DENI LA TAIFA
1. Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa
limeongezeka kwa kasi kubwa sana, hali ambayo inatishia ustawi wa taifa kama
halitasimamiwa kwa umakini na haraka. Hotuba ya Waziri wa Fedha inaonesha
kwamba hadi kufikia Machi 2014, Deni la Taifa lilifikia shilingi trilioni
30.563 ikilinganishwa na shilingi trilioni 23.674 la Machi 2013. Hili ni
ongezeko la takribani trilioni 7 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 29 kwa
kipindi cha mwaka mmoja tu.
2. Mheshimiwa Spika, hili ongezeko
la mikopo ya takribani shilingi trilioni 7 kwa mwaka mmoja tu, halijawahi
kutokea katika historia ya nchi yetu. Ongezeko hili la takribani trilioni 7 ni
sawa na bajeti nzima (full budget) ya mwaka 2008/9 ambayo ilikuwa ni shilingi
trilioni 6.839. Ikumbukwe kuwa mwaka 2008/9 ni miaka mitano tu iliyopita.
Ukopaji wa namna hii unatishia uchumi na usalama wa nchi.
3. Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa ripoti za Benki Kuu na hotuba za bajeti za miaka iliyopita
za Mawaziri wa Fedha, deni la Taifa limeongezeka kwa kasi kutoka shilingi
trilioni 9.3 mwaka 2007/8 hadi shilingi trilioni 30.6 mwaka 2013/14. Hii ni
wazi kuwa deni liliongezeka kwa kiasi cha shilingi trilioni 21.3. Serikali
imelipa shilingi trilioni 4 na kufanya fedha zilizokopwa kuwa jumla ya shilingi
trilioni 25.3 katika kipindi hicho cha miaka saba tu. Huu ni ukopaji hatarishi
kwa uchumi wa taifa letu.
4. Mheshimiwa Spika, licha ya
deni hili kuwa hatarishi kwa uchumi wa Taifa, Serikali bado inatajaria kuongeza
deni hilo kwa kukopa shilingi trilioni 4.3 kama ilivyoainishwa katika bajeti ya
mwaka 2014/15.
5. Mheshimiwa Spika, Serikali
imeonesha kushindwa kulipa deni hilo kwa kutumia vyanzo vyake vya mapato,
badala yake imekuwa ikikopa ili kulipa deni. Mfano hotuba ya bajeti ya mwaka
2014/15 imeonesha kuwa katika shilingi trilioni 1.8 zilizokopwa katika
soko la ndani, zaidi ya shilingi trilioni 1.1 zilitumika kulipa madeni ya hati
fungani wakati shilingi trilioni 0.69 tu ziliwekwa kwenye miradi ya
maendeleo. Hiki ni kiashiria cha karibu sana kwa serikali kufilisika.
Kukopa mikopo ya kibiashara yenye riba kubwa ili kulipa mikopo yenye riba ndogo
au kwa uendeshaji wa kawaida wa serikali au taasisi zake ni kiashiria cha
kutosha kuainisha maamuzi yasiyo na uelewa wa kawaida sana wa utawala na
usimamizi wa fedha. (basic business and economic sense). Mikopo ya
kibiashara hutafutwa kwa matumizi ya uwekezaji wenye lengo la uzalishaji.
6. Mheshimiwa Spika, katika uchumi
unaokuwa kwa wastani wa asilimia kati 6.5 na 7 kwa mwaka, ni vigumu sana kuweza
kulipa deni la Taifa linalokua kwa wastani wa asilimia kati ya 15 na 30 kwa
mwaka. Bila kuwa na vyanzo vipya vya mapato au kusamehewa deni hili
itakuwa vigumu sana kuweza kulipa deni hilo kikamilifu. Hii ni kwa sababu
uwiano wa ukuaji wa uchumi hauendani na kasi ya ukuaji wa deni hata kidogo.
Pamoja na upungufu wote huu, Serikali imeendelea kujitapa kuwa inakopesheka, na
hivyo kuashiria kutokuwepo na hofu yeyote ya kukopa huku holela.
7. Mheshimiwa Spika,
kinachosikitisha zaidi ni kuwa sehemu kubwa ya mikopo hii inakopwa katika
soko la ndani. Hali hii imekuwa ikileta ushindani mkubwa kwa wananchi na
wajasiriamali wanaotaka kukopa ili kukuza mitaji. Hali hii hufanya riba za
mabenki kushindwa kushuka na hivyo kuwaathiri wakopaji na uchumi wa nchi kwa
ujumla. Kwa maneno mengine, serikali imekuwa inazuia wajasiriamali wasikope kwa
riba za bei nafuu, hivyo kufanya baadhi ya wanaokopa kwa riba zilizopo, ambazo
ni kubwa kufilisiwa. Hali hii hurudisha biashara nyuma na inainyima serikali
fursa ya kukuza uchumi na kukusanya mapato zaidi.
8. Mheshimiwa Spika, mataifa mengi
duniani yanakopa na yana madeni makubwa. Suala la msingi la kutofautisha
nchi moja na nyingine ni kasi ya kukua kwa deni husika na matumizi ya
mkopo huo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inauliza na kutaka majibu kutoka kwa
Serikali matumizi ya fedha zilizokopwa na nchi yetu ndani ya miaka 7 ni yapi na
yameleta maendeleo kiasi gani kwa Taifa ( value for money).
TOFAUTI KATI YA BAJETI YA SERIKALI NA
BAJETI MBADALA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KWA MWAKA 2014/2015.
|
BAJETI MBADALA YA KAMBI YA UPINZANI
2014/2015
|
BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2014/2015
|
1
|
Bajeti
isiyo na Mikopo ya kibiashara hivyo bajeti inalenga kulipunguzia taifa mzigo
wa madeni.
|
Bajeti
ya Serikali ina mikopo yenye masharti ya kibiashara ya shilingi trilioni 4.3 na hivyo bajeti hii inawaongezea wananchi
mzigo wa madeni.
|
2
|
Bajeti
inayoendelea kusisitiza umuhimu wa kuwalipa pensheni wazee wote nchini wenye
umri wa miaka 60 na kuendelea.
|
Bajeti
ya Serikali iko kimya kabisa kuhusu malipo ya pensheni kwa wazee wote nchini.
|
3
|
Bajeti
inayoendelea kusisitiza kushusha kiwango cha
tozo ya kodi ya mapato ya ajira kwa wafanyakazi (PAYE) hadi kufikia asilimia
9.
|
Bajeti
ya Serikali imeendelea kuwakandamiza wafanyakazi kwa kutoza asilimia 12
ya kodi ya mapato ya ajira (PAYE) kwa wafanyakazi.
|
4
|
Bajeti
ya Upinzani imeainisha vyanzo vipya
vya mapato ya ndani na hivyo
inayojitegemea kwa asilimia 84.38
|
Bajeti
ya Serikali ni tegemezi kwa asilimia
36.4 kutokana na kukopa kwa kiwango kikubwa na hivyo kuongeza deni la taifa.
|
5
|
Bajeti
Mbadala, mapato ya ndani ni asilimia 34.55 ya pato la Taifa
|
Bajeti
ya Serikali, mapato ya ndani ni asilimia 23 ya pato la taifa.
|
6
|
Bajeti
inayolenga kupunguza misamaha ya Kodi hadi kufikia asilimia 1 ya Pato la
Taifa ili kuongeza mapato ya ndani.
|
Bajeti
ya Serikali imetaja tu azma ya kupunguza misamaha ya kodi lakini haijataja ni
kwa asilimia ngapi ya pato la taifa wala haijaainisha watakaofutiwa misamaha
hiyo.
|
7
|
Bajeti inayolenga kutekeleza
kikamilifu miradi ya maendeleo kwa
kutenga asilimia 42.67 ya bajeti
yote kugharamia miradi ya maendeleo.
|
Asilimia 22 ya Bajeti yote ya Serikali inakwenda kulipa deni la Taifa na asilimia
67.5 ni matumizi ya kawaida. Hivyo
miradi ya maendeleo haijapewa kipaumbele.
|
8
|
Bajeti inayolenga kukusanya mapato kutoka
kwenye vyanzo ambavyo havimuumizi mwananchi wa kawaida
|
Bajeti ya Serikali imelenga kukusanya
mapato kutoka katika bidhaa zinazotumiwa kila siku na wananchi kama vile
vinywaji na hivyo kuwaongezea wananchi ugumu wa maisha.
|
9
|
Matumizi ya Kawaida ni asilimia 57.33 tu
ya bajeti yote
|
Matumizi ya Kawaida ni 67.5%
|
10
|
Bajeti ya kumsaidia mwananchi wa kawaida
kutoka katika wimbi la umaskini.
|
Bajeti isiyo mtambua mwananchi maskini na
kuongeza matumizi makubwa kwa watawala.
|
|
|
|
No comments:
Post a Comment