Kelele, kukunjana na kunyoosheana vidole jana mchana vilitawala nje ya ukumbi wa Bunge wakati wabunge wa CUF kutoka Zanzibar walipotaka ‘kumkanya’ Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy. Sakata hilo la aina yake lililodumu kwa takriban dakika 15 lilitokea saa 7:05 mchana baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuahirisha kikao cha Bunge. Wabunge hao Mussa Haji Kombo (Chakechake), Kombo Khamis Kombo (Magogoni) na Muhammad Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe), walitaka ‘kumkanya’ Keissy kutokana na kile alichosema alipokuwa akichangia Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mwaka 2014/15 na kusema Zanzibar haichangii katika Muungano, hivyo haina haki ya kuhoji mambo ya upande wa pili. Kauli hiyo licha ya kulalamikiwa na wabunge wote wa CUF kutoka Zanzibar kiasi cha kufikia hatua ya kusimama na kuomba mwongozo wa Spika, Keissy alizidi kuwashambulia na kusema kuwa majimbo ya Zanzibar watu wake wanaweza kukusanywa sehemu moja kwa kupigiwa filimbi tu.
“Nyie Zanzibar idadi yenu ya watu ni asilimia 2.8 ya watu wote wa Tanzania. Sasa mnataka kupata kila kitu sawa ili iweje! Mnataka ajira asilimia 21 na Watanganyika wakafanye kazi wapi?” alisema Keissy. Baada ya kuahirishwa kwa kikao hicho na wabunge kuanza kutoka nje, wabunge hao wa CUF walikwenda kumsubiri Keissy karibu na jengo la kantini. Mbunge wa kwanza kumvaa Keissy alikuwa Khamis Kombo ambaye kabla ya kumfikia alizuiwa na Mbunge wa Mpanda Kaskazini (CCM), Moshi Selemani Kakoso. Wakati Keissy akishangaa alitokea Haji Kombo ambaye naye alizuiwa na Mbunge wa Mikumi (CCM), Abdulsalaam Selemani Amer. “Mimi sitaki kupigana bwana ninachokijua ni kwamba nilikuwa nikichangia mjadala wa bajeti na nilichokisema ni ukweli mtupu,” alisema Keissy huku akiwa amenyanyua mikono yake juu na kuondoka eneo hilo.
“Wewe (Keissy) sijui una nini wewe. Unapenda kutufuata fuata sana watu wa Zanzibar. Hivi una nini wewe? Hivi hujui kuwa Tanzania ni Muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar?” alisikika akisema Khamis Kombo. Kwa upande wake, Sanya hata baada ya wenzake kutawanyika eneo hilo, aliendelea kumlaumu Keissy na kuwataka wabunge wa CCM kumuonya. “Anapenda sana kutoa kauli mbaya dhidi ya Zanzibar. Jamani mkanyeni mwenzenu haiwezekani kila siku awe yeye tu anayetukashifu bungeni,” alisema Sanya huku akitulizwa na mbunge wa Kibiti (CCM), Abdul Jabiri Marombwa. Baadaye Keissy alisema: “Nimesema ukweli kabisa hakuna jambo hata moja la uongo. Sina kosa hata kidogo kwa sababu nimeonyesha ujasiri kwa kusema ukweli.” Kwa upande wake, Haji Kombo alisema: “Ana kauli za kibaguzi sana na tulitaka kumkanya tu na siyo kumpiga.” Alisema mbunge huyo amekuwa akitoa kauli za kibaguzi na kwamba walimvamia kutokana na kupandwa na jazba. “Ndiyo maana siku zote tunasema Muungano wa Serikali mbili siyo muungano kabisa, ni bora Serikali tatu, alichokifanya si kitu kizuri.”
Sakata lilivyoanza
Sakata hilo lilianza wakati Haji Kombo akichangia bajeti ya Mambo ya Nje na kueleza kuwa Zanzibar haitendewi haki katika uteuzi wa mabalozi nje ya nchi, akisema haiwezekani iwe na asilimia 1.3 ya mabalozi 34 wa Tanzania. “Bajeti hii ipo katika mambo ya Muungano lakini Zanzibar ina mabalozi wanne tu, huku ni sawa na kuoneana. Tanganyika inaifanya Zanzibar kama koloni lake. Ndiyo maana tunasema Tanganyika imevaa koti la Muungano,” alisema Kombo. Ilipofika zamu ya Keissy kuchangia mjadala huo alisema: “Idadi ya Wazanzibari ni asilimia 2.8 ya Watanzania wote na wala hamchangii gharama ya Muungano kwa miaka 20 sasa. Hao mabalozi wanalipwa kwa kodi za wananchi wa Nkasi, Biharamulo na Dar es Salaam.” Keissy alimtaka Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe atakapokuwa akijibu hoja za wabunge aeleze, Zanzibar inachangia kiasi gani katika Muungano.
“Mnasema upande mmoja umevaa koti la Muungano, hata sisi (Tanganyika) koti hilo limeshaanza kutubana. Kama koti limewavaa amueni moja njia mbona nyeupe, acheni chokochoko zenu,” alisema Keissy na kuongeza: “Fedha za mfuko wa jimbo mnachukua mara mbili (kwenu na Bara). Kwanza jimbo moja la Zanzibar ni kama mawili ya jimbo la Nkasi na hata ukitaka kuwaita watu wake unapiga filimbi tu wote wanakusanyika.” Keissy alizidi kuwapandisha hasira wabunge hao baada ya kuwaeleza kuwa Zanzibar hailipi umeme unaotoka Bara. “Usimchokoze mwehu halafu unakimbilia nyumba ya vioo. Sisi pia tuna uchungu na nchi yetu, hatuna maji wakati kwenu mnasema kila mtu anapata maji na umeme.” Baada ya kauli hiyo Haji Kombo aliomba mwongozo kwa Spika na kabla ya kupewa ruhusa, Keissy alisikika akisema, “Toa taarifa nitakujibu.”
Katika mwongozo wake Kombo alisema, “Nchi hii haina wendawazimu namna hii. Hii ni nchi yenye heshima na watu wanaoheshimiana.” Kauli hiyo ilimchefua Ndugai ambaye alimkatisha Kombo na kumtaka aeleze mwendawazimu ni nani. “Mwendawazimu ni mtu anayesema maneno yasiyo na busara. Wazanzibari siyo watu maskini na wameingia katika Muungano kwa masikitiko makubwa. Kati ya Watanzania milioni 45, Wazanzibari wapo milioni 1.3 tu,” alisema Kombo na kuongeza: “Hakuna chochote mnachotusaidia. Ni aibu mbunge wa CCM, chama ambacho kimekubali kuungana na Zanzibar kuzungumza maneno kama haya. Naomba mwongozo wako Mheshimiwa Spika, mwambie (Kessy) asivuke kuja Zanzibar.” Hata hivyo, Ndugai aliukataa mwongozo huo kwa maelezo kuwa ulikuwa ni taarifa tu na kumtaka Keissy kujibu taarifa hiyo. “Siikubali hiyo taarifa na namwona yeye ndiyo mwendawazimu zaidi.”
Kessy alisema lazima Zanzibar ichangie Muungano kama inataka kuwa na idadi sawa ya mabalozi kauli ambayo iliwafanya wabunge wa CUF kutoka Zanzibar kusimama, huku Mbunge wa Ole, Rajab Mbarouk Mohamed akiomba mwongozo. “Jamani niacheni nizungumze mbona nyinyi mlizungumza na mkaachwa. Subirini nimalize kuchangia mwiba unatokea ulipoingilia, vumilieni tu na kama hamtaki tokeni nje,” alisema Keissy. Ndugai aliingilia kati na kusema, “Naona mmeamua kuleta mada ya Bunge Maalumu la Katiba la Mheshimiwa Sitta (Samwel). Subirini litakapoanza.”
Sauwa S., & Butahe F. / Mwananchi
No comments:
Post a Comment