na makopo ya plastiki barabarani ama kwenye majalala, ni
mwendawazimu, ila tulipofikia hata wazazi wetu, wazee ambao hawana pensheni na
wanaishi kwa mazingira magumu, wameingia mitaani na kuanza kuokota makopo kama
sehemu ya ajira kwao. Wazee wetu wanaokota makopo, vijana wanaokota makopo,
watoto wanaokota makopo, kwa kuwa taifa sasa limekosa mwelekeo wa kuweza
kuandaa mazingira kwa wazee, vijana na watoto katika kujikwamua kimaisha kwa
mipango endelevu ya kazi na ajira nchini.
Mheshimiwa Spika,
kati ya mambo ambayo yamesababisha ukosefu wa ajira nchini ni pamoja na
kutolingana kwa uhitaji na upatikanaji
wa wa ajira katika soko lo ajira, uanzilishwaji wa ajira katika shughuli za
uchumi unaotokana na sera
zisizotekelezeka za uwekezaji, kutokuwepo kwa programu mbalimbali za
ajira zinazoweza kuchangia upatikanaji wa ajira katika sekta mbalimbali kuanzia
ngazi ya taifa mpaka serikali za mitaa.
Mheshimiwa Spika,
Moja ya changamoto kubwa ambayo vijana wengi wa kitanzania tunakutana nazo ni
pamoja na kukosa elimu, maarifa, mafunzo na ujuzi unaotakikana katika soko la
ajira hapa nchini na katika jumuia ya Afrika mashariki. Wakati huohuo, kazi
nyingi zinatoa na ajira zisizoleta tija zenye masharti magumu. Kiuhasilia, kuna
matatizo mengi ya kimuundo na vikwazo vinavyofanya ajira kwa vijana na
uwezekano wa vijana kuajiriwa kuwa mgumu. Waajiri wengi, kwa mfano wanatoa
matangazo ya nafasi za kazi na ajira kwa kuweka vigezo kama ujuzi wa kazi wa
kuanzia miaka mitano na kuendelea, wakati vijana wengi, kama inavyjulikana,
hawana uzoefu wala ujuzi katika ajira hizo zinazotangazwa ingawa wana uwezo wa
kuzifanya na kuzitekeleza. Ingawa , waajiri wote katika sekta binafsi na umma,
wanaweka masharti au vigezo vya ujuzi na uzoefu kuwa moja ya masharti magumu ya
ajira kwa vijana, wanasahau kuwa
Tanzania tumekosa mpango maalumu wa mafunzo yanayoendana sambamba na
elimu ya kijana, ili kumfanya kijana apate ujuzi katika taaluma yake na katika
sekta inayohusika. Hali hii inasababisha ugumu kwa waajiri, katika kutoa nafasi
za kwa kazi kwa vijana, kwa kuwa kuajiri mtu asiye na ujuzi au uzoefu
inachukuliwa kama ni gharama, kwa kuwa mwajiri lazima aingie gharama za kutoa
mafunzo ya awali tena kwa vijana atakaoajiri. Hii inasababisha waajiri wengi
kukwepa kuwaajiri vijana kwa kigezo cha kupunguza gharama za mafunzo.
Mheshimiwa Spika,
tatizo la ajira kwa vijana pia linachangiwa
zaidi kwa kutokuwa na uoanishaji
mzuri na ushirikiano kati ya taasisi za elimu na mafunzo kwa upande
mmoja na viwanda au soko la ajira kwa upande mwengine. Na hii ni kwa kuwa,
mitaala ya sasa ya elimu na mafunzo haindeshwi kwa kushirikisha wadau wengine,
hasa katika masuala ya kazi na ajira. Mabadiliko makubwa ya kisera yanatakiwa
kufanyika katika sekta mbalimbali ambazo zina msukumo katika kuongeza thamani
ya ya mtafuta kazi kwenye soko la ajira . Kati ya maeneo ya muhimu ambayo
yanatakiwa kufanyiwa mabadiliko ni pamoja na kuazimia kufanya mabadiliko katika
mfumo wa elimu uliopo sasa kwa kufanya
maboresho kwanza; kwa kuhakikisha kuwa elimu ya msingi na sekondari inatolewa
bure kwa watanzania wote. Pili mfumo na
mtaala wa elimu uliopo sasa urekebishwe ili uweze kukidhi mahitaji ya soko la
ajira ambalo huwa linabadilika. Lazima Serikali kwa kupitia wizara ya elimu na
mafunzo ikubali kufanya mapinduzi ya sera ya elimu itakayomfanya kijana wa
kitanzania aweze kuajiriwa popote pale hasa katika jumuia ya Afrika Mashariki.
Lakini pia ni kwa Serikali kuhakikisha mipango na mikakati ya ukuzaji wa sekta mbalimbali inaambatana na uanzishwaji wa kazi na ajira kwa vijana wa
kitanzania. Kila sekta iendane na mipango endelevu ya kukuza ajira kwa vijana.
Kwa mfano ukuzaji wa sekta ya miundombinu, uendane na kutoa nafasi za ajira kwa
vijana wa kitanzania pamoja na kuwalipa mishahara na posho zenye staha,
zitakazowezesha vijana kujikwamua na hali ngumu ya kiuchumi na maisha.
Mheshimiwa Spika,
ushindani wa kidunia, unafanya uchumi wa nchi mbalimbali kuendana na mabadiliko
mbalimbali, hasa mabadiliko ya teknolojia. Hapa nchini, tumeshuhudia mabadiliko
makubwa na mapinduzi ya teknolojia kuanzia kwenye uzalishaji, kilimo, habari na
mawasiliano. Mabadiliko makubwa yanayoendelea katika vigezo na masharti ya
kazi, ni kiashiria kikubwa kuwa vijana lazima wasaidiwe katika kukabiliana na
changamoto za ukuaji wa kasi wa
teknolojia. Hata vijana ambao wanapata fursa ya ujasiriamali lazima wapate
mafunzo ya kukabiliana na ukuaji wa teknolojia.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na ahadi mbalimbali ambazo zilitolewa kipindi cha uchaguzi wa mwaka 2010 za kuongeza ajira kwa vijana na
kukabiliana na tatizo la ukosefu kwa ajira za vijana, ikiwemo kutatua
changamoto za vijana waliopo katika sekta isiyo rasmi ;wamachinga, wachuuzi wa
bidhaa ndogondogo,wakulima wadogowadogo,wasanii,wavuvi,wajasiriamali,mamalishe,
wafanyabiashara ndogondogo, wachimba madini, waliopo kwenye sekta ya utalii;
matumaini ya vijana wengi yalikua ni utekelezaji wa ahadi za Serikali kwa
wakati. Pamoja na taifa kuwa na takribani ya vijana milioni 16, ambapo katika
kupitisha bajeti ya vijana, fedha zilizotengwa kwa ajili ya vijana zilikua ni
kiasi kidogo cha bilioni 3.
Mheshimiwa Spika,
Katika kuweka fursa sawa kwa wote na kuleta usawa katika mgawanyo wa rasilimali
za nchi hii, kwa tengo hilo la fedha za kiasi cha bilioni 3 kwa vijana milioni
16 wa kitanzania, basi kila kijana ana uwezekano wa kupata kiasi cha shilingi
za kitanzania 187.5 kama mtaji.
Mheshimiwa Spika, Huu si upotoshaji kama mnavyouita bali ni
ukweli halisi ambao watanzania leo wanakumbana nao kwa kuwa na Serikali ambayo
haina vipaumbele katika kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana. Kumekua na
ongezeko la vijana wanaojihusisha na biashara za madawa ya kulevya, ujambazi,
ukahaba, hali inayochangiwa na fursa chache za kufikiwa kwa malengo na miradi
mbalimbali ya programu za vijana.
Mheshimiwa Spika,
jitihada za kutengeneza mazingira kwa vijana na watanzania kwa ujumla hasa
wanaofanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi maarufu kama wamachinga, unaleta
changamoto katika uchumi wa taifa letu na katika utatuzi wa migogoro
inayotokana na ukosefu wa ajira nchini. Serikali inatakiwa kuweka mpango
mkakati wa kuoanisha idadi ya vijana ambao wamekuwa wakifanya biashara zao
katika maeneo yasiyokubalika,na
kuwatengea maeneo ambayo yatawakutanisha na wateja wao ili waendeshe biashara
zao bila bughuza kwa wengine. Hii iambatane na mifumo dhabiti ya kuhakikisha
kuwa vijana wanapata fursa ya mikopo katika taasisi za fedha nchini yenye
masharti nafuu.
Mheshimiwa Spika,
kuna haja ya Serikali kuanzisha mpango wa kuwadhamini vijana waliotimiza
masharti ya kibiashara inayoambatana na michanganuo kwa kushirikiana na Benki
ambazo zina matawi mpaka sehemu za vijijini, ili mipango ya kifedha ya
kuwanufaisha vijana iwafikie kwa ukaribu na kwa wakati ili kukabiliana na
tatizo la ajira kwa vijana hapa nchini.
Mheshimiwa Spika,
tatizo la ajira nchini bado ni kubwa sana na linazidi kuwa siku hadi siku huku
kukiwa hakuna ufumbuzi wa kuaminika unaotolewa na viongozi wa nchi.Vijana
wamekuwa wakiendelea kuhitimu katika vyuo mbali mbali nchini huku wakiwa
wanakosa kazi maalum za kufanya na hivyo kujikuta wakiishi maisha ya dhiki na
yasiyotamanika huku wakiwa wamekata tamaa. Katika jitihada za kutatua tatizo la
ukosefu wa ajira nchini,wataalam mbalimbali wamekuwa wakishauri kwamba
suluhisho la kuwanusuru vijana ni kuwahamasisha na kuwajengea mazingira ya
kujiajiri wenyewe kwenye sekta binafsi kama ufundi,kilimo, ujasiriamali na
kadhalika.
Mheshimiwa Spika,
kwa kuwa ni dhahiri kuwa vijana wengi wameendelea kuhitimu elimu ya juu nchini
kila mwaka katika fani mbalimbali. Pamoja na ugumu wa soko la ajira
nchini,lazima Serikali iweke mikakati ya kuhakikisha kuwa kundi hili linapewa
elimu na mafunzo ya kuwawezesha kutumia taaluma zao ili waweze kusaidia kada
mbalimbali nchini.Moja ya mikakati ambayo Serikali inaweza kuitumia ni pamoja
na kuingia ubia na makampuni yaliyo katika sekta mbalimbali nchini ambazo
zitakua zinatoa nafasi za mafunzo ya kazi 'internship' kwa muda utakaopangwa
kama moja ya wajibu wa mashirika kwa umma 'Corporate
Social Responsibility'. Hii si tu itawajengea vijana uwezo wa kujifunza
bila pia italisaidia taifa kutunza thamani ya mtaji rasilimali watu(Human Capital Value) na kuwa taifa lenye
ujuzi na maendeleo ya nguvu kazi (human
resoures development ).Lazima serikali sasa itambue kuwa kundi vijana ndilo
chachu ya mabadiliko ya kila kitu hivyo wakishirikishwa ipasavyo katika sekta
mbalimbali wanao uwezo wa kuliletea maendeleo ya kweli taifa hili.Kama serikali
haitakuwa makini katika kuutafutia ufumbuzi mgogoro huu wa ajira, ni wazi kuwa vijana wataendelea kudai mabadiliko hata kwa
kutumia nguvu pale inapobidi kutokana na ugumu wa maisha na ufinyu wa fursa za
kuwakwamua kimaisha.
6.1 UKOSEFU WA AJIRA KWA
MAKUNDI MAALUMU NA CHANGAMOTO ZAKE ZA KISERA.
Mheshimiwa Spika,
Kambi rasmi ya upinzani inaendelea kuitaka Serikali kuboresha sera za kazi na
ajira, sera za usalama wa mahali pa kazi pamoja na sheria mbalimbali ambazo
zitatoa nafasi na fursa kwa makundi maalumu yalipo katika jamii yetu.
Ukiangalia mifumo mbalimbali ambayo ipo nchini, kuanzia mifumo ya elimu, mifumo
ya kifedha na mifumo ya uendelezaji wa mtaji watu, makundi maalumu hasa
walemavu wamekua wakikumbana na changamoto nyingi ambazo zimewakatisha tamaa.
Soko la ajira na kazi leo, halijawekea mfumo utakaohakikisha kuwa unatoa fursa kwa
walemavu ili nao wapate nafasi zaajira na majukumu ya kazi yatakayoweza
kuwaendeleza na kujikwamua kiuchumi.
Mheshimiwa Spika,katika
mawasilisho ya bajeti kwa wizara hii kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013 , waziri
alieleza kuwa kwa jumla ya watu wenye
ulemavu 308 walipatiwa mafunzo ya ujuzi wa fani
mbalimbali kwa kupitia mafunzo ya ujuzi kwa kushirikiana na wadau kama
CCBRT(Comprehensive Community Based Rehabilitation in Tanzania), CEFA na Radar
Development ambapo kati ya wahitimu hao 145 wameajiriwa na 163 wamejiajiri.
Mheshimiwa Spika,
idadi hii haileti taswira halisi ya makundi maalumu katika jamii ambayo yana
watanzania wenye elimu, ujuzi na utaalamu katika fani mbalimbali lakini
wamekosa fursa za ajira kutokana na hali zao. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka wizara kutoa takwimu ya jumla ya watanzania walio kwenye makundi
maalumu walioajiriwa katika sekta mbalimbali na waliojiajiri pamoja na kutoa
tathmini ya ufuatiliaji wa utekelezwaji wa Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008
katika kuhakikisha kuna usawa wa fursa za ajira na kipato kwa makundi yote.
Kambi rasmi ya upinzani inataka kujua ni kiasi gani cha fedha za maendeleo
amacho wizara imetenga kwa mwaka huu katika kuwawezesha walemavu nchini katika
kukabiliana na changamoto za maisha aidha kwa kuwaanda kujiajiri ama kwa
kuwaongezea ujuzi na maarifa ili waweze kuajiriwa.
6.2 TATIZO LA AJIRA MBAYA KWA
WATOTO NA ATHARI ZAKE
Mheshimiwa Spika,
kwa miaka mingi haki za watoto zinakiukwa hasa katika suala la kuwaajiri
kinyume cha umri wao, ambapo kimsingi ni kosa na ni kinyume na sheria na
taratibu za nchi.Hali hii inachangiwa na ugumu wa maisha hasa kwa watoto
wanaoishi vijijini na wale ambao wamekumbana na athari mbalimbali ikiwemo wale
ambao wazazi wao wamefariki kutokana na ugonjwa wa UKIMWI. Zaidi pia inatokana
na hali mbaya ya umasikini uliokithiri katika familia nyingi za kitanzania,
hali inayomnyima mtoto kufanya maamuzi sahihi kutokana na umri wake na hivyo
kukimbilia kwenye ajira hatarishi kwa misingi ya kujikomboa kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, lakini
ni wazi kuwa watoto walio katika ajira mbaya wananyimwa elimu na fursa ya kukua
na kujenga vipaji na uwezo utakaoweza kuwakwamua wao, familia na jamii zao
kutoka kwenye mzunguko wa umaskini. Tumeshuhudia ajira mbaya za watoto ambao
wengi wanafanya ajira hatarishi na zenye kuleta madhara si tu ya kiafya bali
kisaikolojia ikiwemo ajira za kwenye mashamba makubwa ya kahawa, chai, tumbaku;
ajira za viwandani; ajira za kazi za nyumbani; ajira hatarishi kwenye migodi ya
madini na machimbo na kadhalika. Hii si tu ni hatari kwa taifa ambalo tunasema
watoto ni taifa la kesho, bali kwa mustakabali wataifa ambalo lina amini katika
misingi ya haki na usawa pamoja na kuwalinda watoto dhidi ya mazingira
hatarishi.
Mheshimiwa Spika,katika
kukabiliana na tatizo la ajira mbaya kwa watoto,mwezi Machi mwaka huu ,
Marekani ilitoa ruzuku ya Sh. bilioni 16 kwa Kamati ya Uokoaji wa Kimataifa
nchini (IRC) kwa ajili ya kukabiliana na ajira mbaya kwa watoto katika mikoa ya
Kigoma na Tanga ambapo fedha hizo zitatumikakupitia kwenye mradi mpya
ujulikanao kama ”Wekeza” na kuwa IRC itashirikiana na wabia wake kukabiliana na
ajira kandamizi na za kinyonyaji dhidi ya watoto.
Mheshimiwa Spika,
Balozi Lenhardt alikaririwa akisema kuwa
“Mradi utalenga wilaya sita katika mikoa
ya Kigoma na Tanga ambako kuna
tatizo kubwa la utumikishwaji wa watoto
katika ajira mbaya kwenye shughuli za kilimo na kazi za majumbani na utawahudumia waathirika pamoja na kujenga uwezo wa serikali kulishughulikia
tatizo hilo,”
Mheshimiwa Spika,
pamoja na msaada wa Marekani katika kukabiliana na ajira mbaya kwa watoto,
Serikali kwa kupitia wizara itupatie majibu ni mkakati gani uliowekwa katika
kukabiliana na ajira mbaya kwa watoto katika sehemu mbalimbali za taifa hili
tofauti na wilaya hizo 6 zilizofadhiliwa na Marekani.
7.0 PENSHENI KWA WAZEE WOTE
NCHINI
Mheshimiwa Spika; katika maoni yake kuhusu bajeti ya Serikali
na Ofisi ya Waziri na Wizara ya Kazi na Ajira ya mwaka 2011 na 2012 kwa nyakati
mbalimbali Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA imeitaka Serikali
kuharakisha kuanza kutoa pensheni kwa wazee wote nchini.
Mheshimiwa Spika;
majibu ya Serikali hii inayoongozwa na CCM yamekuwa ni ahadi kwa wazee kwamba
pensheni hiyo itaanza kulipwa kwa kuwa serikali iko katika hatua ya mwisho ya
kufanya utafiti na kuandaa mfumo wa kisheria.
Mheshimiwa Spika;
tarehe 6 Agosti 2012 wakati akijibu maswali bungeni hatimaye Waziri wa Kazi na
Ajira Gaudencia Kabaka akatoa ahadi mahususi kwamba mwanzoni mwa mwaka 2013
ingetungwa sheria ya wazee ambayo pamoja na mambo mengine ingeweka mfumo
madhubuti wa wazee wote kuanza kulipwa pensheni kuanzia mwaka huu wa 2013.
Waziri alilihakikishia Bunge kwamba Serikali iko katika hatua za mwisho za
kuandaa mpango madhubuti wa ulipaji wa pensheni kwa wazee nchini kuanzia mwaka
2013.
Mheshimiwa Spika;
badala ya kutimiza ahadi hiyo huku mwanzoni mwa mwaka 2013 ukiwa umepita bila
sheria husika kutungwa wala pensheni kuanza kulipwa, Rais Jakaya Kikwete
akihutubia kilele cha wiki ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Mkoani Dodoma tarehe
17 Mei 2013 aliagiza Wizara ya Kazi na Ajira kuanza ‘kufikiria’ kuwalipa
pensheni wazee wote na kujiridhisha kabla ya kuanza kutoa mafao hayo.
Mheshimiwa Spika;
kufuatia agizo hilo la Rais, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na
CHADEMA inaitaka Wizara ya Kazi na Ajira itoe taarifa ya kina kwa Bunge kueleza
Mpango Madhubuti ambao ilijibu bungeni kwamba uko katika hatua za mwisho
umeishia wapi na kuwasilisha bungeni rasimu ya mpango huo iliyokuwa tayari
mpaka wakati Waziri alipojibu bungeni mwaka 2012. Aidha, Wizara ya Kazi na
Ajira ieleze juu ya matumizi ya fedha za umma zilizotumika kufanya tathmini na
utafiti ambao Wizara ilieleza katika majibu yake ya wakati uliopita iwapo ni
sasa ndipo wizara hiyo imeagizwa ianze ‘kufikiria’.
Mheshimiwa Spika;
Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaona kauli hizo za Serikali
inayoongozwa na CCM ni za kutowajali wazee na za kuwepwa kuwajibika kutimiza
ahadi kwamba kuwa tathmini na tafiti zimefanywa mpaka na asasi za kiraia na
Serikali kupewa nakala. Aidha, kufuatia tafiti hizo Wizara iliahidi bungeni
kwamba wameanza kuandaa mfumo wa kuorodhesha wazee ikiwa ni sehemu ya kuanza
kuandaa mchakato wa malipo ya pensheni hizo.
Mheshimiwa Spika;
Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali inayoongozwa
na CCM kuanza kutoa kauli ya kuanza kulipa pensheni hiyo kwa Wazee mwaka huu
2013 na kuingiza katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014 kwa kuzingatia maoni
na mapendekezo tuliyotatoa mwaka 2011 na 2012.
Mheshimiwa Spika;
Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitahadharisha Serikali
inayoongozwa na CCM kwamba ahadi hii isipotekelezwa, tutawakumbusha wazee wote
juu ya ahadi alizotoa Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika kilele cha siku ya Wazee
duniani tarehe 1 Oktoba 2010 alipotumia
vibaya nafasi ya kiserikali kutafuta kura za wazee kwa niaba ya CCM ili wazee
wafanye maamuzi sahihi ya kukikataa chama hicho. Kambi Rasmi ya Upinzani
inayoongozwa na CHADEMA inawakumbusha wazee wote nchini kwamba miaka takribani
kumi imepita toka sera ya wazee itungwe mwaka 2003 hata hivyo utekelezaji wake
chini ya Serikali inayoongozwa na CCM umekuwa ni wa kusuasua.
8.0 SHERIA ZA KAZI NA HAKI ZA
WAFANYAKAZI
Mheshimiwa Spika,
tumeendelea kushuhudia kuwepo na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika
maeneo mengi ya kazi. Tatizo hili limechangiwa kwa kiasi kikubwa na wafanyakazi
kutosimamia au kutojua haki zao za msingi kama wafanyakazi na hivyo kusababisha
waajiri kutumia fursa hiyo ya wafanyakazi kutozijua sheria, kuvunja sheria na
haki nyinginezo za kibinadamu.
Mheshimiwa
Spika, Ni muhimu kwa mfanyakazi wa sekta yoyote ile kujua haki zake za msingi
kama mfanyakazi na mwajiri kuziheshimu haki za kila mfanyakazi kama
zilivyoainishwa katika sheria ya kazi namba 6 ya mwaka 2004 na Sheria za
Taasisi za kazi Na.7 ya mwaka 2004. Sote tunatambua kuwa mfanyakazi ni mtu
ambaye ameingia mkataba na mtu, taasisi au serikali.Kimantiki, mkataba,
kulingana na Sheria ya Ajira Na. 6 ya mwaka 2004 kifungu cha 14 ambayo imetoa
aina tatu za mikataba ambayo ni mkataba usio na muda maalum kwa ajili ya
watalaam.Mkataba wenye muda maalum kwa ajili ya wafanyakazi wasio kwenye
taaluma ya utawala na mikataba kwa ajili ya shughuli maalum kwa muda muafaka na
kifungu cha 15 cha Sheria ya Ajira imefafanua kwamba, mikataba yote lazima iwekwe
katika maandishi.
Mheshimiwa Spika,
hata hivyo kuna pengo kubwa la sheria katika kulinda haki za wafanyakazi pindi
kunapotokea uhamisho wa shughuli yaani(Transfer of Undertakings) kwa upande wa
muajiri hususani kwenye sekta binafsi ambapo kumekuwa na migogoro mingi baina
ya pande mbili hizi inayotokana na
mapungufu sheria hii.
Mheshimiwa Spika,
aidha wakati nikiwasilisha hotuba ya kambi ya upinzani ya wizara hii kwa mwaka
2012/2013 kambi rasmi ya upinzani iliishauri serikali kuleta muswada wa sheria bungeni
utakaosimamia maslahi ya wafanyakazi katika suala hili, jambo ambalo
linaonekana ni kitendawili mpaka sasa kwa serikali inayojiita siikivu masikioni
pa watanzania.
9.0 HAKI NA WAJIBU WA
MFANYAKAZI
Mheshimiwa Spika, mwajiriwa ana haki ya kupata likizo ya siku
28- ambapo kifungu cha 31 kinamtaka mwajiri kutoa likizo ya siku 28 mfululizo
kwa kila mwaka wa ajira.Siku 28 hizo zinajumuisha sikukuu iwapo zitaangukia
ndani ya siku hizo, na siku za mwisho wa juma. Mwajiri anaweza kupunguza siku za likizo iwapo
mwajiriwa aliomba mwenyewe likizo fupi za muda na ambazo alipokea malipo.
Mheshimiwa
Spika, Ikumbukwe kuwa katika Sheria Ajira, likizo ni suala la lazima kwa
kila mfanyakazi na tabia ya kuzuiana likizo kati ya mwajiri na mwajiriwa
hairuhusiwi kwani sheria inamlazimisha mwajiri kumlipa mwajiriwa au mfanyakazi
fedha ya likizo, ambayo ni nauli ya mfanyakazi, mke wake na watoto wasiozidi
wanne na wategemezi wawili, Katika
sheria hiyo ya kazi kuna likizo ya uzazi, kifungu 33, ambapo mfanyakazi
atakayekuwa mjamzito anapaswa kutoa taarifa ya maandishi ya miezi mitatu kabla
ya kuanza likizo yake ya uzazi na taarifa hiyo ni lazima iambatanishwe na cheti
cha daktari. Mjamzito anaweza kuanza likizo yake wakati wowote, ilimradi tu
yawe yamebaki majuma manne kabla ya kujifungua .
10.0 MALIPO BAADA YA
KUACHISHWA KAZI
Mheshimiwa Spika,
mara baada ya kuachishwa kazi, mfanyakazi anatakiwa kulipwa mafao yake yote
yanayotokana na ajira yake kwa kipindi chote cha ajira. Malipo hayo ni pamoja
na mapunjo ya mshahara, kiinua mgongo na nauli ya kumsafirisha hadi kituo cha
karibu na nyumbani kwake. Hata hivyo kumekuwepo na usumbufu mkubwa kwa
wafanyakazi wa sekta binafsi na serikali mara baada ya kustaafu
katika kufuatilia na hata kulipwa stahili hizo jambo ambalo ni ukiukwaji
wa sheria ambazo zipo kwa ajili ya kulinda na kuhifadhi haki za wafanyakazi hao
11.0 VYAMA VYA WAFANYAKAZI
NCHINI
Mheshimiwa Spika, uhuru wa vyama vya wafanyakazi nchini unatambuliwa na
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uangalizi wa sheria za kazi na
Mahusiano ya kazi ya mwaka 2004. Uhuru huu una umuhimu sana katika maeneo ya
kazi na historia yake ipo tangu Mapinduzi ya viwanda nchini Uingereza karne ya
19, katika bara la Ulaya na Marekani. Uhuru wa vyama vya wafanyakazi ni msingi
muhimu wa haki za binadamu kwa kutoa haki za kila mmoja, kuunda na kujiunga na
vyama vya wafanyakazi katika eneo lake la kazi, haki ya kugoma na kuandamana na maridhiano /matakwa ya
kitaifa na kimataifa.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo hali hii ni tofauti kwani vyama hivi
vimeendelea kupigia kelele madai na maslahi mbalimbali kupitia vyama vyao
lakini Serikali imeendelea kuwa kimya na kukimbilia mahakamani kunyamazisha
madai/malalamiko yao, jambo ambalo si suluhisho la masuala hayo bali ni sawa na
kujifunika shuka katikati ya mvua kubwa ya mawe huku ukidhani utaikwepa mvua
hiyo.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani tunaitaka na kuishauri serikali
kushughulikia kwa dhati masuala yote ya wafanyakazi ikiwa ni malimbikizo ya
mishahara, kuboresha mazingira mahali pa kazi na bima za afya kwa wafanyakazi.
12.0 TAKWIMU ZA RASILIMALI WATU
NCHINI
Mheshimiwa Spika, katika mkutano wa mwaka wa 47
wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), uliofanyika juni 2012 jijini Arusha, Waziri wa kazi na ajira alisema tatizo la ajira kwa vijana limepungua kutoka
asilimia 12.9 mwaka 2000/2001 hadi asilimia 11.7 mwaka 2006. Waziri Kabaka
alisema kitendo cha wanasiasa kuendelea kusema tatizo la ajira kwa vijana ni
bomu linalosubiri kulipuka, siyo kweli kwani utafiti uliofanywa na wizara yake
kwa kushirikiana na Taasisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), unaonyesha kuwa tatizo
hilo limepungua kwa asilimia 1.2. Waziri aliendelea kueleza kuwa, utafiti
uliofanywa na NBS mwaka 2006, kwa kushirikiana na wizara hiyo umebainisha kuwa
nguvu kazi ya Tanzania ni milioni 20.6 kati ya watu milioni 37.5, kwa wakati
huo.
Mheshimiwa
Spika, Ni wazi hali ya uchumi duniani kwa sasa si nzuri hasa kwa nchi
zinazoendelea, na changamoto kubwa ni hali ya uchumi pamoja na kubadilika kwa
vigezo na masharti katika soko la ajira. Majibu ya serikali kuwa tatizo la
ajira kwa vijana limepungua, kwa kuangalia takwimu za mwaka 2006 halitoi
taswira halisi ya tatizo hili, hivyo kutoa majibu kwa makadirio ya takwimu kuwa
tatizo la ajira limepungua si sahihi. Katika hotuba ya wizara ya kazi na ajira
kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013 waziri wa kazi na ajira alikiri kuwa tatizo la
takwimu za ajira ni changamoto kwa kuwa linaleta picha hasi na aliahidi kuwa
wizara yake kwa kushirikiana na Shirika
la Kazi Duniani (ILO) imempata mshauri mwelekezi anaye andaa mfumo wa taarifa
za soko la ajira utakaokamilika katika mwaka 2012/2013. Na kwa kuwa wakati akijibu swali la Mheshimiwa Naomi Kaihula, tarehe 13 aprili
2011,mheshimiwa naibu waziri wa kazi na ajira alikiri kuwa ni vigumu kupata
taarifa za uwiano wa vijana wanaomaliza shule na vyuo na wanaopata ajira
kutokana na kukosekana mfumo wa utuatiliaji (Trace Study) kamilifu, ambao
ungetuwezesha kufahamu ni vijana wangapi kati ya waliomaliza shule au vyuo
wameweza kuajiriwa. Kutokana na upungufu huo, naibu waziri aliahidi kuwa wizara
inaandaa mfumo wa upatikanaji wa taarifa za soko la ajira,ambao ungeanza
kufanya kazi mwishoni mwa mwaka 2011 na kusaidia kupatikana kwa taarifa hizo.[4]
13.0 WAKALA WA USALAMA NA AFYA
MAHALI PA KAZI (OSHA)
Mheshimiwa
Spika,OSHA ilianzishwa kwa kutumia Sheria ya
Executive Agencies Act, No 30 ya mwaka 1997. Na wajibu wa OSHA ni
kufanya kaguzi na kufuatilia uzingatiaji wa masuala ya usalama na afya na
kuhakikisha kuwa waajiri wanazingatia sheria na kanuni za usalama mahali pa
kazi hasa Sheria ya Afya na Usalama katika Maeneo ya Kazi (OHS)Na. 5 ya mwaka
2003. Mpaka kufikia Mei 2012, jumla ya kesi 16[5]
zilikua mahakamani. Tunaitaka wizara itupe mrejesho wa kesi hizo dhidi ya
waajiri waliokiuka sheria na kanuni za
usalama mahali pa kazi.
Kambi
rasmi ya upinzani inaitaka Serikali kupitia wizara kuiwezesha OSHA kwa kuipatia
rasilimali za kutosha ili iweze kufanya kaguzi zake ikiwemo kutekeleza wajibu
wake wa uainishaji na usajili, ukaguzi wa usalama na afya,tathmini za maafa
yawezayo kutokea mahali pa kazi na athari zake.
Mheshimiwa
Spika, kumekua na matukio mbalimbali ambayo yanatokea nchini ambayo
yanasababisha athari si tu kwa raia wengine bali kwa wafanyakazi ambao wanakua
ni wahanga wa matukio hayo. Katika kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16, jijini
Dar Es Salaam ni kielelezo cha kutofanyika pia kaguzi za usalama na afya mahali
pa kazi. Lazima Serikali ya CCM ikiri kuwa imeshindwa kuhakikisha kuwa mahali
pa kazi ni salama kwa kila mtanzania. Ni fedheha kuwa na wakala wa Serikali
mwenye dhamana ya kuhakikisha usalama na afya mahali pa kazi unazingatiwa
lakini inashindwa kuwa na vitendea kazi pamoja na rasilimali za kutosha kwa
ajili ya kulinda usalama na afya za mahali pa kazi kutokana na ufinyu wa bajeti
na rasilimali kazi.
Idadi ya Mahali pa kazi
zilizosajiliwa kulinganisha na zisizosajiliwa nchini
Year
|
Makadirio
ya Mahali pa Kazi nchini
|
Sehemu
za Kazi zilizosajiliwa
|
%ya
sehemu za kazi zilizosajiliwa
|
2009
|
6,825
|
1,747
|
25
|
2010
|
11,691
|
2,069
|
22
|
2011
|
21,068
|
5,045
|
24
|
2012
|
27,500
|
6,599
|
24
|
Kambi
rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka wizara, kulipatia Bunge majibu ya maswali
yafuatayo kutokana na takwimu zilizopo hapo juu. Je , ni sababu zipi ambazo
zimeifanya OSHA ifanye kaguzi za usalama wa afya na mahali pa kazi bila ya
kufikia nusu ya sehemu hizo? Na kwa kutumia takwimu ambazo waziri alizitoa
katika Bunge hili wakati wa mawasilisho ya bajeti kwa mwaka wa 2012/2013 kwa
kutoa taswira kuwa OSHA imefanya asilimia 85.6% ya kazi zilizopangwa kufanyika
mahala pa kazi, ni wazi kuwa waziri alikua anaupotosha umma kuwa OSHA
imefanikiwa kwenye kusimamia usalama na afya kwa mahali pa kazi, huku ukweli
ukiwa kuwa wizara imeshindwa kwa asilimia 76% kusajili mahali pa kazi nchini,
hali ambayo inaonesha kuwa si kipaumbele cha Serikali hii ya CCM katika kujali
usalama wa watu wake sehemu za kazi.Kambi rasmi inataka kujua ni hatua gani za
kisheria ambazo asilimia 75 ya mahali pa kazi ambazo hazijasajiliwa
zitachukuliwa kama ambavyo sheria inaelekeza kutoa adhabu? Na je Serikali
imeweka mkakati gani wa kuhakikisha kuwa kila mahali pa kazi nchini
panasajiliwa? Na kwa kuwa inakadiriwa kuwa kiasi cha shilingi milioni 600
zinahitajika kwa OSHA ili kuweza
kusajili sehemu zote za kazi nchini, je wizara imetenga kiasi gani kwa mwaka
huu wa fedha wa 2013/2014?
Mheshimiwa Spika,
aidha kambi rasmi ya upinzani inataka kujua pia kama wizara imefanya usimamizi
na tathmini ya kaguzi zinazofanywa na OSHA na kama wamefanya tathmini ya
shughuli za OSHA, ni vigezo vipi vya ambavyo vimetumia katika kupima na
kusimamia utendaji wa OSHA?
14.0 MAPITIO YA UTEKELEZAJI
BAJETI 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MWAKA 2013/2014
Mheshimiwa Spika,
katika fungu 1001 utawala na rasilimali watu katika mwaka wa fedha 2012/2013
zilitengwa jumla ya shilingi 2,780,306,000,
aidha kwa mujibu wa randama ya wizara ni kuwa jumla ya shilingi 705,400,000 zilikuwa ni kwa ajili ya
kulipia pango la ofisi ya wizara ,maji,umeme na simu na hii ni kwa mujibu wa
randama ya wizara shughuli namba D03S01.
Kambi rasmi ya upinzani, inaona
kuwa fedha hizi ni nyingi sana kutengwa kila mwaka kwa ajili ya kulipia pango
la ofisi ya wizara na ikizingatiwa kuwa ni wizara ambayo inasimamia haki za
wafanyakazi ambao kila leo wanalia kutokana na kiwango kidogo cha mishahara ,
tunataka kujua wizara ina mpango gani wa kujenga ofisi zake ili iachane na
mpango wa kulipia mamilioni ya walipa kodi kila mwaka kama pango na ofisi hizo
zijengwe Dodoma kama ambavyo serikali mara zote imekuwa ikisisitiza kuwa ofisi
zake zitajengwa Dodoma kama sehemu ya maandalizi ya kuhamia Dodoma.
Mheshimiwa Spika,
katika fungu hilo hilo la 1001, namba ya mradi D03S08 randama ya wizara inaonyesha kuwa jumla ya shilingi 8,000,000 zilitengwa kwa mwaka wa fedha
2012/2013 kwa ajili ya gharama za safari za waziri na Naibu waziri kwenda
Majimboni na hadi mwezi Mei 2013 jumla ya shilingi 5,600,000 zilikuwa zimetumika kwa ajili ya safari tatu za Majimboni
kwa Mhe.Waziri na Mhe.Naibu Waziri .
Aidha
, kwa mwaka huu wa fedha wizara imeomba kutengewa kiasi cha shilingi 16,710,000 (randama uk 21) kwa ajili ya
kuwezesha safari nne za majimboni kwa Mhe.Waziri na Naibu Waziri ,maana yake ni
kuwa kila safari moja inatumia wastani wa shilingi milioni nne (4,000,000)hata
kwa Naibu waziri ambaye Jimbo lake lipo Ukonga Dar Es Salaam .
Kambi rasmi ya upinzani,
inataka kujua kuhusiana na safari ya waziri Jimboni kwani tunajua kuwa huyu ni
Mbunge wa Viti maalum na hana jimbo hiyo ziara alifanya kwenye Jimbo gani na
fedha za mwaka huu anategemea kwenda kufanya ziara jimbo gani? Aidha , tunataka
kujua fedha wanazolipwa kama posho ya mafuta na Bunge kwa ajili ya kufanya
ziara majimboni huwa wanazitumia kufanya nini wakati wizarani nako wanajitengea
fedha kwa ajili ya kwenda majimboni, ni kwanini wao Mawaziri na Manaibu wawe
wanalipwa mara mbilimbili fedha kwa ajili ya kazi moja ? Pia ni mamlaka gani
huwa inapanga na kuidhinisha viwango hivyo, au kila wizara inajipangia kutokana
na wanavyotaka .
Mheshimiwa Spika,
Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
.......................................
Cecilia Daniel Paresso (Mb)
k.n.y Msemaji Mkuu wa Kambi
Rasmi ya Upinzani-
Wizara ya Kazi na Ajira.
29.05.2013
No comments:
Post a Comment