Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Thursday, April 18, 2013

Mwenendo wa Bunge walalamikiwa



BAADHI ya wananchi wameeleza kusikitishwa na lugha za matusi zinazoendelea kutolewa bungeni na kuhoji hatua ya kiti cha spika kutotenda haki katika kutoa adhabu kwa wabunge wa pande zote. Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya wabunge kutoleana lugha chafu wakati wakichangia hoja bungeni hali iliyomfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kutangaza kutumia askari kuwatoa nje wale watakaoendelea na tabia hiyo. Patrick Enock, mkazi wa Dar es Salaam alisema hatua ya kufanya upendeleo kwa wabunge inayofanywa na spika na naibu wake haitastawisha Bunge hilo. “Spika na naibu wake watende haki ili kuwezesha Bunge kustawi na kwa kufanya hivyo kutawezesha wabunge kujadili mambo yanayowahusu wananchi kuliko ya vyama vyao.

“Ukweli kuhusu Bunge, kinachofanyika ni kama Simba na Yanga tu kwani anayofanya spika ni kama refa ambaye anachezesha mpira na kuegemea upande mmoja, mfano ni kama jana mbunge aliyetoa tusi zito hajakemewa wala kutolewa nje. Je, hao wanaotukanwa nao wakae kimya?” alihoji Enock. Naye Juma Amos, alimwelezea Naibu Spika, Job Ndugai, kuwa ana mfumo kandamizi na kuhoji elimu yake kama inatosha vizuri. Mwananchi mwingine Ramadhani Rashid alisema inashangaza kuona utaratibu uliowekwa na spika ukivunjwa wazi wazi tena na naibu wake aliyekaa kimya wakati Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM) akitoa tusi zito bungeni.


Alisema ikiwa utaratibu umewekwa hakuna haja ya viongozi kufunika kombe mwanaharamu apite (kunyamazia). Alieleza kuwa kuna haja kwa vyombo vya habari kuendelea kuibua mambo yanayotokea ndani ya Bunge ili wananchi waone aina ya wabunge waliowachagua. Alikilaumu kituo cha Taifa cha Utangazaji (TBC) kwa kuacha kuonesha kile kilichoendelea juzi usiku baada ya Naibu Spika kuamuru askari kuwatoa nje wabunge sita wa CHADEMA. Wabunge hao ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Highness Kiwia (Ilemela), Mchungaji Perer Msigwa (Iringa Mjini), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana). Naye Andrew Komu, alisema kuwa vurugu hizo zinatokana na uongozi mbaya unaoelemea upande mmoja wa Spika Makinda na wasaidizi wake.

Mweka hazina wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu nchini (Shivyawata), Abdulrahman Lugone, alisema kuwa tatizo lililopo ni kwamba Bunge linaendeshwa kishabiki zaidi kuliko kuangalia mahitaji ya wananchi. Aliwataka wananchi kuwa makini katika uchaguzi wa mwaka 2015 kuchagua wabunge wa maana, wenye akili timamu na viongozi imara wa kuwasaidia. Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema lugha chafu zinazotolewa na wabunge zinatia kichefuchefu na hazifurahishi hata kidogo.

Dk. Bana alisema Bunge ni mahali patakatifu hivyo kuna haja kwa wabunge kupaheshimu. “Nami ni kama wewe sifurahii kinachoendelea bungeni, wabunge watambue kuwa wao ni waheshimiwa hivyo wana haki ya kulinda hadhi ya uheshimiwa wao wawapo bungeni na popote pale,” alisema.

Source: Ngoromera H. (April 2013). Mwenendo wa Bunge walalamikiwa. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: