Gharama za ziada zinaweza
kuepukwa mathalan kwa kuiondosha Ofisi ya Makamu wa Rais na kuivunjilia mbali
ofisi ya Waziri Mkuu butu asiye na meno hata kucha
Kinachoelekea
kuuteka mjadala wa katiba mpya hivi sasa ni pendekezo la serikali tatu. Naunga
mkono serikali tatu kwa kuwa kiuhalisia imethibitika kuwa vigumu kuwa na
serikali moja kwa kisingizio cha kumezana. Na hizi mbili zimechusha kero zake
na viraka vimekuwa vingi mno kiasi kwamba nguo yetu hii Muungano itatatuka
pasipo kujitafakari upya.
Sababu kubwa
inayoonekana kuwa nzito ni kuhusu gharama. Ninachangia hili la gharama kwenye
makala hii fupi. Serikali
tatu zinaweza kuokoa sana gharama ikiwa tutaacha hofu ya kisichojulikana na
kujikita katika kufikiri kwa kutumia mbongo na sio visigino nk kama
walivyofanya kina Nyerere na Karume walivyofikiri kwa mbongo zao na nia na
dhati ya mioyo kabisa. Nasi sasa tunao wajibu; Tukiutimiza wajibu
huu tutatuzwa na tukiutelekeza tutatwezwa maana ilishanenwa Likulli
ajalin kitab', yaani kila zama ina kitabu
chake,”
Gharama za
ziada zinaweza kuepukwa mathalan kwa kuiondosha Ofisi ya Makamu wa Rais na
kuivunjilia mbali ofisi ya Waziri Mkuu butu asiye na meno hata kucha (ofisi
na sio mhe Pinda). Viongozi wakuu wa serikali hizi mbili yaani Tanzania
Barana Zanzibar ndiyo watakuwa wasaidizi wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mawaziri wachache wa kisekta
watakuwa wasaidizi wa karibu wa viongozi wakuu wa serikali hizi mbili za
Tanzania bara na Zanzibar .
Bajeti
inayotumika sasa kuendesha ofisi ya Rais itatumika kuendesha ofisi ya Rais wa
Muungano sambamba na kusimamia masuala ya Muungano. Gharama za uendeshaji wa
ofisi ya Waziri Mkuu na sehemu ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais sasa
zitatumika kuendesha Ofisi ya Kiongozi wa Serikali ya Tanzania Bara (bila
kujali cheo cha kiongozi huyo ataitwaje). Bajeti za wizara ambazo si za
muungano (hizo zipo hata sasa) hata hivyo zinaweza kupunguzwa.
Gharama za
uendeshaji wa serikali ya Zanzibar wala haina haja hata kuhofia maana hizo zipo
hata sasa.
Ni gharama
zipi tunazozihofia kuongezeka katika kuendesha serikali tatu?
Kwa upande
wa Bunge
Bunge la
Muungano halitakuwa na haja ya kukaa muda mrefu kama ilivyo sasa kwani masuala
ya muungano si mengi kiasi hicho. Gharama za muda utakaookolewa zitatumika
kuendesha bunge la Bara. Hali kadhalika Bunge la Tanzania Bara litapungua
ukubwa wake na hivyo kupunguza gharama tofauti na hivi sasa ambapo wakati wa
kujadili masuala ya bara yasiyo ya muungano wabunge kutoka zanzibar huwa
hawatoki wanakuwepo na posho wanalamba kama kawaida ilhali mijadala
inayoendelea inahusu mambo ‘yasiyowahusu’.
Gharama gani tunazihofia? Mambo yasiyo ya Muungano
kwa upande wa Visiwani yanajadiliwa na baraza la wawakili hata sasa. Serikali
tatu zinaweza kupunguza gharama hata zile za vikao vya mapatano na kutanzua
kero za muungano wa serikali mbili za sasa ambazo hazitanzukiki.
Adam/Upole Blog
No comments:
Post a Comment