CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA
kimesema kimeanza mkakati kuhakikisha kinakuwa na mabalozi wa nyumba kumi kwa
kila eneo. Hatua hiyo ni katika kukiimarisha chama hicho kuanzia ngazi ya taifa
hadi kitongoji . Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Wilbrod
Slaa alisema hatua hiyo imeanza kwa kutoa mafunzo kwa viongozi wa ngazi ya
taifa ya chama hicho.
Alikuwa akifungua mafunzo ya kuwajengea
uwezo viongozi wa taifa waweze kwenda kutoa mafunzo ngazi ya kanda ambao nao
wataendelea kutoa elimu hiyo kwenye jimbo kata hadi vijiji. Lengo la chama hicho ni kuhakikisha
kinajiimarisha na kuwa na viongozi wenye kufuata maadili na misingi ya chama na
kujiandaa kushika dola kwa kuwa na uongozi wenye weledi wa hali ya juu,
alisema.
“Sisi hatutaki mwanachama anunue shashada
ya kura, tunajiandaa tunapeleka silaha ya kujiandaa kushika dola na ndiyo maana
tunawaandaa kuhakikisha tunaposhika dola, tunakuwa tayari na viongozi wenye
weledi mkubwa,” alisema Dk. Slaa. Dk. Slaa aliwashangaa watu wanaodai kuwa
M4C imekufa.
Alisema watu hao hawajui kuwa Chadema
imejipanga na ina mbinu za utawala ambazo hazina hila kama baadhi ya vyama
vingine vinavyofanya. “ Navishangaa vyama vingine vinasifika
kwa hila badala ya kuijenga Tanzania na wananchi wake… serikali za mitaa hadi
wilaya ni wizi mtupu sisi tunatengeneza wataalamu wenye uchungu wa kulinda
rasilimali zao,” alisema.
Mkurugenzi wa Oganaizesheni wa chama
hicho, Benson Kigaula alisema inategemewa watafundishwa wakufunzi 30,606 ambao
watavifikia vitongoji vyote nchini. Alisema hadi Oktoba mwaka huu vijiji
18,000 vitakuwa vimefikiwa na kupewa walimu na wakufunzi hao.
Source: Chapewa R. (April 2013). CHADEMA
kuwa na mabalozi nyumba 10. Morogoro. Retrieved from Mtanzania

No comments:
Post a Comment