Katika karne iliyopita, wasomi mbali mbali wakiwepo wanauchumi, pamoja na wataalamu wa maswala ya kijamii waligundua umuhimu wa rasilimali watu katika kukua kwa uchumi wa dunia. Kuwepo kwa elimu bora, na ujuzi katika nafsi ya binadamu huwasaidia watu kujitengenezea vipato vikubwa. Tanzania inahitaji idadi kubwa ya rasilimali watu ili iweze kupiga hatua kubwa za kiuchumi.
Kuwepo kwa mali asili kama madini, mafuta na gesi asilia kwa kiwango kikubwa imekuwa laana kwa mataifa kwani yamekuwa vyanzo vya unyanyasaji wa kijamii na umasikini uliopitiliza kwa jamii zisizokuwa na rasilimali watu ya kutosha ili kuzisimamia na kuziendeleza.
Baada ya vita vya pili vya dunia, Ujerumani ilikuwa katika wakati mgumu wa kujinyanyua kiuchumi. Miundombinu mingi iliharibiwa kipindi cha vita. Na Ili kujinyanyua kutoka katika uharibufu mkubwa uliosabishwa na vita, serikali ya Ujerumani ilibuni mfumo wa elimu ambayo ilielekeza juhudi zake katika kutayarisha rasilimali watu.
Elimu ilipewa kipaumbele; Ilifanywa kuwa ya bure na ya lazima kwa kila mjerumani. Mfumo huu wa elimu ulifanywa kuwa wa vitendo zaidi na lazima kwa kila mtoto mwenye umri wa miaka tano hadi kumi na tisa, huku kila mwanafunzi akipewa nafasi kuchagua cha kujifunza kutokana na uwezo wake lengo kubwa ikiwa ni kutayarisha rasilimali watu
Jitihada hizi za serikali ya Ujerumani ilizaa matunda makubwa ambayo yaliitwa miujiza ya kiuchumi. Leo, uchumi wa Ujerumani ndio uchumi mkubwa zaidi katika bara la Ulaya, na pia ndio mdhamini mkubwa wa mataifa taabani kiuchumi kama Ugiriki, Hispania nk. Ujerumani ni moja ya mataifa yaliyo juu zaidi kwenye maswala ya uhandisi inaongoza kwa uhandisi. Ujerumani inaongoza kwa uzalishaji wa viwanda ikiuza nje ya nchi bidhaa yenye thamani ya dola za kimarekani trillion 1.52 kwa mwaka 2012 tu. Haya ni mafanikio yaliyotokana na kuipa elimu kipaumbele, pamoja na matumizi ya rasilimali watu zilizoko ndani na nje ya nchi
Mataifa yasiyokuwa na mali asili nayo yameonyesha ubunifu wa hali ya juu. Israel kwa mfano, ni taifa dogo lenye rasilimali chache, huku ikizungukwa na maadui ambao lengo lao kubwa ni kuliangamiza. Ikiwa imezingirwa na maadui kila kona pamoja na kukosa rasilimali za asili, Israel imelazimika kutumia rasilimali watu ili isiangamizwe kijeshi na kiuchumi.
Licha ya kujitengenezea baadhi ya taasisi bora za kielimu na utafiti duniani, Israel iligeukia wataalamu wenye asili ya kiyahudi waliotapakaa katika kila pembe ya dunia, ikiwapa uraia watu wote wanaotaka kurudi nchini humo. Leo Israel ndio moja ya nchi iliyoendelea zaidi kiteknolojia. Vyuo vikuu vya Israel vimezalisha wataalamu wa kila aina ambao wanasaidia nchi hiyo kujiendeleza kiuchumi na kujilinda kijeshi
Baada yakugundua kwamba hatma yake haikuwa nzuri kiuchumi na kijamii, Singapore, nchi ndogo barani Asia ilianzisha mapinduzi ya miundombinu , viwanda, mawasiliano, na ya kielimu ili iweze kustahimili mabadiliko ya kiuchumi ya baadae. Leo, Singapore ni nchi ya nne duniani kwenye maswala ya kifedha na mmoja wa magwiji katika masoko yanayochipukia. Korea kusini nayo haina tofauti na Singapore, kwani ilikuwa masikini zaidi ya Kenya mwaka 1960. Leo hii Korea ya Kusini ina uchumi wenye thamani ya dola za kimarekani trillion 1.56 ambayo ni mara 47 ya Kenya. Hii yote imetokana na jitihada zake za kuzalisha rasilimali watu
Marekani imekuwa ni taifa lenye nguvu zaidi ya nchi yoyote ile duniani kiuchumi, kiteknolojia na kijeshi. Kwa kipindi kirefu sasa. Mapinduzi ya viwanda ya karne ya 19 iliisukuma nchi hiyo kutumia kila mbinu ; Marekani ilitumia rasilimali zake zote ikiwemo rasilimali watu. Mafanikio ya taifa hili kubwa duniani hayakuwa ya kubahatisha, yametokana na kufanya kazi kwa bidii bila kukata tamaa, na pia kujivunia kile wanachokifanya.
Wamarekani wamewekeza kwenye elimu kwa kiwango kikubwa. Wameanzisha vyuo vikuu vya elimu na utafiti bora kuliko zote duniani. Sera zao za uhamiaji zimekuwa kivutio kwa wataalamu bora kutoka kila pembe ya dunia ili tu watu wenye vipaji waendelee kusadia taifa hili kuendelea kuongoza kiuchumi. Hazina kubwa ya Tanzania imetapakaa ulimwenguni. Wataalamu mbali mbali wenye asili ya kitanzania wametapaa kila pembe ya dunia wakitafuta maisha huku wakichangia maendeleo ya mataifa mengine kutokana na kukosa uhuru wa kuchangia nchi yao ya kuzaliwa.
Wataalamu wenye asili ya Kitanzania wapo katika taasisi kubwa za kitafiti nchini marekani na mataifa mengine makubwa; wapo kwenye mashirika makubwa ya kifedha, wapo kwenye taasisi kubwa za afya nk. Mifano ni mingi ambayo siwezi kuielezea yote kwa leo, ila lengo langu ni kuielemisha jamii yetu kuhusiana na umuhimu wa watanzania waishio ughaibuni
Ushindani mkubwa wa kiuchumi katika eneo la maziwa makuu ni msukumo tosha kwa Tanzania kutumia kila mbinu inayoweza kuwa mstari wa mbele tukizingatia kwamba, Tanzania ni moja ya nchi chache barani Afrika yenye utajiri mkubwa; kwani imebarikiwa na kila aina ya rasilimali muhimu ambazo zingesaidia kuharakisha maendeleo yake. Ugunduzi wa gesi asilia na mafuta, madini pamoja na mbuga zake za wanyama ni rasilimali adimu na muhimu kulikwamua taifa kutoka katika wimbi la umasikini.
Kinachohitajika ni rasilimali watu; Kinachohitajika ni wataalamu wenye asili ya kitanzania waliopo ndani na nje ya nchi kushirikiana ili kuleta maendeleo ya haraka. Lazima watu wote wenye asili ya Kitanzania wapewe haki yao ya kikatiba pamoja na nafasi ya kushiriki kulijenga taifa, kijamii, kiuchumui na kisiasa
Kamwe Tanzania haiwezi na haitaweza kuendelea ikitegemea wageni. Watakaoleta maendeleo na mabadiliko makubwa ni watanzania wenyewe. Mipaka ya dunia imefunguka katika hii karne ya ishirni na moja. Badala ya kukumbatia misaada inayotudhalilisha na wageni wanaoiba rasilimali zetu, tutumie hazina kubwa tuliyonayo ya rasilimali watu, ili tuweze kujikwamua kutoka katika wimbi la umasikini.
Wataalamu wa kitanzania waliotapakaa duniani, wanastahili haki ya kurudi kwenye ardhi yao ya kuzaliwa bila vikwazo vya aina yoyote. Katika kuandaa katiba mpya ya Tanzania, tusifanye kosa la kuwafungia nje ndugu zetu walio ughaibuni kwa kuwa na vibali vya kuishi na kusafiri. Ikumbukwe kwamba, pamoja na kuwa na vibali hivyo, bado asili zao na mioyo yao itabaki Tanzania. Tusiruhusu historia ituhukumu hasa katika kipindi hiki ambapo ushindani wa maendeleo ya kiuchumi unazidi kuongezeka duniani
Mungu Ibariki Tanzania
John Mashaka
Mashaka.john@yahoo.com
No comments:
Post a Comment