Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, September 4, 2013

Madiwani CCM watishia kujiuzulu


      MADIWANI 14 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya wametishia kujivua nyadhifa zao kwa madai kuwa Serikali Kuu imekuwa ikiwafanyia vitendo vya ubabaishaji. Walitaja baadhi ya vitendo hivyo kuwa ni kuwaletea watumishi wasiokuwa na viwango katika halmashauri hiyo kinyume cha utaratibu. Madai hayo yalikuja baada ya kufanyika kikao cha baraza la madiwani jana kilichokuwa na ajenda moja ya kujadli hoja ya Mkaguzi wa Hesabu katika Halmashauri hiyo, ambapo Mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro. 

       Diwani wa Lwangwa, Robert Mwaibata, alidai Halmashauri ya Busokelo imetokana na Halmashauri ya Rungwe na baada ya kupewa hadhi ya kuwa halmashauri waligawana watumishi pamoja na magari, lakini anashangaa kuona baadhi ya watumishi wakirudishwa kufanya kazi tena katika Halmashauri ya Rungwe bila ya wao kujulishwa. Alisema watumishi watatu  kutoka Idara ya Elimu ya Msingi wamepelekwa kufanya kazi Rungwe pia baadhi ya watumishi wamenyang’anywa magari waliyokuwa wakiyatumia bila kujali changamoto walizonazo za upungufu wa watumishi na usafiri. Diwani wa Mpombo, Anyosisye Njobelo, alisema Halmashauri mpya ya Busokelo ina upungufu mkubwa wa watumishi, kwani katika idara nyingi zimekaimishwa na wao kama madiwani ambao ndio wenye halmashauri wanataka wapewe kibali ili wawathibitishe waliokaimu kuwa wakuu wa idara kamili na si kuletewa watumishi wengine kinyemela na kupewa ukuu wa idara.


      Naye Diwani wa Kandete, Salome Mwakalinga, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo alisema amekuwa akifuatwa na madiwani kwa nyakati tofauti wakitaka kuachia ngazi kutokana na ubabaishaji unaofanywa na serikali, ikiwa ni pamoja na kutoipa kipaumbele halmashauri hiyo. Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chrispin Meela, mbali na kukiri kuwapo na changamoto hizo, aliwataka madiwani hao kuwa wavumilivu kwani tayari amezungumza na katibu mkuu wa wizara husika kwa ajili ya kutoa kibali na kuwa ameahidiwa ndani ya siku saba atakuwa amepewa na ndipo atakapowakabidhi ili waanze mchakato wa kuajiri watumishi.


Source: Yassin I. (Sept. 2013). Madiwani CCM watishia kujiuzulu. Rungwe. Retrieved fromTanzania Daima

No comments: