MAKALA: KITILIA MKUMBO
MJADALA kuhusu
Rasimu ya Katiba Mpya umeanika sura halisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Kwamba
wamepinga mambo yote ya maana katika rasimu hiyo si jambo la ajabu na
inatukumbusha kwa mara nyingine kwamba chama hiki kitasimama kinyume na jambo
lolote linalotishia uhai wake madarakani, hata kama jambo hilo ni la manufaa
kiasi gani kwa nchi.
Ukiacha suala
la serikali tatu, katika rasimu inayoendelea kujadiliwa na mabaraza ya katiba,
CCM wamepinga pia uwepo wa haki za binadamu ndani ya Katiba na kuingizwa kwa
maadili katika Katiba mpya. Kupinga kuingizwa kwa haki za binadamu ndani ya
Katiba ni kiashiria muhimu kwamba Chama cha Mapinduzi na serikali yake ni
wavunjifu wa haki hizi na wana mpango wa kuendelea kuzivunja lakini sasa
wanaogopa zikiingia kwenye Katiba zitawatia kitanzini.
Kupinga kwao
kuingizwa kwa maadili ndani ya Katiba ni kiashiria kingine kwamba chama hiki na
serikali yake hawataki vitendo vya ufisadi vikome hapa nchini. Ikumbukwe kwamba
suala la maadili liliingizwa katika rasimu kutokana na wananchi wengi waliotoa
maoni kuhusu Katiba mpya kupigia kelele suala la ufisadi unaofanywa na
viongozi. Ni kwa sababu hii tume wakatafsiri kwa usahihi kabisa kwamba ni
muhimu maadili iwe sehemu ya Katiba ili vitendo vyovyote vya ufisadi
vitakavyofanywa na kiongozi ijulikane kwamba kiongozi huyo amevunja Katiba na
hivyo anastahili kupoteza madaraka yake wakati hatua za kisheria zikiendelea
kuchukuliwa dhidi yake. Upinzani wa CCM dhidi ya maadili haushangazi kwa sababu
wangeunga mkono vipi maadili iwe sehemu ya Katiba wakati uwepo wao madarakani
unatokana na kukiuka maadili?
Pamoja na
kupinga mambo mengine katika Katiba mpya, CCM wanapaza zaidi sauti zao katika
kupinga rasimu juu ya serikali tatu. Na katika kuimarisha upinzani wao dhidi ya
serikali tatu wanatumia zaidi hoja ya gharama. Kwamba kuendesha serikali tatu
ni gharama kubwa kuliko kuendesha serikali mbili na hivyo uwepo wa serikali
tatu ni kuibebesha nchi na walipa kodi gharama za ziada zisizo za msingi.
CCM wametumia
mwanya wa Watanzania wengi kutokuhoji mambo kuipenyeza hoja hii dhaifu kwa kasi
kubwa, na wananchi wanaelekea kukubaliana nao bila kuuliza maswali ya msingi.
Katika kujenga hoja yao pinzani dhidi ya serikali tatu CCM hawatuambii ni kiasi
gani cha gharama kinatumika sasa hivi katika kuendesha serikali mbili, na kiasi
gani kitatumika katika kuendesha serikali tatu ili tupime tofauti ya hizo
gaharama.
Hawakokotoi
hesabu hizi kwa sababu wanajua kwamba ukweli utajulikana na hoja yao itakosa
nguvu. Kwa hivyo, hakuna ushahidi wowote wa maana unaoonyesha kwamba gharama za
kuendesha serikali tatu itakuwa kubwa kuliko ile ya kuendesha serikali mbili.
Kama CCM wangekuwa na uchungu kweli juu ya gharama za kuendesha serikali tatu
wangepigania uwepo wa serikali moja ya Muungano ambayo kwa vyovyote gharama
zake zingekuwa ndogo zaidi kuliko kuendesha muundo wa serikali mbili au tatu.
Kwa hivyo, kama alivyopata kueleza mwanasiasa machachari na msomi wa sheria na
haki za binadamu Tundu Lissu, hoja ya gharama za kuendesha serikali ina lengo
la kuwatoa wananchi kwenye mjadala wa msingi juu ya umuhimu wa Katiba mpya na
matatizo ya muundo wa Muungano ulivyo sasa.
Ukweli ni
kwamba hata ukifanya hesabu za haraka haraka utakuta kwamba gharama za serikali
tatu zitakuwa ndogo zaidi kuliko serikali mbili. Nitatoa mfano katika eneo moja
la Bunge. Kwa mujibu wa Rasimu ya Katiba Mpya, kutakuwa na wabunge wa Muungano
75. Bunge la Zanzibar litakuwa na wabunge 50 watakaotokana na majimbo ya sasa,
na Bunge la Tanganyika litakuwa na wabunge 189 wa majimbo ya uchaguzi ya sasa.
Kwa hiyo ukijumlisha hapa utaona kwamba mabunge yote matatu ya Muungano,
Tanganyika na Zanzibar yatakuwa na idadi ya jumla ya wabunge 314.
Ukilinganisha
na Muungano uliopo sasa hivi ambapo tuna idadi ya wabunge 239 wa majimbo ya
Muungano, wabunge wa viti maalumu 102, wabunge 10 wa kuteuliwa na Rais, wabunge
watano wanaowakilisha Baraza la Wawakilishi, pamoja na Mwanasheria Mkuu
tunapata jumla ya wabunge 357 wa Bunge la Muungano pekee.
Tukijumlisha na
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wapatao 81 waliopo sasa hivi tunapata jumla ya
wabunge 438! Kwa hiyo utaona hapa kwamba gharama za kuendesha mabunge katika
muundo wa Muungano wa serikali tatu itakuwa ndogo kwa upungufu wa wabunge 124
ukilinganisha na mfumo wa sasa. Hali itakuwa ni hii hii tukifanya hesabu za
kuhudumia taasisi mbalimbali za serikali katika muundo wa serikali tatu dhidi
ya mbili.
Ndio maana
ninasema CCM wanazungumza juu juu na hawataki kwenda ndani kwa sababu wanajua
wataumbuka na hoja yao itakufa. Bahati mbaya makada wa CCM wamezoeshwa
kubebeshwa hoja kama kasuku na hawajafundishwa kutafakari. Wamejazana kwenye
mabaraza ya katiba na wanaimba kama kasuku kwamba muundo wa serikali tatu ni
gharama bila ushahidi wowote wa kimantiki na kihesabu.
Inabidi
tukumbushane vilevile kwamba hoja ya serikali tatu haijaanza leo na mara zote
imeibuliwa ndani ya CCM yenyewe. Hoja hii iliibuliwa rasmi mara ya kwanza
miaka ya 1990 wakati wa mjadala wa uwepo au kutokuwepo vyama vingi uliokuwa
ukiendeshwa na Tume ya Jaji Mkuu Marehemu Francis Nyalali. Jaji Kisanga naye
aliibua hoja hii mwaka 1998 wakati wa mjadala wa mabadiliko ya katiba. Majaji
hawa kama, ilivyo kwa Jaji Warioba, waliteuliwa na marais wa CCM na baadhi yao
kama Warioba wanajulikana kwa ukada wa CCM kuliko vijana wanaoibukia leo.
Kabla ya hapo
mwaka 1993 wabunge machachari 55 wa CCM walipeleka hoja bungeni ya kutaka
kuundwa kwa serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, na hoja ilikuwa ipite
kama Mwalimu Nyerere hakuingilia kati. Katika Gazeti la Uhuru la Jumatatu ya
Agosti 5, 2013 amekaririwa Nape akijinasibu kwamba wanaotaka serikali tatu
hawana akili timamu. Nami namuuliza Nape kati yake na hao majaji niliowataja
hapo juu ni nani asiye na akili timamu?
Kama
nilivyosema mwanzoni mwa makala hii, CCM hawana hulka ya kuunga mkono mambo
mema kwa nchi hii. Tukumbuke kwamba ni CCM hawa hawa waliopinga uwepo wa vyama
vingi. Wakawalisha maneno makada wao waliotapakaa nchi nzima wakatae mfumo wa
vyama vingi na ikawa hivyo. Hata hivyo, busara za kawaida za Mwalimu Nyerere
ziliokoa jahazi na tukaingia kwenye mfumo wa vyama vingi huku CCM wakiwa
hawajaridhia wala kuridhika.
Ndio maana hadi
leo CCM wanaamini kwamba wenyewe ndio chama pekee kinachostahili kuongoza nchi
na vingine vipo tu kwa ajili ya kuonyesha kwamba tupo katika mfumo wa vyama
vingi ili tupate misaada ya wazungu. CCM hawahawa pia walipinga kuwepo kwa
katiba mpya na wakaapa kwamba hili ni jambo lisilowezekana nchini Tanzania.
Wakamtumia mwanasheria mkuu na waziri wa sheria wa wakati huo kupiga kelele
barabarani wakijanadi waziwazi kwamba suala la katiba mpya tusahau na halipo.
Kilichookoa jahazi ni kujitoa ‘muhanga’ kwa Rais Kikwete ambaye aliamua binafsi
kwamba kuna haja ya mchakato wa Katiba mpya. Naamini hii ngwe iliyobaki, ambayo
ni ngumu zaidi, ni Rais Kikwete pekee atakayeokoa jahazi kwa kuwakemea makada
wenzake waweke mbele maslahi mapana ya nchi hii dhidi ya maslahi mafupi na
hafifu ya chama chao.
Bila Rais
Kikwete kujitoa ‘muhanga’ kama alivyofanya katika kuanzisha mchakato wa Katiba
mpya tutakwama na nchi itaingia katika mgogoro usio wa lazima wa kisiasa. Yote
hii ni kwa sababu makada wa CCM wametapakaa katika kila chombo kitakachoshughulikia
Katiba mpya, kuanzia kwenye mabaraza hadi kwenye Bunge la Katiba. Bahati
mbaya makada wengi wa CCM hawajitegemei kimawazo na wanasubiri kuelekezwa cha
kusema na chama chao na hapa ndipo umuhimu wa Rais Kikwete unapoingia. Hivyo,
tunamsihi Rais Kikwete asikubali CCM wamtibulie alama ya utawala wake ambayo ni
katiba mpya. Ni muhimu ahakikishe kwamba jahazi alilolianzisha linafika
mwisho salama na hii ndio itakuwa alama kubwa zaidi ya utawala wake.
No comments:
Post a Comment