Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Saturday, September 7, 2013

CCM yafisidi Katiba Mpya

MBUNGE WAO AUNGA MKONO WAPINZANI, AMSHANGAA NDUGAI


         KUNA njama za kisirisiri za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhujumu mchakato wa Katiba Mpya kama njia ya kumkomoa Mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete, ambaye baadhi yao wanadai anawazunguka katika suala hilo, Tanzania Daima Jumapili limebaini. Miongoni mwa wanaopanga hujuma hizo ni wabunge na baadhi ya mawaziri waandamizi, ambao wanaona kuwa iwapo Katiba Mpya itapatikana kabla ya mwaka 2015, hawatakuwa na matumaini ya kurejea madarakani. Ingawa katika vikao na kauli rasmi CCM inaonekana inaunga mkono mchakato huu, mwenendo na kauli za baadhi ya mofisa wake waandamizi vinaonesha kuwa wana nia tofauti. Wanasema walishindwa kuzuia mchakato huu mapema kwa kuwa Rais Kikwete hakuwashirikisha, bali aliamua tu kuwakubalia wapinzani, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kabla ya vikao vya CCM kushirikishwa, na sasa wanasubiri kuzuia rasimu ya Katiba Mpya kwenye Bunge la Katiba lenye wajumbe wengi wa CCM.

         “Lengo letu hapa ni kumhujumu yeye na CHADEMA yake; maana inaonekana ameamua kuwabeba kwa kuwapa jambo ambalo halikuwa sehemu ya ilani ya uchaguzi ya CCM,” alisema mbunge mmoja wa CCM kwa sharti la kutotajwa jina. Duru za siasa nchini zinaeleza kuwa vurugu zilizotokea juzi bungeni na kusababisha kambi nzima ya upinzani kususia mjadala wa muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya Katiba ni sehemu ya mkakati wa CCM kwa kutumia kiti cha Spika wa Bunge, kuhakikisha Katiba Mpya ijayo, ama inachelewa au inabeba masilahi yao. Hii ni mara ya pili kwa wabunge wa CCM kuthubutu kumhujumu Rais Kikwete bungeni katika mchakato wa kuandaa Katiba Mpya. Novemba mwaka jana, wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, walitoka nje ya Ukumbi wa Bunge kwa madai ya kutoafikiana na baadhi ya vipengele vya Muswada wa sheria ya mabadiliko ya Katiba.

        Muswada huo ulipitishwa na wabunge wa CCM, lakini CHADEMA waligoma, na wakaenda kuonana na Rais Kikwete, ambaye alilazimika kukieleza chama chake juu ya umuhimu wa hoja za CHADEMA, wakarejesha muswada bungeni kwa ajili ya marekebisho. Hata hivyo ulipitishwa tena kwa wingi wa wabunge wa CCM na kuviacha vipengele vingi ambavyo Rais Kikwete alikuwa amekubaliana na CHADEMA. Baadhi ya Wana CCM wamediriki hata kuhoji kwanini Rais Kikwete alikubaliana na mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu muundo wa serikali tatu katika Muungano, jambo ambalo wanasema rais na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, walikula njama dhidi ya chama chao. Katika vurugu za juzi ambazo ni mwendelezo wa hujuma za CCM dhidi ya Kikwete, Naibu Spika na wabunge wa CCM walikataa kusikiliza hoja ya upinzani kuwa muswada huo umewabagua Wazanzibari, kwani Kamati ya Bunge haikuwasikiliza, na badala yake iliwasikiliza vigogo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wakati suala linalojadiliwa ni la Muungano, linalopaswa kujadiliwa na wananchi, si viongozi pekee.

          Zogo hilo lilizuka baada ya Mbunge wa Mkoani, Ali Khamis Seif, kuomba mwongozo wa Spika, akitaka hoja ya muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya Katiba iahirishwe hadi hapo Wazanzibari watakaposhirikishwa kama wenzao wa Tanzania Bara. Naibu Spika Job Ndugai aligoma kuwasikiliza. Hata aliposimama Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kutoa hoja, Ndugai alikataa kumpa fursa ya kuzungumza. Alimwamuru akae chini; na baada ya kuona Mbowe amekataa kukaa chini, aliamuru askari wa Bunge wamwondoe. Amri hiyo ya Ndugai ilizua tafrani baada ya wabunge wa CHADEMA kumzunguka Mbowe wakizuia askari hao kumwondoa. Katika tafrani hiyo, askari walimbeba mzobe mzobe Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, na kumtoa nje, huku askari mmojawao akidaiwa kumpiga ngumi.

        Hatimaye wabunge wote wa upinzani walitoka bungeni na kuwaacha CCM peke yao, ambao hata hivyo, hawakujadili muswada, bali kila aliyepata nafasi ya kuchangia muswada alitumia dakika zote 10 kutukana wapinzani. Juzi wabunge hao walipitisha muswada huo bila kuujadili, na bila kuzingatia hoja ya ushirikishwaji wa Wazanzibari. Hatima ya muswada huo iko mikononi mwa Kikwete ambaye anakabiliwa na wakati mgumu kama ataamua kuusaini au kulitaka Bunge litimize kwanza hitaji hilo lililoleta sokomoko inayoweza kudhuru mchakato mzima huko mbeleni. Kama Rais Kikwete atatumie busara kama za awali, upo uwezekano mkubwa muswada huo ukarejeshwa bungeni ili ujadiliwe baada ya kutimiza vigezo. Akizungumzia hali hii, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema msimamo wa CCM uko wazi, na kwamba hayo yanayojadiliwa pembeni si ya chama.

       Nape alisema CCM haiwezi kuruhusu wabunge au wanachama wake wamhujumu rais wala Warioba. Alisisitiza kwamba chama chake kinaunga mkono kazi ya Tume ya Marekebisho ya Katiba, ingawa kina msimamo katika maeneo kadhaa unaokinzana na rasimu iliyotolewa na tume hiyo. Alisema hata hivyo, msimamo wa chama unabaki kuwa wa chama, na kwamba wananchi watakapoamua aina ya Katiba wanayotaka ndio msimamo utakaokuwa wa mwisho. Alipuuza kauli za wanaosema kuwa Katiba Mpya haikuwa sehemu ya ilani ya uchaguzi ya CCM, akisema kuwa alichofanya Rais Kikwete ni kutazama hali halisi na matakwa ya wakati. Kwa sababu hiyo, alisema hata katika suala la Katiba Mpya, kitakachoamua hatima na aina ya Katiba Mpya ni mahitaji ya wakati, si ilani ya CCM au chama chochote.

Kauli ya Dk. Slaa

         Naye Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema walichofanya wabunge wa CCM kupitisha muswada huo juzi ni kielelezo kuwa Katiba inayoandaliwa ni mali ya CCM, kwani inatengenezwa kwa maoni ya CCM. Akizungumza na gazeti hili jana, Dk. Slaa alisema kuna upotoshaji unaofanywa na viongozi wa Bunge kwa kushirikiana na serikali katika hoja ya ushiriki wa Wazanzibari. Dk. Slaa aliwashangaa wabunge wa CCM kwa kushindwa kujadili jambo zito lililokuwa mbele yao na badala yake wakaishia kuwashambulia wabunge wa CHADEMA na CUF. Alisema anaamini kuwa hali hiyo ina msukumo kutoka nje ya Bunge, na akatahadharisha juu ya mhimili mmoja kuingilia uamuzi wa muhimili mwingine. Alisema hali hii itawafanya Watanzania wasipate Katiba waliyoitarajia.

      Alisema madhara ya hali hiyo yamejionesha katika sura mbili kwa wabunge kuonesha ushabiki wa kichama zaidi badala ya kupigania masilahi ya taifa. “Lissu alisema Wazanzibari hawajashirikishwa, sasa hawa wanakuja na barua ya serikali. Tunafahamu walipata maoni ya baadhi ya viongozi wa serikali wanaotokana na CCM lakini hawajawafikia Wazanzibari wengi wa kawaida,” alisema Dk. Slaa. Kutokana na hali hiyo, alisema wananchi wameshaanza kuchanganyikiwa juu ya dhamira ya serikali katika kuheshimu maoni ya wananchi kupitia rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Jaji Joseph Warioba. Akizungumzia udhalilishaji aliofanyiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Dk. Slaa alisema Tanzania inafuata kanuni za mabunge ya Jumuiya ya Madola ambayo nafasi ya kiongozi wa upinzani bungeni ni sawa na waziri mkuu kwa upande wa serikali.

      “Kwa maana hiyo, anaposimama Kiongozi wa Upinzani bungeni au Waziri Mkuu lazima jicho la anayeongoza kiti cha Spika limtupie jicho kwa kuwa ni lazima atakuwa na hoja ya kusikilizwa. “Nilishasema katika hili Ndugai alikuwa hatumii akili yake alikuwa anaongozwa kutoka nje ya Bunge na hili Watanzania wanapaswa watambue mabavu yaliyotumika ni kielelezo cha wazi cha ukosefu wa demokrasia nchini,” alisema Dk. Slaa. Alisema waliopitisha rasimu hiyo wameua matumaini ya Watanzania na sasa ni jukumu la wananchi kuamua hatima ya nchi yao. Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Zanzibar Hamad Masoud, alisema hawana taarifa yoyote ya wananchi kushirikishwa katika muswada huo wa mabadiliko ya sheria ya Katiba. Alisema hali hiyo inadhihirisha nia mbaya ya serikali katika kutatua matatizo ya wananchi kupitia Katiba huku akilaumu uamuzi wa kamati kufanya mambo yake kwa siri.

Maige alishambulia Bunge

         Wakati wabunge wa CCM wakiwashambulia wenzao wa kambi rasmi ya upinzani waliosusia muswada huo, Mbunge wa Msalala, Ezekil Maige (CCM), amelishambulia Bunge, hususan kiti cha Spika kwa kushindwa kutumia busara kuepusha vurugu bungeni. Katika taarifa yake aliyoitoa kupitia mtandao wa Kijamii wa Wanabidii, Maige ambaye amepata kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema kuwa alitazama kwa mshangao na kutoamini kuhusu kilichojiri bungeni juzi. Alisema kwa bahati mbaya hakuwepo Dodoma siku hiyo kwani alikuwa mjini Arusha kikazi, lakini hakuona sababu kabisa ya kufikia hapo kwani hali hiyo ingeweza kuepushwa na kiti cha Spika. “Ingewezekana kabisa kuahirisha muswada na kutoa nafasi kwa Kamati ya Katiba na Sheria kwenda Zanzibar kupata maoni ya wenzetu wa huko.

        “Najua kuna maelezo mazuri ya kushirikishwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Lakini kikanuni, Baada ya Muswada kusomwa mara ya kwanza, unakuwa mikononi mwa Bunge na kamati ndiyo inayokusanya maoni si serikali,” alisema Maige. Maige ambaye anakuwa mbunge wa kwanza wa CCM kukosoa kiti cha Spika, alisema kwa kuwa hakuna ushahidi wa ‘public hearing’ kufanyika Zanzibar na kuwasikia Wazanzibari wa kawaida (nje ya serikali), basi kulikuwa na hoja kabisa ya kurekebisha kasoro hiyo kwa kutoa nafasi kwa kamati kwenda Zanzibar. “Suala la Katiba ni kubwa hivyo ni vema zikafanyika jitihada za kutosha kuhakikisha tunakwenda pamoja (na wenzetu hasa wenye mtazamo tofauti na sisi) badala ya kutumia wingi wetu kwani mwisho wa safari tukienda hivi wapo watakaodai Katiba Mpya si yao, hivyo kuikosesha ‘social legitimacy’,” alisema.

      Kwa mujibu wa Maige, hatua ya Ndugai kutomsikiliza Kiongozi Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, nako kulitibua mambo bila sababu. “Mbowe angepewa nafasi ya kusikilizwa, hata kama hoja yake isipokubaliwa ingekuwa nafuu sana na shari na aibu ya jana ingeepukika. “Tumesameheana, lakini tujifunze na tujitahidi sana kwenda kwa maelewano,” alisema Maige katika taarifa hiyo.

Source: Tanzania Daima ( Sept. 2013).CCM yafisidi Katiba Mpya. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: