Uamuzi wa Halmashauri ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera kuwavua uanachama madiwani tisa na baadaye chama hicho ngazi ya Taifa kubatilisha maamuzi hayo, umeibua mgawanyiko wa wazi, baada ya uongozi wa mkoa kusema maamuzi yake ni halali. Agosti 13, mwaka huu uongozi wa Mkoa wa Kagera ulitangaza kuwavua uanachama madiwani hao kwa maelezo kuwa wamekuwa wakifanya vitendo vya kukihujumu chama hicho na kwamba wameitwa mara kadhaa katika vikao, lakini wamekuwa wakikaidi. Waliofukuzwa kwa mujibu wa Katibu wa CCM mkoa wa Kagera, Eveline Mushi, ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kashai.
Wengine ni Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Alexander Ngalinda, ambaye pia ni Diwani wa Buhembe na Meya wa zamani wa manispaa hiyo, Samuel Ruhangisa ambaye ni Diwani wa Kitendaguro. Wengine ni Dauda Kalumuna (Ijuganyondo); Deus Mutakyahwa (Nyanga); Robert Katunzi (Hamugembe); Richard Gasper (Miembeni) na Murungi Badru Kichwabuta (Viti Maalum). Hata hivyo, Mushi, alisema kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa hakikuchukua hatua zozote dhidi ya Ngaiza kama Mwenyekiti wa chama wa wilaya badala yake suala lake litapelekwa ngazi za juu za chama.
Siku moja baada ya kufanyika maamuzi hayo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, aliitisha mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi na kutangaza kubatilishwa kwa maamuzi ya CCM Mkoa wa Kagera, akisema kuwa taratibu hazikufuatwa ikiwamo kutowapa watuhumiwa fursa ya kujitetea. Nape alisema kwa mujibu wa taratibu CCM, Mkoa wa Kagera walitakiwa kuwasilisha tuhuma hizo ngazi za juu ili zijadiliwe na kuamuriwa na Kamati Kuu (CC). Aliongeza kuwa kwa mujibu wa taratibu, viongozi wa kuchaguliwa na wananchi kama wabunge na madiwani, hawawezi kuvuliwa uanachama na vikao vya chini bali chombo chenye mamlaka hayo ni CC.
Nape alisema kuwa CC ambayo itakutana mjini Dodoma Agosti 23, mwaka huu na suala hilo litakuwa miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa na kufanyiwa maamuzi. Katika hali ya kushangaza, CCM mkoani Kagera jana kilisiisitiza kuwa uamuzi wa kuwafukuza madiwani hao ni halali, kwa kuwa ulifanywa na kikao halali kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho. Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Kagera, Costansia Buhiye, alisema kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho, hakuna kikao chochote ndani ya chama kinachoweza kukinzana na kikao kingine kwa hivyo, bado madiwani hao wamefutiwa dhamana ya uanachama kama mkoa ulivyoamua.
Buhiye alisema kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa ndicho kikao kikuu chenye maamuzi ya kumwajibisha mwanachama yeyote iwapo atabainika kwenda kinyume cha taratibu na kanuni za chama, kwa mujibu wa katiba ya CCM. “Mpaka sasa maamuzi yaliyofikiwa ya kuwafukuza madiwani wanane ndani ya manispaa ya Bukoba ni halali, kwa mujibu wa kanuni na katiba yetu vikao vya chini vya CCM viheshimu vikao vya juu na pia vikao vya juu viheshimu maamuzi ya vikao vya chini, na kuwa viongozi waliowajibishwa wamo ndani ya mamlaka ya Halmashauri Kuu ya Mkoa,” alisema.
Alisema baada ya kikao walimwagiza katibu wa CCM, ambaye ndiye mtendaji wa chama mkoa aandae taarifa ya maamuzi yao na kuzipeleka ngazi zinazohusika na pia aandae barua kwa ajili ya waliofukuzwa uanachama na kuwa ana imani kazi hiyo ilifanyika. Buhiye hadi sasa hawajapata taarifa yoyote ya maandishi kutoka kwa uongozi wa ngazi za juu na wala kutoka kwa waliowajibishwa. Akizungumzia kauli iliyotolewa na Nape kuhusiana na uamuzi wa CCM mkoa, Buhiye alisema yeye binafsi hakusikiliza kilichoongelewa na kiongozi huyo, hivyo hana uhakika kama yanayodaiwa kusemwa aliyasema kwa kuwa Nape anaelewa kanuni na miongozo ya katiba ya CCM juu ya vikao na uhalali wake. “Ninachoweza kusema sipingani na Nnauye, ila ninachoweza kuwahakikishia ni kwamba hakuna kikao kinachoweza kufuta kikao kingine,” alisema.
KAULI YA NCHEMBA
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba, alipoulizwa na NIPASHE kuhusiana na kauli ya Mwenyekiti wa Mkoa wa Kagera, alisema anachozungumzia Mwenyekiti wa mkoa ni mapendekezo kwa kuwa maamuzi rasmi ya kuwatimua au la madiwani hao yatafanywa na CC katika kikao kitakachofanyika mjini Dodoma wiki ijayo. Nchemba alisema kuwa kwa mujibu wa katiba ya CCM, chama Wilaya ya Bukoba na Mkoa wa Kagera walitakiwa kupendekeza kwa CC na kwamba kimsingi, ngazi ya wilaya na mkoa wamemaliza kazi yao ya kutoa mapendekezo na kwamba CC ndiyo itatoa maamuzi ya mwisho wiki ijayo.
WALIOTIMULIWA WANENA
Wakati huo huo, baadhi ya hao wamekishukuru chama kwa kubatilisha uamuzi huo kabla hayajatokea madhara makubwa. Robert Katunzi , alisema amepokea kwa furaha maamuzi hayo yaliyotolewa na Katibu wa itikadi na Uenezi Taifa, Nape Nnauye, akisema maamuzi ya CCM mkoa yangesababisha mpasuko. Deus Mutakyahwa (Nyanga), aliishukuru CCM makao makuu kwa kufanyia kazi kwa haraka rufaa yao hali inayoepusha kutokea kwa mgawanyiko zaidi ambao unaweza kukiathiri chama.
Imeandikwa na Raphael Kibiriti (Dar); Kibuka Prudence, Lilian Lugakingira (Bukoba) na Godfrey Mushi, Moshi.
Source: Kibiriti R., Prudence K., Lugakingira L., & Mushi G. (August 2013). Madiwani Bukoba waigawa CCM. Retrieved from Ippmedia/ Nipashe
No comments:
Post a Comment