WIMBI la matumizi mabaya ya fedha za umma limezidi
kukiandama Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo hivi sasa kinatuhumiwa kutumia
fedha za umma katika ziara na ukaguzi wa miradi. Tanzania Daima imedokezwa kuwa kila ziara ya CCM
inakofanyika, mkurugenzi wa halmashauri husika hutoa magari au fedha za
kuwakirimu wahusika. Imedokezwa kuwa miongoni mwa ziara ambazo zinatumia fedha
za halmashauri ni inayofanywa hivi sasa mikoani na Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana. Inaelezwa kuwa ziara hizo hazipaswi kugharimiwa na fedha
za serikali kupitia halmashauri mbalimbali kwakuwa zinatokana na wananchi wenye
itikadi tofauti pamoja na wasio na itikadi.
Michango hiyo ndiyo inadaiwa kuwapa nguvu vigogo wa CCM na
kuacha kupitisha bakuli kuomba misaada kwa makada wake kama ilivyozoeleka siku
za nyuma. Tanzania Daima limedokezwa kuwa vyama vya upinzani na CCM
vimekuwa na utaratibu wa kuomba misaada kwa makada wao au wahisani, wafadhili
wa ndani na nje ya nchi. Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni utaratibu huo
unaonekana kutumiwa zaidi na wapinzani kutokana na kutokuwa na uwezo wa
kuwaamrisha au kuwashawishi wakurugenzi wa halmashauri kugharimia ziara zao. Tanzania Daima liliwasiliana na Katibu wa Itikadi na
Uenezi, Nape Nnauye, ambaye alisema kuwa taarifa hizo zinalenga kukichafulia
jina chama tawala. “Madai hayo ni ya kiupuuzi na kwamba misafara yetu
inawaumiza viongozi wa CHADEMA, sisi tunapoamua jambo tunakuwa na mipango
sambamba na kujitosheleza,” alisema.
Hata hivyo, Tanzania Daima limepata taarifa kuwa baadhi ya
halmashauri ambazo Kinana na timu yake wameshapita ziligharamia malazi, chakula
na usafiri wa ndani ikiwemo magari ya serikali kutumika. Halmashauri ambazo taarifa zake zimekusanywa na gazeti
hili ni pamoja na Nzega, Igunga na Uyui zilizopo mkoani Tabora na Iramba
iliyopo mkoani Singida huku wakurugenzi wake wakikiri kutumia magari ya
serikali na baadhi ya watumishi kuhudhuria katika ziara hiyo. Katika Wilaya ya Igunga, msafara wa Kinana ulikaa kwa muda
wa siku tatu ambapo halmashauri kupitia viongozi wa CCM wa wilaya hiyo
waligharimia usafiri wa ndani, chakula na malazi pamoja na kukodisha pikipiki
50.
Kigogo mmoja wa CCM, alidokeza kuwa walitakiwa kuandaa
chakula cha watu 200 huku sahani moja ya chakula ikiuzwa kwa shilingi 5,500. Alisema walikodisha pikipiki 42 kwa sharti la kila mwenye
pikipiki aliyehudhuria mapokezi ya Kinana, atalipwa sh 7,000 na kuwekewa lita
mbili ya mafuta. Alibainisha pia walitakiwa wahakikishe msafara wa Katibu
Mkuu unapatiwa malazi. “Sisi chama tulibeba jukumu lile kwa kuwa ni ugeni wa
chama, lakini hakuna hata senti moja tuliyotumia kutoka mfuko wa chama zaidi ya
fedha hizo kutoka ndani ya halmashauri yetu,” alieleza mtoa habari wetu kutoka
Igunga. Katika Wilaya ya Nzega, Uyui na Iramba, msafara wa Kinana
ulipatiwa mafuta ya magari na chakula kwa fedha zilizotoka katika halmashauri
na kukabidhiwa viongozi wa CCM wa wilaya, huku suala la malazi likiachwa kuwa
jukumu la waliokuwa katika msafara.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti,
wakurugenzi wa wilaya zilizofanyiwa uchunguzi walikanusha kugharamia ziara
hizo, lakini wakikiri kutoa magari yaliyozunguka katika miradi iliyokuwa
ikikaguliwa na Kinana. Mkurugenzi wa Wilaya ya Igunga, Rusika Turuka, alipoulizwa
juu ya halmashauri yake kugharamia ziara ya Kinana, alitaka apewe muda kwa
maelezo kuwa yupo katika mkutano na hata alipopigiwa tena simu hakupokea. Mkurugenzi wa Wilaya ya Nzega, Abraham Mndeme, alikiri
ofisi yake kutoa magari yaliyowabeba watumishi wa serikali na madiwani wa
CCM kuongozana na Kinana katika ziara hiyo wilayani mwake. Mndeme, alisema ugeni uliofika katika wilaya yake ni wa
kitaifa, na kwamba miradi iliyohitaji kukaguliwa ni ile iliyosimamiwa na
halmashauri ya wilaya.
“Walioambatana na msafara wa Kinana ni madiwani na sisi
tulitoa magari ya kuwasafirisha kwenda kwenye miradi na kwa watendaji mimi
nilitumia gari moja na mhandisi wa manispaa,” alisema Mndeme. Mkurugenzi wa Wilaya ya Uyui, Hadija Mkauani, alipoulizwa
juu ya kugharamia ziara ya Kinana, alimuomba mwandishi akutane nae ofisini na
alipoambiwa simu inapigwa kutoka Dar es Salaam alikata simu. “Baba naomba tuonane ofisini tuweze kuongea vizuri hayo
mambo au umtume mwakilishi wako hapa mkoani si mnaye huku, tutaongea vizuri
tu,” alisema Mkauani. Kaimu Mkurugenzi wa Iramba, Mariam Mpita, alisema gharama
za ziara hiyo zilibebwa na CCM huku yeye, watendaji wa halmashauri hiyo
waliambatana na Kinana kukagua miradi ya maendeleo.
Nape afafanua
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, badala ya
kujibu hoja ya ziara zao kutumia fedha za umma aliilaumu CHADEMA. Alisema ziara zao zinawaumiza CHADEMA waliokuwa wakifanya
ziara za aina hiyo ili kujiimarisha, lakini sasa wanaona zinafanywa na CCM
wanahofia kuanguka mwaka 2015. “Hata mtoto wa darasa la kwanza akisikia hayo madai atajua
ni upuuzi, lakini ulizeni halmashauri iliyochangia hata shilingi moja. Najua
ziara hizi zinawaumiza sana CHADEMA,” alisema. Alipoulizwa kama ziara yao ina lengo la kuwaumiza CHADEMA
au kuangalia changamoto zinazowakabili wananchi, na CCM itakavyoishauri
serikali kutatua yatakayobainika, Nape alisema swali aliloulizwa ni fikra za
kijinga za CHADEMA.
Nape alisema CHADEMA hawana ujanja wa kukwepa kifo chao,
huku akisema uzushi na uongo hautawasaidia kupona. Wakati Nape akikana halmashauri hizo kugharamia ziara za
chama hicho, wiki iliyopita katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Jiji la
Arusha, Mkurugenzi wa jiji hilo, Juma Idd, alikiri kufanya hivyo. Idd, alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu maswali ya
madiwani wa jiji hilo waliohoji sababu za ziara za madiwani au viongozi wa CCM
kutumia magari ya halmashauri. Idd, alisema walitoa magari hayo ikiwa ni utekelezaji wa
maelekezo ya serikali iliyotaka viongozi wa CCM kupita kukagua utekelezaji wa
ilani yao. Alisema kuwa jiji walitoa wataalamu
na gari kwa ajili ya kwenda kutoa ufafanuzi juu ya miradi hiyo.
Khamis A. / Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment