Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa
Huduma za Nishati na Maji (EWURA), katika kikao chake cha tarehe 10 Desemba
2013 pamoja na mambo mengine, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme kwa
viwango mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja hatua ambayo itaongeza
mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi na itaathiri uchumi wa nchi.
Maamuzi hayo yamefikiwa kufuatia tarehe 11 Oktoba
2013, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwasilisha maombi ya kurekebisha bei
ya umeme kwa EWURA. TANESCO ilipendekeza kuongeza bei kwa asilimia 67.87
kuanzia tarehe 1 Oktoba 2013, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1 Januari 2014 na
asilimia 9.17 kuanzia tarehe 1 Januari 2015. Vilevile TANESCO waliomba
kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme kulingana na mabadiliko ya
bei za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko ya thamani ya shilingi ya
kitanzania.
Maamuzi hayo ya Bodi ya EWURA ambacho ni chombo cha
Serikali yamethibitisha kwamba Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter
Muhongo alisema uongo kwa nyakati mbalimbali mwaka 2012 na 2013
alipowahakikishia wananchi kwamba bei ya umeme haitapanda hata baada ya
TANESCO kuwasilisha mapendekezo ya kupandisha bei ya umeme.
Aidha, kwa kuwa leo tarehe 9 Januari 2014 Waziri Muhongo
amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kwamba sekta ya nishati sio
porojo; natoa mwito kwake kuanza kwanza kujirekebisha yeye mwenyewe kwa kuacha
porojo na uongo na kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuzuia utekelezaji wa maamuzi
ya kupandisha bei ya umeme ambayo yataongeza ugumu wa maisha kwa wananchi
kinyume na ahadi ya maisha bora kwa kila mtanzania iliyotolewa na CCM.
Pia, kwa nafasi ya Waziri Kivuli wa Nishati na
Madini natoa mwito kwa wote wenye kuathirika na maamuzi hayo ndani ya wiki moja
kuanzia sasa watume maoni na mapendekezo yao kwa barua pepe kupitia anuani
mbungeubungo@gmail.com. Maoni na mapendekezo hayo yanaweza pia kutumwa
kwa njia nyingine za kuwasiliana na Ofisi ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inayoongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Maoni na
mapendekezo hayo yahusu athari ambazo wamezipata na/au wanatarajia kuzipata
kutokana na maamuzi hayo na mapendekezo ya hatua ambazo wanataka zichukuliwe.
Narajia kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa
wananchi mbalimbali hususan kutoka pia kwa wateja wa TANESCO ambao
wamepandishiwa bei katika makundi yafuatayo:
Kundi D1: Hili ni kundi la wateja wadogo wa
majumbani, hasa vijijini, ambao hutumia wastani usiozidi wa Uniti 75 kwa mwezi. EWURA imeongeza wigo wa mahitaji ya umeme na kufikia uniti 75 kwa mwezi, kwa
kile kilichoelezwa kuwa lengo likiwa ni kuongeza idadi ya wateja wa TANESCO
wanaoweza kulipa kidogo kwa matumizi ya umeme kwa kiwango hicho, na pia
kuwahamasisha kutumia zaidi umeme. Awali kundi hili lilikuwa linatunia wastani
wa matumizi ya uniti 50 kwa mwezi. Bei mpya ni shilingi 100 kwa uniti moja,
kutoka shilingi 60 za sasa, sawa na ongezeko la shilingi 40.
Kundi T1: Hili ni kundi la watumiaji wakubwa wa
umeme majumbani, biashara ndogondogo, mashine za kukoboa na kusaga nafaka, taa
za barabarani, mabango n.k. Bei iliyoidhinishwa ni shilingi 306 kwa uniti moja,
ikiwa ni ongezeko la Shilingi 85 ya bei ya sasa. TANESCO ilipendekeza ongezeko
la shilingi 131.
Kundi T2: Hili ni kundi la watumiaji umeme wa
kawaida ambao hupimwa katika msongo wa volti 400, na ambao matumizi yao ya
wastani kwa mwezi ni zaidi ya uniti 7,500 wateja wafanyabiashara kubwa, viwanda
vya kati. Bei ya nishati iliyoridhiwa ni shilingi 205 kwa uniti moja, sawa na
ongezeko la shilingi 73 ya bei ya sasa. TANESCO walipendekeza ongezeko la
shilingi 145 ya bei ya sasa.
Kundi T3-MV: Hili ni kundi la wateja wakubwa kama
viwanda vikubwa waliounganishwa katika msongo wa kati (Medium Voltage). EWURA
imeidhinisha bei ya nishati kwa kiwango cha shilingi 166 kwa uniti moja, sawa
na ongezeko la shilingi 45 ya bei ya sasa. TANESCO walipendekeza ongezeko la
shilingi 148 kwa uniti moja.
Kundi T3-HV: Hili ni kundi la wateja wakubwa
waliounganishwa katika msongo wa juu (High Voltage – Voti 66,000 na zaidi)
ikiwa ni pamoja na ZECO, Bulyanhulu, na Twiga Cement. Bei iliyoidhinishwa ni
shilingi 159 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la shilingi 53 la bei ya sasa. TANESCO
waliomba ongezeko la shilingi 80 kwa uniti moja.
Mara baada ya kupokea maoni na mapendekezo hayo,
pamoja na hatua ambazo nitachukua kupitia nafasi ya Waziri Kivuli wa
Nishati na Madini nitawasilisha pia mapendekezo kwa Kambi Rasmi ya Upinzani
kuchukua hatua za kibunge na CHADEMA kuchukua hatua za nje ya Bunge ili
kunusuru uchumi wa nchi na kutetea maslahi ya wananchi.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
09/01/2014
No comments:
Post a Comment