Wilaya ya Mbarali imepata hati mbaya ya mahesabu ikiwa peke katika ya halmashauri zote nchini katika mwaka ulioishia Juni 30, 2012, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) imebainisha. Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita, halmashauri hiyo ilifanyiwa ukaguzi maalumu uliofanyika uliohusisha miaka ya fedha ya 2010/11 na 2011/12.
Baadhi ya mambo yaliyojitokeza katika halmashauri hiyo ni kutokuwepo na kumbukumbu za msingi kama vile ya vikao, majina ya wajumbe wa kamati ya ujenzi, stakabadhi na vitabu vya malipo, hati za malipo, taarifa za benki na mengineyo kwa ajili ya fedha zinazokusanywa katika ngazi ya serikali za vijiji.
Pia ilibainika kuwa zabuni kwa ajili ya makusanyo ya mapato ya ndani hazikutangazwa nje ya eneo la halmashauri, kinyume na Kanuni 80 (5) ya Kanuni ya Ununuzi ya Umma ya mwaka 2005.
Kutokana na hali hiyo, ilibainika kuwa mawakala wa kukusanya mapato hawakurejesha ya jumla Sh150,900,133 katika halmashauri kinyume na agizo 38 (1) la Memoranda ya Fedha ya Serikali za Mitaa ya mwaka 2009.
“Katika kiasi hicho jumla ya Sh75,410,000 zilizochukuliwa na watumishi wa halmashauri hazikurejeshwa halmashauri. Tatizo jingine la halmashauri hiyo ni mawakala wa kukusanya ushuru kutorejesha vitabu vitabu vya stakabadhi, ambapo vitabu 1,254 (visivyo na viwango) na vitabu 1,292 (vyenye viwango) hadi kipindi cha ukaguzi Novemba, 2012 vilikuwa havijarejeshwa.
CAG pia alibaini katika halmashauri hiyo jumla ya Sh16,475,000 zilikusanywa kutoka vyanzo mbalimbali, hakukuwa na ushahidi wa mapato hayo kupelekwa benki au kuwepo katika ofisi ya fedha ya halmashauri. Pia halmashauri hiyo ilishindwa kupeleka kiasi cha Sh370 milioni kwenye ujenzi wa bwawa la umwagiliaji Mashalla na Uturo, na kutumia fedha hizo kutekeleza kazi nyingine bila kibali cha Wizara ya Fedha.
“Fedha za nyongeza za Mfuko wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) zilitumika kufanya malipo ya kugushi ya Sh724,633,829,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Madudu mengine katika halmashauri hiyo hayakubanika kwa kuwa hati za malipo zenye jumla ya Sh1,973,200,811 hazikuwasilishwa kwa ajili ya ukaguzi.
Wananchi wanasemaje
Baadhi ya wananchi wa Mbarali wanasubiri kwa hamu kubwa hatua ambazo wahusika watachukuliwa. “Tumezoea kusikia hati chafu,lakini inasikitisha sana kuona kwamba mara nyingi hakuna hatua za maana zinazochukuliwa dhidi ya viongozi ambao wanakula fedha za umma,” anasema mkazi mmoja wa Mbarali, Hosea Magida.
Baadhi ya wananchi wamekuja juu wakitaka wahusika wote wa ubadhirifu na wizi wa mali za umma wanachukuliwa hatua haraka kama kweli Serikali inataka kuona maendeleo nchini.
Wanasema serikali imekuwa ikifanya ukaguzi maeneo mengi kuona namna fedha zinavyotumika, lakini hata baada ya kufahamu, hakuna hatua za kisheria zinazochukuliwa, kitu ambacho kinaondoa maana ya kufanya ukaguzi.
Kanuni za serikali inampa CAG mamlaka ya kufanya ukaguzi maalumu pale anapoona inafaa. Hata hivyo itakuwa na maana zaidi ikiwa CAG atapewa uwezo wa kuwapeleka mahakamani wale wote ambao wanaonekana kutumia fedha na mali za umma isivyo, kwani kujua tu kwamba Mbarali wana hati chafu haina maana.
Source: Mwananchi. (April 2013). Mbarali:Wilaya pekee nchini iliyopata hati. Retrieved from Mwananchi

No comments:
Post a Comment