MBUNGE wa Iringa
Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (48) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Iringa kwa tuhuma za kujeruhi katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata
ya Nduli. Mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Godfrey Isaya, Mwendesha
Mashtaka wa Polisi, Elizabeth Swai, alisema Mchungaji Msigwa alitenda kosa hilo
Februari 5, 2014 katika Kijiji cha Nduli, mjini Iringa. Katika kesi hiyo
namba 28 ya mwaka 2014 mbunge huyo anadaiwa kumjeruhi Salum Kahita kinyume cha
kifungu kidogo namba 225 cha sheria ya kanuni za adhabu. Msigwa
anayetetewa na Wakili Lwezaula Kaijage alikana kosa hilo na hakimu aliahirisha
kesi hadi Machi 10 itakapotajwa tena kwa kuwa upelelezi wake haujakamilika.
Pamoja na mbunge
huyo, Jeshi la Polisi limewapandisha kizimbani Meshack Chonanga (22) na Paulo
Mapunda wote wanakijiji cha Nduli mjini Iringa wakituhumiwa kumjeruhi Alex
Mpiluka wakati wa kampeni hizo. Hata hivyo watuhumiwa wote walipata
dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili walioweka
dhamana ya ahadi ya sh milioni mbili kila mmoja.
Wakati
huohuo, Mahakama ya Hakimu
Mkazi Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, imemwachia kwa dhamana Mbunge wa
Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbayi (CHADEMA). Dhamana ya mbunge huyo
ilishindikana juzi kutokana na zuio la hati ya kiapo kutoka kwa Mwendesha
Mashitaka wa Serikali, Shukrani Madulu. Kasulumbayi na
wenzake 12 akiwemo Diwani wa Buselesele, Christian Kagoma wanakabiliwa na
tuhuma za kuwacharanga mapanga wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye
kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wilayani Kahama.
Awali akisoma
uamuzi mdogo mahakamani hapo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya, Gadiel Mariki,
alitupilia mbali cheti cha kiapo kwa madai ya kuwa na upungufu wa kisheria,
hivyo kukosa uzito wa kuzuia dhamana kwa watuhumiwa hao. Hakimu Mariki
alisema cheti cha kiapo hakikuonyesha taarifa ya majeruhi watatu ambao hali zao
ni mbaya, kimetolewa na nani, pia nafasi ya mkurugenzi wa kiapo haikuwa na
sahihi wala kuonyesha kiapo cha dini gani.
Baada ya kutupa
kiapo hicho, alisema dhamana ipo wazi kwa watuhumiwa wote 13 na kwamba kila
mshitakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili huku mmoja akiwa na hati ya
vielelezo vya mali isiyohamishika yenye thamani isiyopungua sh milioni 10. Licha ya watuhumiwa
wote kupewa dhamana, ni mbunge huyo peke yake aliyeweza kutimiza masharti ya
dhamana huku watuhumiwa wenzake wakiendelea kusota rumande kwa kushindwa
kutimiza masharti hayo.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment