MADIWANI wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) waliofukuzwa katika Manispaa ya Bukoba, wamesema wako tayari
kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kama chama chao
kitaendelea na msimamo wa kuwafukuza. Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya
simu, mmoja wa madiwani hao (jina na kata yake tumevihifadhi), alisema wako
tayari kuhamia Chadema muda wowote kama hawatarudishiwa uanachama wao.
Alisema,
madiwani wote waliofukuzwa wana msimamo mmoja, ambapo wanasubiri vikao vya
Kamati Kuu ya CC ili wajue hatima yao, lakini vikishindwa kuwarudisha kwenye
chama, watahamia Chadema ili kuendeleza harakati zao walizozianzisha.
Alisema,
wanachokifanya wao ni kutetea maslahi ya taifa na wananchi waliowapigia kura na
si kulinda biashara za watu binafsi, hata kama wanaungwa mkono na uongozi wa
juu wa CCM.
Msimamo huo wa madiwani umekuja siku mbili baada ya Mwenyekiti wa
Chadema Taifa, Freeman Mbowe, kuwakaribisha madiwani hao katika chama chake na
kusema wako tayari kuwafundisha siasa za mageuzi.
Mbowe aliyasema hayo katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Uhuru, mjini Bukoba, juzi,
katika mwendelezo wa mikutano ya mabaraza ya wazi ya chama hicho kujadili rasmu
ya Katiba mpya.
Mbowe alikwenda mbali zaidi akisema chama chake kiko tayari
kushirikiana na kiongozi wa CCM anayepinga ufisadi kama anavyofanya Mbunge wa
jimbo hilo, Balozi Khamis Kagasheki.
Alipoulizwa kama wamepata mawazo ya
kujiunga na Chadema, baada ya kauli ya Mbowe, diwani huyo alisema wao
walikwishakuwa na mawazo hayo, lakini kauli ya mwenyekiti huyo imewaweka huru
zaidi.
“Si kama tumeamua sasa, mawazo ya kuhamia Chadema tulikuwa nayo baada
ya uongozi wa mkoa kutangaza kutuvua uanachama, lakini kwa kauli ya Mbowe
kutukaribisha rasmi, kumetujengea ari mpya kwamba hatujapotea.
“Tatizo letu na
meya linafahamika kwamba ni ufisadi wake tulioulalamikia tangu mwaka jana,
kwenye vikao vya Baraza la Madiwani, hatukusikilizwa, badala yake tunaonekana
wasaliti wa chama.
“CCM wanapaswa kujua kwamba, hoja za wapinzani zikiwa
sahihi wananchi wanawaunga mkono, vivyo hivyo na sisi hatuwezi kubeza hoja zao
kwa sababu tu ni wapinzani, tutaonekana watu wa ajabu,” alisema diwani huyo.
“Tumefarijika
na kauli ya Mbowe, baadhi yetu tulikuwepo katika mkutano wake jana (juzi) pale
Uwanja wa Uhuru, ni suala la muda tu mtasikia Bukoba imezaliwa upya,” alisema.
Mbali
na hilo, mgogoro huo unaofukuta katika Halmashauri ya Bukoba unahusishwa na
sababu za kisiasa kati ya Kagasheki na Meya wa mji huo, Anatory Amani.
Balozi
Kagasheki, ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), anatajwa kuwa na uhasama
wa kisiasa na kada mwenzake, Amani, ambaye awali wawili hao walikuwa na
ushirika wa karibu.
Madiwani wanane waliofukuzwa wanatuhumiwa kushirikiana na
wenzao wa upinzani kusaini hati maalum na kuiwasilisha kwa Mkurugenzi wa
Manispaa, wakimtaka aitishe kikao ili wapige kura ya kumng’oa madarakani Meya
Amani mwishoni mwa mwaka.
Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa kilichokaa
Agosti 3, mwaka huu, kiliwafukuza uanachama na uongozi madiwani hao, akiwamo
Mwenyekiti wake wa Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza na Diwani wa Kata ya Kashai.
Wengine
waliofukuzwa mbali na mwenyekiti huyo, ni Diwani wa Kata ya Buhembe, Alexander
Ngalinda, ambaye pia ni Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.
Wengine
na kata zao kwenye mabano ni Meya wa zamani wa manispaa ya hiyo, Samwel
Ruhangisa (Kitendaguro), Dauda Kalumuna (Ijuganyondo) na Deus Mutakyahwa
(Nyanga).
Wengine ni Robert Katunzi (Hamugembe), Richard Gasper (Miembeni) na
Murungi Badru Kichwabuta, Diwani wa Viti Maalumu.
Source: Peter A. (CHADEMA). Madiwani Bukoba: Tuko tayari kwenda Chadema. retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment