Na Bryceson Mathias
VIWANGO vya Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Spika wa Bunge la Tisa, Mbunge wa Urambo Mashariki na Waziri wa Afrika Mashariki, Samweli John Sitta, vimeanza kudorola kama si kwisha kabisa, kutokana na kuonekana kushindwa kuliongoza Bunge hilo kwa madai anakumbatia Uchama na Udini.
Kutajwa kushuka na kudorola kwa viwango vya utendaji wa SItta kuliongoza Bunge hilo kumesikika zaidi wakati wa uchaguzi wa Wenyeviti wa Kamati za Bunge hilo, ambapo isivyo kawaida yake, Sitta alionekana kukipendelea Chama chake cha Mapinduzi (CCM) na kuwatosa wapinzani hadharani, bila uoga.
Kutokana na tabia hiyo kumvaa Sitta bila kujitambua, wananchi walio wengi kwa nyakati tofauti, wameanza kujiuliza, Sitta amelogwa na nini kiasi cha kutaka kuharibu utendaji wake wa Viwango, na Uadilifu uliovishwa Mavazi Mororo ya kupinga Ufisadi na Mafisadi?.
Mbali ya Umaarufu aliojipatia kwa kukemea Ufisadi wa EPA, Richmond, Dowans, Rada na mengine, kuna watu wanaanza kupata Shaka juu yake kwamba, Matarajio na mategemeo yao kuwa, Bunge hilo lingemsababishia kuandika Historia ya Utendaji wa kutukuka iwapo angeongoza Bunge hilo vizuri, sasa anajiharibia.
Wananchi wengine wanadai pengine Sitta amezidiwa na nguvu za Mafisadi ambao huenda wamefanya kila linalowezekana kuona kuwa wanamnyamazisha ili asiongeze Kiwango cha Umaarufu wake wa Bunge la Tisa, na pengine kuhakikisha Majigambo ya kuwa ni Kiongozi mwenye Viwango vya uchapa kazi vinafutika.
Wasomi na Wana zuoni wengi wanadai, kinachomharibia Sitta kwa sasa, ni kujisahau na kuvaa koti lenye matope la Uchama na bila kujua linaupigia chapuo Udini, wakati kwa viwango vyake vya uumini wa Mustakabali wa kulipenda Taifa na wananchi wake, asingestahili kuegemea huko.
Kiongozi mmoja Mkubwa wa Kanisa ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema, Maandiko ya Mungu yanasema, “Kilichotarajiwa kikikawiakuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima” Mithali 13:12.
Anachofanya sasa Sitta, ni yale ambayo vitabu vya dini vinasema, “Usije ukawapa wengine heshima yako, Na wakorofi miaka yako; Wageni wasije wakashiba nguvu zako; Kazi zako zikawa ndani ya nyumba ya mgeni. Mithali 5:9-10.
Wananchi na Viongozi wa Taasisis mbalimbali walikuwa na Matarajio makubwa na Sitta kuendesha Bunge la Katiba kwa umakini na viwango vya hali ya juu zaidi ya Bunge la Tisa, lakini kinachotokea sasa na kufanywa na Sitta, hakikutarajiwa na kinawaumiza wananchi wote!
Kutokana na udhaifu ambao Sitta anauonesha kwenye Bunge Maalum la Katiba, tayari wananchi wameanza kusema, hali hiyo inawapa mwanya Mahasimu wake wa Kinyang’anyiro cha Makundi ya Urais – 2015 ambapo wamesema watatumia Turufu hii ya Udhaifu kushindana naye.
Pamoja na kwamba Karata ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba ilikuwa inawapa nafasi kubwa sana Sitta na kundi lake lake la Mbio za Urais 2015, sasa imeonekana nafasi hiyo inachafuliwa kama Kitumbua kuingia Mchanga, ambapo Mahasimu wataoneka kufaulu kuibomoa Ngome ya akina Sitta.
Hata hivyo baadhi ya viongozi wa CCM waliohojiwa huku wakikataa kutaja majina yao kutokana na kuwa waumini wa Serikali Tatu, wamesema walikuwa kwenye kundi la Mbio za Urais 2015 upande wa Sitta, lakini kwa jinsi Dalili zinavyokwenda watalazimika kuachana njia panda, na Serikali Mbili ndizo zitakazowatengeanisha.
No comments:
Post a Comment