Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Tuesday, August 20, 2013

Wananchi wamtimua mwenyekiti wa CCM


          MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Manyara na Diwani wa Kata ya Loiborsiret wilayani Simanjiro, Lucas ole Mukusi, juzi alikumbana na nguvu ya umma baada ya kufukuzwa kutoka kwenye mkutano wa wananchi wa Kijiji cha Kimotorok, wilayani Simanjiro waliofunga barabara kuu ya Babati-Kiteto kushinikiza mgogoro wa mpaka kati yao na Mkungunero Game Reserve utatuliwe. Kijiji cha Kimotorok kiko ndani ya Kata ya Loiborsiret ambayo Ole Mukusi ndiye diwani wake.

      Kigogo mwingine aliyekumbana na hasira za wananchi kwa kutimuliwa kwenye mkutano huo ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM taifa (NEC), Wilaya ya Kiteto, Emmanuel Papia, pamoja na mwenyekiti wa kijiji hicho, Daniel Melau. Wananchi walifikia uamuzi wa kufunga barabara hiyo kutwa nzima baada ya askari wa Mkungunero kuchoma nyumba ya mwenzao, Daudi Balarika, katika tukio lililotokea Agosti 12, mwaka huu. Wakizungumza kwa jazba mbele ya diwani wao kabla ya kumtimua, Michael Laizer na Napile Kinyaa walisema kiongozi huyo pamoja na wenzake wa Wilaya ya Simanjiro na Mkoa wa Manyara wamepuuza tatizo hilo lililodumu tangu mwaka 2004.

       “Tangu mgogoro huu ulipoanza zaidi ya nyumba 50 za wananchi zimechomwa moto bila serikali kuchukua hatua yoyote dhidi ya wahusika. Tumechoka kunyanyasika huku viongozi tuliowachagua wakitupuuza,” alisema Laizer. Kwa mujibu wa Laizer, wananchi wa Kimotorok tayari wamefikisha malalamiko yao ngazi mbalimbali ya serikali kuanzia wilaya, mkoa na taifa bila mafanikio. Baada ya kutimuliwa kikaoni, viongozi hao walitoa taarifa polisi ambao walifika eneo la tukio baada ya saa tano tangu barabara kufungwa na kufanya majadiliano na viongozi wa mila kuomba barabara ifunguliwe.

      Akizungumza na wananchi hao kuwasihi kufungua barabara, Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Manyara, Jerome Ngowi, aliahidi kufikisha malalamiko yao kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa ili alifikishe kwa Mkuu wa Mkoa, Elaston Mbwilo, kwa ufumbuzi. Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu madai ya wananchi, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Daniel Melau, alisema tangu mwaka 2004, yeye pamoja na viongozi wengine wa mila wa jamii ya Kimaasai (Laigwanan), wamejaribu kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo bila mafanikio.

Source: Tanzania Daima ( August 2013).Wananchi wamtimua mwenyekiti wa CCM. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: