Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Sunday, September 29, 2013

UVCCM watibuana tena Arusha



    UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani hapa, umetibuka tena baada ya Katibu wa Tawi la Moivo wilayani Arumeru, Ally Shaaban Ally, maarufu kama Majeshi, kudai kuwa alikamatwa na polisi akihusishwa na mauaji ya bilionea Erasto Msuya kutokana na shinikizo la kisiasa. Alidai kuwa kukamatwa kwake kulitokana na vita ya makundi inayoendelea ndani ya chama hicho. Yeye alikuwa akipingana na msimamo wa baadhi ya vigogo kuhusiana na uchaguzi wa mwenyekiti wa chipukizi mkoani hapa uliofanyika Septemba 21, mwaka huu. Alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, na kumtuhumu kigogo mmoja wa UVCCM mkoa (jina tunalihifadhi) kuhusika na mchezo huo mchafu kwa madai kuwa kabla ya kukamatwa na kushikiliwa kwa siku moja kwenye Kituo cha Kati cha Polisi alimwambia kuwa angemfunga. Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Duwan Nyanda ambaye pia ni Ofisa Upelelezi wa Mkoa (RCO), alikanusha Ally kukamatwa na jeshi hilo huku akiwataka waandishi kuwasiliana na kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro mahali kesi hiyo ilikofunguliwa.




       Alisema kutokana na taratibu za kipolisi haiwezekani mtuhumiwa kukamatwa Arusha bila ya yeye kuwa na taarifa, hivyo akasisitiza kuwa hakuna tukio kama hilo, huku akiwataka waandishi kama hawajaridhika wawasiliane na viongozi wa CCM ili kupata ukweli. Majeshi alisema kuwa alikamatwa kimkakati siku ya Ijumaa saa 11:30 jioni akiwa maeneo ya soko la Kilombero na kuhusishwa na kesi hiyo ili kumfanya asishiriki kwenye uchaguzi wa chipukizi wa mkoa ambapo kuna kigogo alikuwa anataka mtoto toka Wilaya ya Monduli ashinde jambo ambalo alikuwa akilipinga. Alisema kuwa polisi watatu, wawili wakiwa wamevaa kiraia na mmoja akiwa na sare za jeshi hilo pamoja na bunduki, walimkamata wakimwambia yeye ni jambazi sugu aliyekuwa anatafutwa kutokana na mauaji ya mtu ambaye hawakumtaja jina, hivyo wakamnyang’anya simu na kuchukua vitu alivyokuwa navyo mfukoni.


          “Walinichukua mpaka Kituo cha Kati cha Polisi, sasa tukiwa pale nikawasikia wanaulizana ‘tumfungulie kesi gani’. Kauli hii kwa kweli ilinitisha na ndiyo inayozidi kuniogopesha kwani inaonyesha kuwa kukamatwa kwangu kuna hila ndani yake, walijadiliana kwa muda, wakakubaliana wanihusishe na kesi ya mauji ya Msuya,” alidai. Alisema kuwa alikaa kituoni hapo hadi siku inayofuata. Hakuandika maelezo yoyote zaidi ya kuandika jina, umri kabila na dini yake. Aliachiwa baada ya kudhaminiwa na Katibu Mwenezi wa CCM Arusha mjini, Gasper Kishumbue. Kada huyo alifafanua kuwa kwa sasa anaishi kwa hofu, kwani ndugu, jamaa na marafiki wa Msuya wanaweza kupata taarifa hizo zisizo sahihi kuwa yeye alishiriki mauaji ya mpendwa wao halafu hajachukuliwa sheria, na hivyo wakamdhuru.

        Katibu wa UVCCM mkoa, Salum Kidima alipoulizwa madai ya yeye kuhusika na sakata hilo, alikanusha huku akisema kuwa hana uwezo wa kulituma jeshi hilo, na kwamba taarifa alizonazo ni kuwa Majeshi alikamatwa baada ya kufananishwa na mtuhumiwa Ally Majeshi anayeishi Simanjiro mkoani Manyara. Msuya aliyekuwa mfanyabiashara wa madini aina ya tanzanite aliuawa na watu wasiojulikana kwa kupigwa risasi zaidi ya 20, Agosti 7, mwaka huu, majira ya mchana eneo la Mjohoroni kando ya barabara kuu ya Moshi – Arusha, ambapo kesi yake inaendelea.

Source: Macha G. ( Sept. 2013). UVCCM watibuana tena Arusha. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: