JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia wakazi wawili wa Tarafa ya Mang’ula wilayani Kilombero baada ya kukutwa wakisafirisha nyara za serikali kinyume na sheria. Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, John Laswai tukio hilo lilitokea Aprili 15 mwaka huu, saa 6.15 usiku katika eneo la Gerereza la Kiberege katika barabara ya Ifakara –Mikumi. Alisema kuwa jeshi hilo lilipokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuhusu kuwepo kwa watuhumiwa wanaosafirisha meno ya tembo. Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Omary Mshamu (42) na Costa Sululu (35) wote wakazi wa Mang’ula wilayani humo.
Laswai aliongeza kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja walikutwa wakiwa na vipande vya meno ya tembo 14 vyenye uzito wa gramu 38.6 sawa na tembo saba waliouawa, wakisafirisha nyara hizo kwa kutumia pikipiki zenye nambari T 781 PBY na T 670 CGN. Naye Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Udzungwa, Vitalis Uruka alisema kuwa meno hayo yana thamani ya sh milioni 33.4. Uruka alisema kuwa kufanikiwa kwa ukamataji huo kumetokana na kuwepo kwa ushirikiano mkubwa kati ya askari wa hifadhi na Jeshi la Polisi katika kuweka mtego wa kuwanasa majangili hao. Hata hivyo, mhifadhi huyo alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano zaidi ili kuweza kukomesha vitendo vya ujangili vinavyofanywa na baadhi ya wananchi wasio na uadilifu.

No comments:
Post a Comment