WAKATI sakata la dawa
za kulevya likiwa limeichafua Tanzania katika uso wa kimataifa, orodha ya
majina ya wanaohusika na biashara hiyo ambayo Rais Jakaya Kikwete alidai kuwa
nayo, amesema amekwishaipeleka kwenye Mamlaka husika. Rais Kikwete mara kadhaa
amekuwa akisema kuwa anayo orodha ya watu wanaouza dawa za kulevya hapa nchini,
hivyo gazeti hili lilimtafuta kupitia kwa msemaji wake, kufahamu suala hilo
lilikofikia.
Akizungumza na gazeti hili
kupitia kwa Msemaji wake, Salvatory Rweyemamu, Rais Kikwete alisema orodha
ambayo alisema anayo alikwishaikabidhi kwa vyombo husika kwa ajili ya hatua
zaidi.
“Rais atembee nayo mfukoni ya nini?
Hata Nzowa katika taarifa yake alisema
alipatiwa… wamepewa vyombo husika, Serikali haiendeshwi kwa vyombo vya habari,
kuna vingi vinafanyika bila kutangazwa. Mtafute Nzowa atakwambia vyema,”
alisema Rweyemamu, wakati gazeti hili lilipotaka kufahamu juu ya orodha hiyo ya
Rais ilikofikia.
Orodha ambayo Rais Kikwete amekuwa akielezwa kuwa anayo,
inadaiwa kuwahusisha vigogo mbalimbali nchini, wakiwemo wabunge, mawaziri na
wafanyabiashara wakubwa ambao hata hivyo imebainika kuwako kwa ugumu wa
kuwachukulia hatua, kutokana na kutokuwa na ushahidi ili kuwabana wahusika.
Kutokana
na kauli hiyo ya Rais kupitia kwa msemaji wake, Gazeti hili liliamua kutafuta
moja ya mamlaka zinazohusika kupambana na dawa za kulevya ili kufahamu juu ya
orodha hiyo iliyokabidhiwa na Rais na hatua ambazo zimechukuliwa.
Mkuu wa
Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi
(ACP), Godfrey Nzowa, hakukiri wala kukana kupokea orodha hiyo kutoka Ikulu.
MTANZANIA
Jumapili: Kamanda sisi ni MTANZANIA Jumapili, tumepata taarifa kwamba Ikulu imekupatia
majina ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, vipi umefikia wapi katika
kuishughulikia?
NZOWA: “Kutoka wapi? Mimi napata kutoka sehemu mbalimbali,
tunakuwa na watu ambao tunakamata na tunawapekua, ikithibitika tunawapeleka
mahakamani
Na hivi karibuni nimepatiwa orodha ya watu 261 wanaodaiwa kufanya
biashara hiyo, lakini katika upekuzi wetu hatukukuta kitu.
MTANZANIA Jumapili:
Kwa hiyo hao mliowapekua ndiyo orodha mliyopatiwa kutoka Ikulu?
Nzowa: Siwezi
kutaja moja kwa moja kwa sababu ninapokea orodha kutoka sehemu mbalimbali, kwa
hiyo si salama kutaja jina la mtu.
Siwezi ku ‘mention’ kuwa ni Ikulu ama nani.
Ushahidi wa moja kwa moja haupo, lakini wa kimazingira upo, tulipeleka kiapo
ili washitakiwe Mahakamani. Kwa mujibu wa Nzowa, wengine zaidi ya 260
waliopatikana na ushahidi wamefunguliwa kesi katika mahakama za hapa nchini.mHivi
karibuni katika Bunge linaloendelea Dodoma, kuliibuka hoja ya kuitaka serikali
kutaja orodha ya wanaodaiwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya, ambapo Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi,
alishindwa kufanya hivyo.
Badala yake, Lukuvi alisema baadhi ya majina ya
wabunge yametajwa miongoni mwa watu wanaoshukiwa kujihusisha na biashara hiyo
na kwamba angetaja majina, Bunge lisingebaki salama.
Lukuvi alisisitiza kuwa
serikali haiwezi kuwataja hadharani kwa haraka, kwani inaogopa kukurupuka na
kushindwa mahakamani.
Hata hivyo, Lukuvi alisema ukubwa wa biashara hiyo hapa
nchini unadhihirishwa na idadi ya Watanzania 274 waliokamatwa kati ya mwaka
2008 hadi Julai, mwaka huu kwa kosa la kujihusisha na dawa za kulevya katika
nchi mbalimbali za nje.
Pamoja na kukamatwa kwa Watanzania hao nje ya nchi,
wageni 31 wanashikiliwa mahabusu katika Magereza ya Keko na Ukonga, Dar es Salaam,
ambao ni raia wa Iran, Pakistan, Senegal na Afrika Kusini.
Sakata la dawa za
kulevya nchini lilitikisa zaidi baada ya kukamatwa kwa wasichana wawili, Agness
Gerald (25) na Mellisa Edward (24) katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo,
Afrika Kusini, wakitokea Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, (JNIA) wakiwa na
dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine kilo 150, zenye thamani ya Sh.
bilioni 6.8 za Tanzania.
Hatua hiyo ilimlazimisha Waziri wa Uchukuzi, Dk.
Harrison Mwakyembe, kuwafukuza kazi wafanyakazi wa JNIA, wanaodaiwa kuhusika na
upitishwaji wa mzigo huo, huku baadhi ya watendaji wakihamishwa vituo vyao vya
kazi. Moto huo uliowashwa na Mwakyembe, ulikuja baada JNIA kutajwa kuwa moja
ya chochoro kubwa za kupitisha dawa hizo, hali ambayo pia imeshuhudia Jeshi la
Polisi kuwaondoa kwa kuwahamisha vituo vya kazi, Kamanda wa Polisi wa Viwanja
vya Ndege, Kamishna Msaidizi (ACP) Deusdedit Kato na Mkuu wa Upelelezi wa
Viwanja hivyo, David Mwafwimbo.
Source: Mtanzania (September 2013). JK: Nilikwishakabidhi orodha ya ‘wauza unga’. Retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment