HOTUBA ya Rais Jakaya Kikwete juzi bungeni imeleta mpasuko
mkubwa miongoni mwa Watanzania, na sasa wengine wanamtuhumu kwa kusaliti Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, wananchi na taifa. Wapo wanaokwenda mbali na kusema rais amevunja Muungano,
kwani ameshindwa kukemea Zanzibar iliyovunja Katiba ya Muungano na kujitangaza
kuwa ni nchi ndani ya nchi, kwa kuandika katiba inayopingana na Katiba ya
Jamhuri ya Muungano. Wanasema Katiba ilivunjwa mbele yake, akakaa kimya; na
kwamba hata alipojaribu kutetea msimamo wa chama chake kuhusu serikali mbili,
huku akibeza pendekezo la serikali tatu, Rais Kikwete alishindwa kuwaamuru
Wazanzibari waondoe vifungu kwenye katiba yao vinavyokinzana na, au vinavyovunja
Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Miongoni mwa wadau wa Muungano waliozungumza na Tanzania
Daima Jumapili kuhusu hotuba ya Rais Kikwete ni viongozi wa vyama vya siasa,
wasomi na wananchi wa kawaida. Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Dk. Willibrod Slaa, ambaye aligombea urais mwaka 2010 na kutoa upinzani wa
kutosha dhidi ya Kikwete, anasema kwa hotuba ile rais hakuwa anazindua Bunge
Maalumu la Katiba bali alikuwa anatoa semina elekezi iliyosheheni msimamo wa
chama chake, CCM. Anasema kitendo cha rais kujiingiza kwenye malumbano
yanayoligawa taifa ni sawa na kupasua nchi. Vile vile, anasema kitendo cha rais kujibizana na
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba, ambaye wiki tatu
zilizopita alikuwa amewasilisha rasimu ya pili ya Katiba mpya bungeni na kusoma
uchambuzi wa hoja za tume, ni sawa na kuisaliti tume aliyoiunda mwenyewe.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, Rais Kikwete aliacha urais wake
Ikulu Dar es Salaam, akabeba uenyekiti wa CCM hadi bungeni, jambo ambalo ni
sawa na kuisaliti taasisi ya urais, hivyo kusaliti wananchi. Dk. Slaa anasema dakika 240 alizotumia Rais Kikwete
kuhutubia Bunge, zilitumika vibaya kwani wajumbe waliokuwamo mle ni wawakilishi
wa makundi mengi yenye mwelekeo tofauti katika masuala nyeti ya kitaifa. Hivyo, haikuwa sahihi kuzindua Bunge kwa msimamo wa chama
kimoja cha siasa na kuzusha malumbano badala ya hoja za kuunganisha Watanzania. Na kwa kuwa rais alikuwa ameshaamua kujadili masuala haya,
na kwa kuwa alisisitiza kuwa asingependa kuona serikali ya Tanganyika
inaanzishwa akiwa madarakani, Dk. Slaa anasema lingekuwa jambo jema kama Rais
Kikwete angewaeleza Watanzania kwanini ameacha Muungano ukawa na nchi mbili
badala ya moja, tena kinyume cha Katiba, katika kipindi cha utawala wake.
Anasema serikali tatu hazipingiki, na kwamba wanaozipinga
watakuja kuhojiwa na vizazi vijavyo. Anasisitiza kuwa kama Rais Kikwete na CCM wanaona msimamo
wao ndio msimamo rasmi, ni vema rais avunje Bunge, ili kuokoa fedha za umma, au
kukusanya upya maoni ya wananchi, kama anadhani tume haikufanya kazi yake
vizuri. Kwa mujibu wa mhadhiri huyo, maoni ya Rais Kikwete na CCM
yalipaswa yapelekwe kwenye tume, si kwenye uzinduzi wa Bunge. “Hata sifahamu aliyemshauri rais kuzungumza vile katika
hotuba yake ya uzinduzi. Alipaswa kutoa maoni yale katika rasimu ya kwanza ili
iboreshwe kwa kuondoa utata wa masuala mbalimbali ambayo angeona yanaweza
kuleta mtafaruku, na si wakati huu katika rasimu ya pili ambayo imefikia hatua
nzuri,” anasisitiza.
Kwa mujibu wa Dk. Bana, jambo ambalo Rais Kikwete alipaswa
kufanya juzi ni kukazia hoja zilizo kwenye rasimu ya pili na kuwasihi wajumbe
kuwa makini ili wawaletee Watanzania vitu makini. Badala yake, anasema, rais
alitoa semina elekezi ya ‘kufundisha’ masuala fulani anayotaka. Dk. Bana anasema ingawa rais aliwataka wajumbe kutumia
mamlaka yao kukataa au kukubali yaliyomo katika rasimu ya pili, hotuba yake
imeonyesha sura nyingine ya kuwafundisha kazi. Kutokana na hilo, amewataka wajumbe wote wasiokubaliana na
rais waachane naye, wahakikishe wanajadili hoja moja baada ya nyingine kwa kuwa
sheria na kanuni walizojiwekea zinawaruhusu. “Nitumie fursa hii kumtaka (Freeman Mbowe) na wenzake kina
(James) Mbatia, Profesa (Ibrahim) Lipumba na wafuasi wao wakiwamo wajumbe ambao
hawakubaliani na maoni ya Rais Kikwete, wahakikishe wanasimamia rasimu ya pili
ili iweze kuleta mrejesho mzuri,” anasema Dk. Bana.
Dodoma
Mjini Dodoma, jana wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba
kupitia Umoja wao wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), walifanya kikako na kuweka
mikakati ya kuidhibiti CCM isichakachue maoni ya wananchi. Baada ya kikao, viongozi wa UKAWA, Prof. Ibrahim Lipumba,
James Mbatia, Freeman Mbowe na Tundu Lissu walizungumza na waandishi wa habari
na kuweka wazi msimamo wao. Walisema Kikwete alivunja kanuni za Bunge kwa kuchambua
rasimu wakati si mjumbe. Kwa mujibu wa Prof. Lipumba, Rais Kikwete amejidhalilisha
kwa kuchukua takwimu za mitaani na kuzitumia akidai ndizo zilitolewa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba. “Ameidhalilisha na kuidharau Tume ya Warioba ambayo
aliiunda mwenyewe na alikuwa akikutana nayo mara kwa mara. Alipaswa kueleza
mawazo hayo huko alikokuwa akijadiliana nao. Pamoja na maudhi, uchakachuaji na
usanii wake, maana rais wetu kila mtu anamjua ni msanii, lakini nawashukuru
wajumbe kuvumilia bila kutoka nje ya Bunge,” alisema.
Aliongeza kuwa kitendo cha rais kumdhalilisha Warioba ni
kudharau na kupuuza wananchi waliotoa maoni yao. “Rais bila aibu anatisha wananchi kuwa tukiingia serikali
tatu jeshi litapindua nchi, Wapemba wa wanaolima vitunguu huku Kibakwe na Tanga
watanyang’anywa ardhi. Huko ni kugawa Watanzania, na huo ni uchochezi,”
alisema. Alifafanua kuwa hatua ya rais ya kuidharau tume ya Jaji
Warioba na kuleta mawazo ya CCM, hawawezi kuivumilia kwa sababu hawako tayari
kuona maoni ya wananchi yakichakachuliwa. Prof. Lipumba alisema kuwa msimamo wao ni kuingia bungeni
na kwenye kamati, kujenga hoja kwa rasimu ya pili kwa kuzingatia matakwa ya
wananchi. “Rais ametuangusha kwa kukubali kwake kuzidiwa nguvu na
chama chake kisha kugeuza Bunge Maalumu la Katiba kuwa mkutano mkuu wa
CCM. Wakwere ni watani zangu lakini katika hili Kikwete amezidisha
utani. Yaani ni sawa na mtu unakaribishwa chakula, wewe unakwenda kucheza
ngoma,” alisema. Alisisitiza kuwa hoja zote za kitoto alizozitoa Kikwete
zimejibiwa vizuri na tume ya Warioba.
Naye Mbatia alisema kuwa licha ya Tanzania kuwa kimbilio
la mataifa mengine yenye machafuko kwa muda mrefu, bado CCM iko radhi machafuko
yatokee ili ibaki madarakani. Alisema inasikitisha kuona wale walioapa kulinda katiba
ndio wanakuwa wa kwanza kuivunja. “Kikwete hajamdhalilisha Warioba bali aliwatukana wananchi
waliotoa maoni yao. Anatukana wale wazee wa tume waliomzidi umri kwa kusikiliza
umbea wa mitaani na kuacha takwimu halali za tume,” alisema. Mbatia alisisitiza kuwa mabadiliko ya kumi ya Katiba ya
Zanzibar yamevunja Katiba ya Jamhuri na hivyo kuleta mgogoro wa kikatiba.
Alisema kuwa ahadi za Rais Kikwete kuwa watawapa
Wazanzibari mamlaka ya kujiunga na jumuiya za kimataifa ni rushwa ya kutaka
waunge mkono serikali mbili. “Tabia kuu nne za dola ni watu, ardhi, mamlaka na uhusiano
wa kimataifa, na vitu hivi vimo kwenye Katiba ya Zanzibar, hivyo kusema atawapa
Zanzibar uhuru wa kufanya hayo tayari amevunja muungano,” alisema. Mbowe naye alisema Kikwete ameweka msingi mbaya wa kubeza
maoni ya wananchi, jambo ambalo Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Kenya, Amos Wako,
alishawapa angalizo. “Seneta Wako alitueleza hapa kwenye semina juzi kwamba
Serikali ya Kenya iliteka nyara maoni ya wananchi na hatimaye katiba
iliyopendekezwa ikakataliwa kwenye kura ya maoni,” alisema. Mbowe alisema kuwa Kikwete si mjumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba, kwa hiyo hotuba yake na wingi wa wajumbe wa chama chake bungeni si
ushahidi kwamba watateka maoni ya wananchi.
Lissu alitoa ufafanuzi kwamba kanuni ya Bunge Maalumu
inayozuia jina la rais lisidhihakiwe ilivunjwa na Kikwete mwenyewe kwa
kufanya dhihaka za chama chake. “Kwa hiyo kanuni hiyo sasa haitatumika, nasi tutajibu
hotuba ya Kikwete hoja kwa hoja ndani na nje ya Bunge. “Wasije kutwambia tunamdhihaki Rais, isipokuwa ameanza
yeye na sisi tunamalizia. Na kuanzia sasa hatutashiriki majadiliano
yanayotokana na uvunjifu wa kanuni,” alisema. Lissu alifafanua kuwa muungano huo umebakia matambala
matupu kwa kuwa kauli ya Kikwete sasa inakiri kwamba ziko nchi mbili na amiri
jeshi wakuu wawili. “Sasa kama amesema watawapa Zanzibar mamlaka wanayotaka,
basi hizo ni serikali tatu,” alisema. Alisisitiza kuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta
alikiuka kanuni kwa kumruhusu Kikwete kuanzisha mjadala wa rasimu ndani ya
Bunge.
Akizindua Bunge hilo juzi, Rais Kikwete alisema serikali
tatu hazitakuwepo kutokana na serikali ya shirikisho inayopendekezwa kutokuwa
na rasimali na uwezo wa kukopa. Kikwete alitumia muda mwingi kupigia debe muundo wa
serikali mbili unaoungwa mkono na chama chake cha CCM akisema kuwa kero
zilizopo zinaweza kumalizwa kwa Zanzibar kupewa mamlaka kadhaa. Hotuba hiyo ilionekana kuwagawa hata wanachama wa CCM
wakidai Rais Kikwete alifanya makosa makubwa kuingiza masuala ya kisiasa kwenye
hoja ya kitaifa.
Dar (Anderw Chale)
Mkurugenzi wa Kampuni ya Hali Halisi Pulishers, Said
Kubenea, ambaye pia ni mchambuzi wa siasa, alimtaka Kikwete kufuta kauli yake
hiyo kwa kuwaomba radhi Watanzania kwani amewakosea kwa kupinga maoni yao
waliyoyatoa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kubenea alisema hayo kupitia kipindi cha moja kwa moja cha
Tuongee asubuhi kinachorushwa na Televisheni ya Star TV, ambapo alisema kama
Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba haikuwa sahihi,
ilikuwaje rais azikubali hatua zote na hakusema chochote zaidi ya kuwaamuru waendelee,
iweje leo awakane hadharani? “Kama ofisi ya waziri mkuu iliyo chini yake ilitoa maoni
yanayofanana na yaliyomo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba ‘ yaani serikali
3’, unawezaje kuyakataa kiasi hicho? Au unataka kutuambia kuwa taasisi za
serikali pia zilikusaliti? Ama hazijui chochote kuhusu changamoto za muungano?”
alihoji Kubenea.
Kubenea alisema, rais alionyesha hofu kuwa
inawezekana kwa muundo wa serikali tatu wanajeshi na polisi kuasi, labda kwa
sababu wanadai mishahara yao au posho zao. “Ukiwa umesahau kuwa Jeshi la Polisi lina madai makubwa
kuliko walimu kwenye muungano huu wa serikali mbili, lakini hawajapindua nchi,
iweje waje kupindua kwenye serikali tatu?” alihoji. Mhariri wa Gazeti la Jamhuri, Deodatus Balile, kupitia
kipindi hicho cha ‘Tuongee Asubuhi’, alimtaka rais kulivunja Bunge hilo kwani
wanamaliza mabilioni ya Watanzania yanayopotea kila siku. “Mimi namshahuri rais avunje bunge na katiba hiyo
itengenezwe na wabunge wachache katika bunge la kawaida hapo baadaye, ila si
hili ambalo yeye mwenyewe rais anaitambua katiba hii,” alisema Balile. Balile alikili kuwa rais ameshindwa kuwapa kile
walichokuwa wakikitegemea na zaidi hotuba yake ilijikita katika kumpinga Jaji
Warioba, hivyo wanaamini kuwa kuipata katiba ya Watanzania kwa sasa itakuwa
ndoto kama tayari rais ana mawazo yake kichwani juu ya katiba hiyo.
Dodoma (Sitta Tumma)
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Mkoa wa
Dodoma, Ramadhani Mwendwa, aliyasema hayo jana wakati alipotoa maoni yake kwa
mwandishi wa habari hizi mjini hapa, kuhusuiana na hotuba ya ufunguzi wa Bunge
hilo Maalumu la Katiba. Katika maoni yake, Mwendwa ambaye pia ni Katibu wa Chama
cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Juu, Habari na Utafiti (RAAWU), Kanda ya Kati,
alisema kwamba kitendo cha Rais Kikwete kupuuza na kudharau maoni ya Watanzania
wengi wanaotaka serikali tatu, kinakinzana na dhamira halisi ya taifa kupata
Katiba inayotokana na matakwa ya wananchi. Katibu huyo wa TUCTA Mkoa wa Dodoma, Mwendwa, alieleza
kwamba, kwa vile Serikali na CCM wanataka muundo wa serikali mbili kinyume na
matakwa ya wananchi wanaowaongoza, ni wazi kwamba hata vitatumika vitisho kwa
wananchi wakati wa kuipigia kura rasimu hiyo baada ya kupitishwa bungeni.
“Msimamo wa serikali mbili kwa wananchi ni wa kulazimishwa
na dola. Hii inatokana na kwamba dola haitambui raia wake kwamba wana haki ya
kusikilizwa na kutimiziwa matakwa yao….na inawezekana kabisa Rais Kikwete
anaamini alichaguliwa kwa bahati mbaya. Bila hivyo asingepuuza na kudharau
maoni ya wananchi kwamba wanataka nini katika nchi yao.
Mbeya
Akizungumza kwa jazba mkazi mmoja wa jijini humo aliyejitambulisha kwa jina moja la Lusimbi, alisema kuwa haoni sababu zozote za
serikali ya Kikwete kukubali uwepo wa mchakato wa katiba mpya huku akijua wazi
moyoni mwake amesheheni uamuzi mwepesi wa chama chake. “Hii ni tabia ya kinyonga, hivi unawezaje kumsikiliza
kiongozi wa nchi aliyeamua mwenyewe kuyageuza mawazo ya wananchi, kuwapandia
hisia zake binafsi, kuwa jaji na hakimu anayeamua mwenyewe anaitaka Tanzania ya
aina gani,” alisema Lusimbi. Alisema kuwa msimamo ulioonyeshwa na Rais Kikwete kwenye
hotuba yake umeingilia kabisa mchakato mzima wa uundwaji wa katiba mpya kwa
kuwa kwa hiari yake na bila kutumwa ameamua kuwatolea maoni wananchi huku
akijua wazi kuwa wananchi ndio wa mwisho kutoa uamuzi kuwa wanataka nini.
Mwananchi mwingine naye aliyejitambulisha kwa jina moja la
Mwakyusa, alisema kuwa hotuba ya rais itachangia kwa kiasi kikubwa kuwapotosha
wananchi, ilhali akijua wazi kuwa Zanzibar ni nchi na kwamba kwa upande wa pili
Tanzania Bara si nchi, kwa kuwa nayo inaendeshwa chini ya mwamvuli wa muungano. Mwakyusa alisema kuwa walitegemea kusikia hotuba
iliyotolewa mjini Dodoma na kiongozi wa nchi kwa weledi mkubwa ikilenga
kuwaonyesha nia na dhamira ya serikali kuchukua uamuzi huo na si kuweka wazi
hisia zake ambazo ni chanzo cha mpasuko ndani ya bunge hilo. “Kwa mara ya kwanza hotuba hiyo imenikera sana,
sikutegemea kusikia hotuba ya ajabu kiasi kile, kama rais alikuwa analo jibu la
aina ya muundo wa serikali katika katiba hakupaswa kuruhusu mabilioni ya fedha
za Watanzania zipotee kwa ajili ya kurudia makosa yale yale ndani ya miaka 50
ya muungano,” alisema Mwakyusa.
Mkazi wa jijini humo pia, Enock Mwaifunga, alisema
serikali imekurupuka kuchukua uamuzi ambao inaonekana dhahiri kuwa haikujiandaa
kwa katiba mpya ndiyo maana hata suala la kutokuwepo kwa kanuni za kuendesha
bunge maalumu la katiba kulitaka kuwagombanisha wajumbe ambao bila staha na
nidhamu walimshushia heshima Mwenyekiti wa muda Pandu Ameir Kificho.
Morogoro (Joseph Malembeka)
Baadhi ya wanachi mkoani Morogoro wakisema hotuba hiyo
imemdhalilisha Jaji Joseph Warioba na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa
ikikusanya maoni ya katiba. Elias Mwalusako, alisema, Rais Kikwete hakutakiwa
kuwasilisha maoni ya msimamo wake na chama chake bungeni humo juu ya rasimu
iliyoandaliwa na tume yake na kuwasilishwa bungeni humo Machi 18 na Jaji
Warioba. “Kama alijua kuwa yeye na chama chake wana msimamo wa
serikali mbili kwanini alitumia mabilioni ya fedha za wanachi kuandaa tume na
kuighamia kuzunguka nchi nzima kukusanya maoni ambayo yeye hayataki…kifupi
avunje bunge hilo arudi Ikulu kusubiri astahafu salama, rais ajae ataaanzisha
mchakato,” alisema Elias Mwalusako.
Mwalusako alisema ndiyo maana hata Jaji Warioba na
Rais Mstaafu Benjamin Mkapa hawakutaka kuonekana katika hotuba hiyo baada ya
kubaini kuwa kitakachokwenda kusemwa na Rais Kikwete kingekuwa cha kukinzana na
matokeo ya tume yake. Lazaro, mkazi wa Bondwa, alisema ingawa Rais Kikwete
alijitahidi kuonyesha changamoto zilizopo kwenye katiba hiyo kwa kupitia
kipengele kimoja baada ya kingine, bado hakuwatendea haki Watanzania alipoamua
kuonyesha msimamo wake mbele ya umma.
Kigoma
Mwalimu Kaijage, amesema amewasikiliza watu wanaomsifia
Rais Kikwete, lakini anamini kuwa Rais Kikwete ndiye chanzo cha tatizo kwa hoja
zifuatazo:
. Rais alikuwa wapi kuwaambia Zanzibar kuwa wamevunja katiba
kwa mabadiliko yao ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010, kusema mtu kutoka
Tanzania Bara hana haki ya kupiga kura Zanzibar mpaka akae miaka 15 ndipo
atakuwa na sifa kama Wazanzibari wengine?
. Mbona Mzanzibari akienda Kigoma au popote Tanzania Bara
anapiga kura bila masharti?
. Rais anasemaje juu ya sheria ya ardhi kule Zanzibar kuzuia
mtu yeyote kutoka Tanzania Bara kupata hata ardhi ya kujenga ilhali sisi huku
Bara hatuna sheria kama hiyo kwa Wazanzibari?
. Wapo wanaosema ardhi ya Zanzibar ni ndogo, kama ndivyo
itamkwe kwenye Katiba ya Muungano kuwa watu kutoka Bara hawaruhusiwi kujenga na
kupiga kura mpaka watimize miaka 15 ya kukaa Zanzibar na si kufanya mambo chini
chini halafu baadaye yanaleta shida.
Rais anasema tume ya Warioba imetoa
taarifa zisizo sahihi, je, ni uongo kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais haikupendekeza
muungano wa serikali tatu? Baraza la ofisi ya waziri mkuu halikupendekeza mfumo
wa serikali tatu na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar linaposema kuwe na
Zanzibar huru, Tanganyika huru na serikali ya Muungano ishughulikie mambo
machache ya muungano maana yake nini?
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment