‘Mbaazi ikikosa Maua, Husingizia Maua’
Na Bryceson Mathias
SERIKALI, Viongozi na Chama kilichopo madarakani kisitafute mchawi na badala yake kijilaumu kwa kuwepo kwa Katiba ya Zsnzibar.
Ifike mahali, tusiwalaumu wanaodai Serikali Tatu ikiwemo ya Tanganyika, kwa sababu Serikali hiyo hiyo ndiyo iliyotoa ruhusa na hoja dhaifu zilizoshawishi marekebisho ya kumi ya Katiba ya Zanzibar kwa madai hazikuwa na mashiko ya kujenga utaifa.
Pamoja na Chama cha Mapinduzi kudai hoja hiyo ilikuwa na sababu za kuleta mpasuko usiokuwa na tija kwa Watanzania, ukweli halisi ni kwamba, marekebisho hayo ndiyo yaliyoitambua Zanzibar kuwa nchi; Na Tanganyika kuachwa Solemba.
Makosa ambayo pande zote mbili za Muungano zinabidi kuyajutia kwa kukosa umakini na kwamba katu zisifike mahali zikahisi kuwa ongezeko la mambo likiwemo la madai ya Serikali Tatu ikiwemo ya Tanganyika ni kuzikandamiza.
Kwa mujibu wa marekebisho hayo, Zanzibar ilitambuliwa kuwa nchi na kumpokonya mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ugawaji wa mikoa na wilaya kisiwani humo, na kumpa mamlaka hayo Rais wa Zanzibar.
Ni hoja iliyowazi kuwa, baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki 1977, sehemu zote mbili za Muungano hazikuona ukweli ni upi wenye tija mpaka kufikia muundo ulioleta mgogoro wa kikatiba uliopo mpaka sasa.
Sababu nyingine ya wazi iliyopelekea majuto hayo, ni kufanya marekebisho hayo bila ushirikishwaji wa watanganyika, ikiwa ni pamoja na msukumo wa kisiasa kutoka kwa vyama vya upinzani na waau, hasa ukizingatia nchi yetu sasa ni ya mfumo wa kidemokrasia.
Ni vyema Serikali na CCM vilivyoko madarakani vikakumbuka athari za Uzanzibari na Uzanzibara zilizoelezwa na Mwalimu Julius Nyerere, badala ya kumcharukia jaji Joseph Sinde Warioba, aliyteuliwa na Rais Jakaya Kikwete huku akijua Changamoto zake.
Hata Katibu wa CCM Abdlahamani Kinana anapompinga Jaji Wariobahii ya Rasimu ya pili ya Marekebisho ya Bunge Maalum la Katiba, hazina mashiko kwa sababu Kinana anaufahamu ukweli halisi wa Ulinzi wa Tanzania Bara na Z’bar akiwa Askari, ila anaukingia Mgongo.
Kinana kupinga mapendekezo ya muundo wa Serikali tatu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Warioba, akisisitiza kuwa waziri huyo mkuu wa zamani anatakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu hoja zilizofichika. Hoja hizo Kinana anazijua fika anawazingua wasiomjua.
Nisingependa kuzungumzia Jinsi Kinana anavyoifahamu Hoja ya Z’bar wakati akiwa jeshini lakini nataka nisema, ‘Kama hata sahihi ya Mwalimu Julius K Nyerere inaweza kufojiwa Serikali na CCM kikitawala, nani alaumiwe ka si Rais, Katibu wa Chma kinachotawala?
Nani Mbaya na Muovu kati ya Jaji Warioba aliyeteuliwa, akatumwa kazi, ambayo kimsingi ameifanya kwa uadilifu si kwa kujifungia pekee yake akaandika aliyosema bali ni maamuzi ya Tume?
Uaadilifu wa Tume ya Warioba, ndiyo unaoiitesa CCM na Viongozi wake!.
Suala la Kinana kuendelea kumchokonoa Jaji Warioba, halina mashiko kwa sababu aji Warioba alishaeleza kila kitu bungeni, ambacho Viongozi wa Serikali katika Ofisi katika mahojiano na tume walisema kwa maandishi.
Binafsi naona hali ya Kuchezewa na Kughushiwa kwa Sahihi za Waasisi wa Mungano wa Tanzani Bara na Zanzibar, ni mbaya zaidi kuliko hatua ya Warioba kuwasilisha mawazo halisi ya walichosema wananchi.
Tusifanye kazi na Tabia ya Mbaazi, Ikikosa Maua husingizia Jua
No comments:
Post a Comment