BAADHI ya wabunge wamekosoa
mbio za Mwenge wa Uhuru, huku wengine wakitaka ufutwe kwa maelezo kuwa hauna
tija kwa sasa. Wabunge hao wakiwamo wa upinzani na CCM, walisema Mwenge umekuwa
kero na kwamba wakati mwingine ofisi za umma hufungwa kutokana na mbio zake na
hivyo kusababisha wananchi kukosa huduma.
Hata hivyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, (Utawala Bora), George Mkuchika, alizomewa na kurushiwa maneno ya kejeli
pale alipojaribu kujenga hoja ya kutetea mbio hizo za mwenge.
Sakata hilo
lilitokea jana bungeni, baada ya Mbunge wa Musoma Mjini Vicent Nyerere
(Chadema), ambaye alitaka kujua faida na hasara zilizopatikana tangu Mwenge wa
Uhuru ulipoanza kukimbizwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Nyerere alisema
wakati fulani viongozi wa Serikali walimtisha Naibu Meya wa Manispaa ya Musoma,
Nyamero Bwire, kutokana na hatua yake ya kuzuia gari la wagonjwa la hospitali
ya wilaya kutumika katika mbio hizo.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wabunge
walimzomea Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Mkuchika, baada ya
kuinuka na kutoa ufafanuzi wa swali hilo lililoulizwa na mbunge huyo.
Katika
swali lake la msingi, mbunge huyo alisema kuwa tangu mwenge ulipohamishiwa
katika mfumo wa Serikali, wananchi wamekuwa wakilazimishwa kuchangia fedha kwa
nguvu pamoja na matumizi yasiyokuwa sahihi ya magari ya Serikali.
“Serikali
haioni kwamba kuanzia sasa ianze kukimbiza mwenge katika maeneo yale tu ambayo
wananchi wake wapo tayari kuchangia michango ya mwenge?” Alihoji Nyerere.
Mbunge
huyo pia alitaka kujua kiasi cha bajeti ya mbio za mwenge kwa mwaka na iwapo
matumizi ya fedha hizo hufanyiwa ukaguzi.
Kwa upande wake Mbunge wa Nkasi
Kaskazini, Ally Kesy (CCM), alisema mbio za mwenge hazina faida kwa Watanzania
walio wengi kwani shughuli za kiuchumi zimekuwa zikiathiriwa. “Binafsi hiki kitu kinachoitwa mwenge
sikitaki kabisa, kwani ni wazi tangu maandalizi yake hadi kufika kwake kumekuwa
na mateso, kwani viongozi wanatakiwa kutoa huduma lakini wote huondoka ofisini. “Wanatumia siku tatu kwa ajili ya kukagua
miradi inayoitwa ya mwenge, huku wananchi wakisota kuwasubiri na hata baada ya
kufika na kukesha katika eneo husika. “Wakati mwingine hutumia siku mbili
kupumzika badala ya kuwahudumia wananchi kwa kisingizio cha mwenge. Sasa
tulipofika inatosha, ni vema mwenge usikimbizwe kwani umekuwa na matumizi
mabaya,” alisema Kesy.
Mkuchika azomewa
Katika majibu yake, Mkuchika alisema
kuanzishwa kwa mwenge huo ulikuwa na lengo la kukimbizwa Tanganyika na hata
kuwamulika maadui wa Tanzania. “Wale wanaodai kwamba mbio za mwenge
hazina umuhimu si kweli. Malengo yake yalikuwa ni kukimbizwa Tanganyika na
umekuwa ukitoa elimu kama vile elimu kuhusu dawa za kulevya, rushwa na kuzindua
miradi ya maendeleo,” alisema Mkuchika. Majibu hayo yalimfanya akumbane na zomea
zomea kutoka kwa wabunge wa kambi ya upinzani, huku zikisikika sauti za wabunge
wakisema; “Mwenge unaeneza Ukimwi”, “unaeneza ufisadi na hatuutaki tena”.
Baada ya jibu hilo baadhi ya wabunge
walisimama na kutaka kuomba mwongozo wa Spika, huku Mbunge wa Wawi Hamad Rashid
Mohamed (CUF), akitaka fedha za mwenge zikaguliwe. “Serikali huwa inatenga fedha kwa ajili
ya mbio za mwenge, pia wananchi huchangishwa fedha kwa ajili ya mwenge huo huo,
lakini fedha zake hazijulikani vizuri matumizi yake. “Tunataka CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali), afanye ukaguzi kwenye matumizi ya fedha za mwenge tangu
ulipoanza kukimbizwa hadi sasa,” alisema. Naye, Mbunge wa Kasulu Mjini Moses
Machali (NCCR-Mageuzi), alitaka Bunge liahirishwe ili kutoa fursa kwa wabunge
kujadili hoja ya mwenge, ambao alisema hauna faida zaidi ya kuwasumbua
wananchi.
Mbunge wa Chakechake, Mussa Haji Kombo
(CUF), aliomba mwongozo wa Spika akihoji kwanini mwenge unakimbizwa Zanzibar
wakati uliasisiwa Tanzania bara. “Mheshimiwa Naibu Spika ninachotaka
kusema hapa, Waziri Mkuchika alisema kuwa Mwenge ulianzishwa na ulikuwa
ukimbizwe Tanganyika, je imekuwaje ukimbizwe Zanzibar,” alihoji. Awali akijibu swali la msingi la Nyerere,
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala alisema
alisema mbio za Mwenge wa Uhuru zilianzishwa kwa falsafa ya kuhamasisha
ukombozi wa taifa na bara la Afrika, mwasisi wake akiwa ni Mwalimu Julius
Nyerere.
Alisema mwenge huo umeendelea kuwa tunu
ya taifa na chombo pekee cha uzalendo kinachohamasisha na kuhimiza mshikamano,
umoja wa kitaifa, uzalendo, uadilifu, kukuza moyo wa kujitolea na kuuenzi
uhuru. Alisema Mwenge wa Uhuru utaendelea
kukimbizwa na kwamba michango ya mbio hizo kwa wananchi ni ya hiari. Makala alisema ni kweli
shughuli za mwenge hubadilisha ratiba katika wilaya husika, lakini faida za
kukimbiza mwenge ni kubwa kuliko shughuli hizo, hivyo utaendelea kukimbizwa.
Source: Kimwanga B. (August 2013). Wabunge waupinga Mwenge. Dodoma. Retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment