Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Friday, September 6, 2013

Tunahitaji maono gani kujua Ndugai hafai?


                                                   Edson Kamukara 

   NAIBU Spika wa Bunge, Job Ndugai, amepoteza hadhi, heshima na sifa za kuliongoza Bunge. Hana busara wala hekima na hatendi haki, amejaa ubabaishaji, ushabiki, upendeleo na ukereketwa kwa Chama chake cha Mapinduzi. Lakini zaidi hapaswi kupewa hadhi ya kukalia kiti alichopewa ambacho kinaheshimiwa sana na Watanzania. Huyu si muwakilishi sahihi wa Watanzania. Hii si mara yangu ya kwanza kulisema hili bali nimelirudia kama msisitizo kutokana na matukio ya aibu yaliyotokea bungeni chini ya uongozi wa kibabe wa Ndugai.

    Ndugai na viongozi wenzake wa upande wa serikali kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, wanadhani kuisadia serikali na CCM bungeni ni kuwadhalilisha wapinzani. Wote tumeona kilichotokea juzi, wapinzani wana hoja lakini serikali na CCM inategemea mabavu ya kupindisha sheria na kanuni na kutumia vyombo vya dola kulazimisha mambo yake yapitishwe.

      CCM inakufa na miongoni mwa wanaochangia kifo hicho cha mende ni Ndugai; sasa sijui tunataka maoni gani zaidi kutambua kuwa huyu jamaa hatufai kuliongoza Bunge letu? Spika wa Bunge, Anna Makinda, na wasaidizi wake wote akiwemo Ndugai kila mara wamekuwa wakituhubiria kuwa kiongozi wa upinzani bungeni anaposimama lazima apewe nafasi lakini juzi Ndugai akajikana mwenyewe. Kwa mujibu wa Ndugai, kiongozi wa upinzani anapewa nafasi ya kusema wakati wowote wakati wa maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu. Huyu ni ndumila kuwili kama si mbabaishaji.


       Potelea mbali hata kama anapingana na mkuu wake, lakini alishindwa nini kutumia busara kumpa nafasi Freeman Mbowe atoe hoja yake kama alivyokuwa ameomba kistaarabu? Ndugai anadhani mamlaka yake yatadumu milele hivyo amelewa ubabe wa kiti akiwaburuza askari wa Bunge wawatoe nje wapinzani wanaotaka kuleta hoja asizozitaka yeye na wana CCM wenzake?

      Vyovyote iwavyo iwe kumbeza au kumpuuza Ndugai lakini lazima tubaki na taswira ya Bunge letu kwamba kumbe wabunge wa CCM hakuna kitu. Hawana uwezo wa kujadili hoja wakiwa wenyewe. Wao wanajua kupongeza serikali, kiti cha Spika na kutetea mambo ya ajabu wakidhani chama chao kitatawala milele kumbe wamejipalia makaa kwa wananchi. Mathalani juzi jioni baada ya vurugu za asubuhi, wabunge wote 12 wa CCM waliopata nafasi ya kuchangia walijielekeza kwenye matusi, kejeli na kuzulia wenzao uongo huku wakiacha kabisa kujadili hoja iliyokuwa mezani.

     Hata Ndugai aliyewachefua wapinzani ili wawapishe wapitishe mambo yao kiholela kama walivyozoea, bado alishindwa kuwasaidia wenzake waliokuwa wakipiga porojo bungeni ili warejee kwenye hoja badala yake naye akawa anachomekea maneno ya kuwatia hamasa. Baadhi ya wabunge hao waliamua wenyewe kujidhalilisha kwa wapiga kura wao kwa kushindwa kujadili hoja na kujidai kuwakandia wenzao wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi waliotoka nje, wakisema wametia aibu.

      Wabunge hao na majimbo yao kwenye mabano ni Masauni Yusufu Masauni (Kikwajuni), Mary Mwanjelwa (Viti Maalum), Khamis Kigwangalah (Nzega), Paul Lwanji (Manyoni) na Kombo Khamis (Tumbe). Wengine ni Livingstone Lusinde (Mtera), John Komba (Mbinga Magharibi), Stella Manyanya (Viti Maalum), Richard Ndassa (Sumve), Saidi Nkumba (Sikonge), Adam Malima (Mkuranga) na Erasto Zambi (Mbozi Mashariki).

     Kilichoniduwaza ni kumwona hata Naibu Waziri wa Kilimo, Malima, naye akiwakejeli wapinzani kuwa wametia aibu huku akisahau kabisa aibu iliyompata mjini Morogoro hotelini alipokwapuliwa kila kitu na ‘kimada’ na kuachiwa silaha zake mbili bunduki na bastola. Hawa ndio aina ya viongozi wanaopewa nafasi na Ndugai kujadili mustakabali wa taifa? Ni jambo la kusikisha na kushangaza Tulimwona hata Dk. Kigwangalah alipoamua kumjadili mke wa Mbowe ambaye kimsingi na kikanuni anajua si mbunge anayeweza kujitetea bungeni lakini kiti kikanyamaza.

        Nauliza tena tukitaka kuona miujiza gani kujua Ndugai hafai kama wabunge aliowapa nafasi walishindwa kujadili hoja ya kibabe waliyokuwa nayo mezani? Mbunge kama Lusinde anaposimama na kusema kuwa wananchi wa Mtera kwao Katiba si kipaumbele bali wanataka maji, umeme na huduma za afya. Huyu kwake hajui kama hiyo ndiyo Katiba yenyewe. Hawa ndio wabunge wa CCM.

      Yako mengi ya kuandika kutokana na michango ya wabunge hao, wanaojidai kuwa serikali ya CCM inayo nia ya dhati kuleta Katiba mpya huku wakikiri kuwa agenda hiyo haikuwa ya chama chao bali ya wapinzani. Ni mtazamo wangu kuwa tuwaache CCM na serikali yao wajipake matope, wananchi wanaujua uwezo mdogo wa kiti cha Spika na hivyo hata wapinzani wachezewe rafu ya namna gani, aibu itabakia kwa wale wale watumia mabavu ya dola.

Tafakari!

No comments: