Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Friday, February 7, 2014

Warioba awashukia wana-CCM wanaobeza Tume ya Katiba


Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba, amewaonya baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waache kubabaika, baada ya tume yake kutoa rasimu ya pili inayopendekeza kuwepo kwa Muungano wa serikali tatu. 
Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili jijini Dar es Salaam, alisema anasikitishwa na tabia ya baadhi ya watu kushutumu rasimu hiyo bila kutoa hoja na badala yake kuegemea kwenye hisia za kujadili watu. Moja ya hatua alizoziita kubabaika na kuweweseka, ni shutuma alizorushiwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Musoma mkoani Mara, Jacob Nkomola, aliyemtaka Warioba aiombe radhi familia ya Marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa kile alichokiita kumsaliti kwa kutoa mapendekezo ya serikali tatu.

      Warioba alisema kimsingi, hawafungi watu midomo wasitumie haki yao kujadili rasimu hiyo, lakini kinachomsikitisha ni baadhi ya watu kutoa maoni bila kujenga hoja, badala yake wanalazimisha na kutoa visingizio ambavyo havina mashiko. Alisema moja ya visingizio hivyo visivyo na chembe ya mantiki ni kama alichokisema Nkomola, cha kuihusisha familia ya Mwalimu na rasimu ya katiba. “Huku ni kuweweseka na kuwaletea bughudha Watanzania, ukiona mtu anajadili watu badala ya kutoa hoja amefilisika, tena inashangaza sana hapa familia ya mwalimu  inaingiaje?”alihoji na kuongeza “Tangu mwanzoni kabisa nilishatoa tahadhari kwamba Mwalimu hakuwa na akili mgando, alikuwa anaamini jambo na kulisimamia, lakini jambo hilo likihitaji mabadiliko alikuwa hasiti kufanya hivyo kutokana na wakati,”

      Kwa mara nyingine alitolea mfano jinsi Mwalimu alivyokuwa muumini wa serikali ya Chama kimoja, lakini wakati ulipofika ni yeye alikuwa wa kwanza kusisitiza kwamba muda wa Tanzania kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi umewadia mwaka 1992. Hata hivyo, alisema anashangazwa na hatua ya baadhi ya makada wa CCM kumshutumu, utadhani rasimu hiyo imetokana na kikundi kisicho rasmi. “Ieleweke kwamba ile ilikuwa ni Tume halali haikuwa kikundi Fulani cha watu. Tulikusanya maoni ya Watanzania, wapo waliotaka serikali moja, wengine mbili na wengine tatu. Tulipoyachambua tukabaini kuwa Watanzania wanahitaji serikali tatu na wala sio mbili,”alisema na kuongeza, tuliona matatizo (kero) yaliyopo kwenye serikali mbili hayawezi kutatuliwa ama kupatiwa ufumbuzi,”. Warioba aliwataka wana-CCM wanaong’ang’ana na hoja ya serikali mbili watoe hoja kwamba ni vipi wataondoa matatizo yaliyopo katika mfumo huo, badala ya kumshutumu yeye binafsi.

     Aidha, alisema anasikitishwa na kauli zinazotolewa, ambazo nyingi kati ya hizo zina maudhui ya kuwadharau wajumbe wa Tume yake na kuonyesha kana kwamba hakuna kazi ya maana waliyoifanya. Alisema wengi wanaotumia jina la mwalimu wamefilisika kimawazo na wala hawaamini kile alichokuwa anaamini muasisi huyo wa taifa. “Mathalani Mwalimu aliamini katika Azimia la Arusha na akasisitiza kwamba kitabu chake alikuwa akisafiri nacho sawa na msahafu, alisema wazi kwamba haoni kitu chenye kasoro ndani ya azimio hilo. Sasa kwanini wanaolikiuka hawaitwi wasaliti wa Mwalimu? Pia Mwalimu wakati Fulani alikubaliana na suala la mgombea binafsi lakini wengine  hawakukubaliana naye, mbona hao nao hawaitwi wasaliti wa Mwalimu?” alihoji.


Simon Mhina/Nipashe

No comments: