Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, August 21, 2013

Vita CHADEMA, CCM, Warioba

HOJA YA SERIKALI TATU YAVURUGA



     MIKUTANO inayofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kote nchini kuhusiana na rasimu ya mabadiliko ya katiba, huku kikihimiza wananchi kuunga mkono pendekezo la kuwepo kwa serikali tatu, imezua na kuzidisha uhasama mkubwa kati yake na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Daima Jumatano limebaini. Habari za uhakika kutoka vyanzo vya kuaminika, zimebaini kuwa mwanzoni mwa wiki hii, kulifanyika jitihada kubwa za kujaribu kuzima mikutano hiyo kwa kutumia vyombo vya dola, lakini ikashindikana. Imedaiwa kuwa mmoja wa viongozi wa juu wa CCM alitaka mikutano hiyo izuiwe na Jeshi la Polisi kwa sababu zozote zile za kiusalama, lakini mpango huo ulikataliwa na baadhi ya viongozi wanaodaiwa kuchoshwa na siasa za kikandamizaji. Hatua hiyo inadaiwa kuchukuliwa baada ya CCM kugundua kuwa mpango wake wa kushinikiza wananchi kwa kutumia mabaraza ya katiba kuunga mkono suala la serikali mbili kuelekea kushindwa vibaya.

       Aidha, kuna madai kwamba kiongozi huyo alitaka CHADEMA isiruhusiwe kama itaendelea na mikutano yake, kuzungumzia suala la serikali tatu, kwa madai kwamba ni kwenda kinyume na sheria iliyokubaliwa ya mchakato wa maoni ya katiba mpya. Wakati CCM ikiwa imetoa msimamo wake na kuwaamuru viongozi wake wa ngazi zote kushikilia msimamo huo na kuusambaza kwa wanachama wake, uamuzi wa CHADEMA wa kuendesha mikutano ya hadhara na kuelezea msimamo wake wa serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba, umeathiri kwa kiwango kikubwa mpango mzima wa chama hicho tawala kutimiza lengo la kampeni yake. Aidha, baadhi ya viongozi wa CCM wanamtuhumu Jaji Warioba kwa kile walichokiita “kuwabeba” CHADEMA na kuchukua hoja yao ya kutaka muungano wa serikali tatu.

     Jana, Jaji Warioba aliyepata kuwa waziri mkuu wa Tanzania, alilazimika tena kutoa kauli akisema kuwa hayupo tayari kuwajibu wanasiasa wanaopinga muungano wa serikali tatu kwa madai kuwa tume imetimiza wajibu wake kwa kuhakikisha wanazingatia maoni ya wananchi wengi. Hata bila kutaja jina la chama, kauli hiyo imeilenga CCM ambayo kupitia kwa katibu wake wa Itikadi na Uenezi, ilisema wazee wanaoshabikia mfumo wa serikali tatu wanangoja kufa. Akizungumza na wajumbe wa Baraza la Habari (MCT), Warioba alisema: “Huu sio wakati wa malumbano bali lazima tukubaliane mambo kwa maslahi ya taifa, tujielekeze kupata katiba kwa ajili ya Watanzania wote, imguse kila mtu.

      “Tusipowasikiliza wananchi tutapata katiba ya makundi jambo ambalo si sawa, panueni mawazo yenu mjadili rasimu kwa msingi wa wananchi kwanza.” Aliwataka wanasiasa kuacha ubinafsi kwa kutaka kuweka mawazo yao kwenye katiba, huku akieleza kwamba tume yake haitapokea maoni ya wanasiasa wanaofanya mikutano ya hadhara. Kwa mujibu wa Jaji Warioba, tume yake haifanyi biashara ya malumbano badala yake anajikita kuhakikisha taifa linapata katiba bora huku akijisifu kwa kufanikiwa kuwa kimya licha ya tume yake kuzongwa na maneno ya wanasiasa na asasi za kiraia. Mwenyekiti huyo alisema tume yake ilipokea maoni mengi kutoka kwa wananchi, lakini waliamua kuchukua mambo ya msingi kwa maslahi ya taifa.

     “Hivi sasa tume ya katiba imetoa nafasi kwa mabaraza ya katiba yanayowakilisha makundi mbalimbali ya watu kujadili rasimu hiyo kwa kuzingatia mahitaji muhimu ya wananchi wote,” alisema. CHADEMA kwa upande wake, imeishambulia vikali CCM kwa madai ya kutojali maslahi ya Watanzania katika kupata katiba bora na yenye manufaa kwa taifa. Juzi, akizungumza mjini Dodoma, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa alisema CCM imeamua kuwa wapinzani wakubwa wa rasimu ya katiba mpya. Akihutubia mkutano wa hadhara mjini humo, Dk. Slaa alisema CCM wanapinga hoja nyingi ambazo zimependekezwa katika rasimu ya katiba mpya na kuwaona viongozi kama vile Jaji Joseph Warioba anayetokana na chama hicho tawala kama adui na msaliti.

     “CHADEMA tunasema iwapo rasimu ya katiba ikichakachuliwa katika Bunge la Katiba kwa kutumia wingi wa wanachama wa CCM, sisi CHADEMA tutatetea haki yetu kwa wananchi,” alisema. Alisema lazima CCM watambue kwamba amani ni tunda la haki na imeasisiwa na viongozi waliotutangulia, hivyo ni lazima wakawa makini kuendeleza amani hiyo iliyoachwa na viongozi waliotangulia kwa matendo na wala siyo kwa maneno. “Lazima haki ya kikatiba igawanywe vizuri bila ubaguzi, waondoe unyanyasaji, na ubaguzi, watende haki, wakifanya hivyo kutakuwa hakuna haja ya kuhubiri amani majukwaani,” alisema Dk. Slaa.

Source: Tanzania Daima (August 2013). Vita CHADEMA, CCM, Warioba, Retrieved from Tanzania Daima

No comments: