Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, August 21, 2013

Ofisi ya Rais yatumika kupora kiwanja


   OFISI ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetumiwa na maofisa wa Wizara ya Ardhi kutaka kuhalalisha jaribio lao la kupora kiwanja namba 170A cha Mwanaidi Alawi kilichopo Kipawa eneo la viwanda, jijini Dar es Salaam. Mwanaidi Alawi (86) ndiye mmiliki mrithi wa kiwanja hicho tangu mwaka 1991 na alipewa hati Na. 38101 na Wizara ya Ardhi. Hati hiyo inasomeka kwa majina ya mama mzazi wa Mwanaidi; Buna Binti Mussa na mama yake mdogo, Asha Mwinyi Kondo (wote marehemu), ambao walikuwa wamiliki wa eneo lote la kuanzia makao makuu ya Tazara hadi Kipawa, Dar es Salaam wakimiliki kwa hati ya serikali ya wakoloni wa Kijerumani (Free hold title) iliyotolewa kwao mwaka 1955, kabla Serikali ya Tanzania kupima eneo lao upya na kugawa kwa watu wengine na wao kuachiwa kiwanja kimoja Na. 170A.

     Lakini katika hali ya kushangaza, mwaka 2009 alijitokeza Mtanzania mwenye asili ya Kiasia, Abdul Khan, akidai ndiye amemilikishwa na wizara kiwanja hicho baada ya wizara kuona kikongwe huyo hawezi kukiendeleza. Hata hivyo, Mwanaidi alipoona kiwanja chake amepewa Muasia bila maelezo wala kulipwa fidia, mwaka 2010 alilalamika kupitia vyombo vya habari na wizara ilichunguza na kuona alikuwa na haki kisheria ya kuendelea kumiliki ardhi yake na wizara kumtaka Khan kutojihusisha na kiwanja cha bibi huyo. Mbali ya Khan kudai kupewa kiwanja cha bibi huyo pia iligundulika kuwa kimefutwa na aliyekuwa waziri wa Wizara ya Ardhi wakati huo, John Chiligati na kurejeshwa kwa rais. Hata hivyo wizara iliona maamuzi hayo yalifanyika kwa kumuonea Mwanaidi kwani hakuwa amepewa taarifa yoyote.

      Machi 25, 2011 msajili wa hati, Subira Sinda, alitangaza katika gazeti la serikali toleo namba 12 ukurasa wa 30 kuwa hati Na. 38101 imerejeshwa kwa Mwanaidi Alawi, ndipo Khan alipokimbilia mahakamani. Baada ya uamuzi huo, Julai 31, mwaka huu Mwanaidi alikwenda wizarani kutaka kulipia kiwanja hicho, ndipo akakuta taarifa inayodai kiwanja chake kimerejeshwa kwa rais tangu Novemba 20, 2011 kwa mara nyingine bila yeye kutaarifiwa. Hata hivyo, taarifa za uhakika kutoka Ofisi ya Rais zinasema Rais Kikwete hajawahi kusaini nyaraka za kufuta umiliki wa kiwanja hicho, na hivyo kuonekana kuwa kuna mchezo mchafu wa uporaji wa viwanja unaofanywa na maofisa wa Wizara ya Ardhi.

Source: Maziku G ( August 2013). Ofisi ya Rais yatumika kupora kiwanja. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: