Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Monday, February 24, 2014

John Mnyika aiweka hadharani Rasimu ya Kanuni


Mbunge  wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, ameamua kuiweka hadharani Rasimu ya Kanuni zote 113 za Bunge Maalumu, ikiwa ni pamoja na kufanya mkutano kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), baada ya uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba kukataa kuwashirikisha wadau kuijadili.

Mnyika, ambaye ni Mjumbe wa Bunge hilo na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliliambia NIPASHE mjini hapa jana kuwa, alijaribu kuushauri uongozi wa Bunge kuwashirikisha wadau kuzijadili ‘kanuni’ hizo kabla ya kujadiliwa na wajumbe wa Bunge, lakini umekataa.  

Alisema hoja iliyotolewa na uongozi wa Bunge kukataa suala hilo, ni kwamba kanuni ni mali ya Bunge, ambalo ndilo lenye mamlaka ya kuzitunga, hivyo haiwezekani kuwashirikisha wasiokuwa wajumbe wa Bunge.

 Kutokana na hali hiyo, alisema alitarajia kuziweka ‘kanuni’ hizo hadharani pamoja na kufanya mkutano huo kupitia mitandao ya kijamii jana. 

Alisema ameamua kufanya hivyo, ili kuwapa fursa wadau wa katiba kuzielewa ‘kanuni’ hizo na kuzitolea maoni, kabla ya kuwasilishwa kwenye Bunge ili wajumbe wake wazijadili na kuamua ama kuzipitisha au la.



Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Thoma Kashililah, aliliambia NIPASHE jana kuwa rasimu ya kanuni hizo itaanza kujadiliwa na wajumbe wa Bunge hilo, bungeni leo. 

 Mnyika alisema mkutano huo wa mtandaoni atakuwa akiufanya kwa saa mbili kila siku usiku na mchana.

Alitaja anuani ya mtandao atakaotumia kuweka rasimu ya kanuni hizo na kufanya mkutano huo, kuwa ni http//  mnyika.blogspot.com.

 Alisema licha ya ‘kanuni’ hizo kuwa ni za ndani ya Bunge, ambalo ndilo lenye mamlaka ya kuzitunga, zinawahusu pia wasiokuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba. 

Mnyika alisema hilo linatokana na wasiokuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuwa na haki ya kujua hatima ya maoni waliyoyatoa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo yameingizwa kwenye Rasimu ya Katiba inayotarajiwa kujadiliwa na kupitishwa na Bunge hilo.

Alisema suala la kuwashirikisha wadau wa katiba wasiokuwa wajumbe wa Bunge katika kuzijadili ‘kanuni’ hizo, ni jambo muhimu na la lazima, kwa kuwa udhaifu mkubwa uliomo kwenye ‘kanuni’ zinazopendekezwa, kama wadau hawatashirikishwa kuzitolea maoni, zinaweza kuwaathiri.
 

Ippmedia/Nipashe

No comments: