MSIMAMO KUHUSU RASIMU YA KATIBA MPYA YA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA
MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA
UTANGULIZI
Ndugu Msomaji wa “Msimamo wa CHADEMA kuhusu Rasimu ya Katiba
Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania: Mambo Muhimu ya
Kuzingatiwa”,
Katiba ni uhai wa Taifa lolote. Katiba ndiyo inayotuunganisha Watanzania, bila
kujali itikadi zetu, dini zetu, jinsia zetu, rika letu, makabila yetu, hali zetu na
tofauti zetu zozote. Katiba tunaweza kuiita Sheria Mama katika nchi. Hivyo hii
ni fursa pekee kwako Mtanzania kushiriki katika zoezi la kuandika Katiba mpya
ya Tanzania. Katiba zote zilizopita, pamoja na kuandikwa maneno ya kuvutia:-
" Kwa kuwa, Sisi Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua
rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya
uhuru, haki, udugu na amani"'
"Na Kwa kuwa misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye
demokrasia ambayo Serikali yake husimamiwa na Bunge lenye wajumbe
waliochaguliwa na linalowakilisha wananchi, na pia yenye mahakama huru
zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote, na
hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumishwa na kulindwa
na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu":-
"Kwa hiyo basi, Katiba Hii ( ya mwaka 1977) imetungwa na Bunge Maalum la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa NIABA ya WANANCHI....".
Pamoja na maneno hayo yenye kuleta matumaini katika Katiba ya sasa, yaani
ya Mwaka 1977, watanzania hawajawahi kushirikishwa kutunga Katiba ya
Taifa lao. Katiba hiyo ilitungwa na Chama Tawala na Serikali "kwa niaba yao",
Bunge lilitumika kama muhuri kwa kuhalalisha maamuzi ‘yao’.
Safari hii , Katiba Mpya inayoandikwa sasa, kuanzia hatua ya kukusanya maoni
ya wananchi, kujadili na kupitisha rasimu ya katiba katika Bunge la Katiba na
kuhalalisha katiba hiyo kupitia kura ya maoni; utaratibu wa kisheria wa ushiriki
na uwakilishi wa wananchi umewekwa ingawaje upo upungufu ambao
tutaendelea kuwaunganisha watanzania urekebishwe.
Ili kupata Katiba bora, inayobeba matarajio yetu Watanzania, ni muhimu
wananchi kuwa macho na mtu yeyote anayetaka kuhujumu Katiba mpya kwa
malengo yake binafsi au ya Chama chake. Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) kinasisitiza, wananchi mkiona ubinafsi wetu katika
Mapendekezo haya, yakataeni. Hivyo hivyo kwa Chama kingine chochote,
ikiwemo Chama cha Mapinduzi (CCM). Yatazamwe maslahi ya Taifa, na
mapendekezo ya chama kisichowakilisha maslahi ya wananchi na ya Taifa
katika ujumla wake yakataliwe bila kumumunya maneno.
Ni kwa msingi huo, Kamati Kuu ya CHADEMA, iliketi tarehe 6 na 7 July, 2013
katika Hoteli ya Blue Pearl Jijini Dar-Es--Salaam, na kupitia kwa kina " Rasimu
ya KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 2013". Aidha, kikao hicho
cha kamati kuu kilichambua kwa kina unaoitwa " Ufafanuzi kuhusu Rasimu ya
Kwanza ya Katiba kwa wanachama na viongozi wa CCM". Baada ya kutafakari
kuhusu nyaraka hizo, Kamati Kuu imefanya maamuzi ya kutoa msimamo wa
CHADEMA kuhusu rasimu ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania wenye kueleza mambo muhimu ya kuzingatiwa.
Pia, kamati kuu iliazima kwamba msimamo huu ufikishwe kwa njia mbalimbali
kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA kote nchini, wapenzi wa chama
na watanzania wote kwa ujumla wenye mapenzi mema na Taifa letu. Kamati
Kuu imebaini mambo kadhaa yanayoashiria kuwa wananchi wasipokuwa
makini na kusimamia maoni yao itatengezwa Katiba ya Serikali na CCM badala
ya katiba ya Watanzania.
Tunao ushahidi kamili kuwa: CCM wamedhamiria mambo yote wanayotaka
wao hata Kama siyo matakwa ya Watanzania yaingizwe ndani ya Katiba Mpya
kwa njia yeyote ile. Tunataarifa za kina kutoka maeneo mbalimbali juu ya wanayoyafanya kutimiza azma yao dhidi ya makundi mengine katika jamii na
wananchi kwa ujumla.
Kitendo cha CCM kuwapa msimamo katika vikao vya ndani wajumbe wa
Mabaraza ya Wilaya waliochaguliwa na wananchi kupitia mikutano ya vijiji ni
ishara ya wazi wa yote tuliyotahadhirisha juu ya uchujaji wa wajumbe kwenye
kazi ya kata zenye kuhodhiwa na CCM. Sasa hali hiyo inatumiwa kuathiri
maoni katika hatua ya mabaraza ya katiba yanayosimamiwa na tume ya
mabadiliko ya katiba.
CCM inafanya matendo hayo kwa kuwa haikuwahi kuwa na dhamira ya kweli
ya kuandika katiba mpya. Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ajenda ya Katiba
Mpya haikuwepo kabisa. Ajenda hiyo ilikuwa ndani ya Ilani ya CHADEMA na
ilikuwa kati ya masuala muhimu katika mikutano ya kampeni ya wagombea wa
CHADEMA wa udiwani, ubunge na urais.
Viongozi wakuu wa chama hicho wakati wote walikuwa wakiibeza ilani ya
CHADEMA kuhusu kuanzisha mchakato wa katiba mpya ndani ya siku 100
iwapo CHADEMA ingeongoza Serikali. Shinikizo la wananchi ambalo
liliongezewa msukumo na uamuzi wa wabunge wa CHADEMA kususia Hotuba
ya Rais ya Ufunguzi wa Bunge wakidai mabadiliko kuliwafanya walegeze
msimamo.
Hatua ilitanguliwa na kauli za viongozi waandamizi wa Serikali ya kwamba
“hakuna haja ya kuwa na katiba mpya”. Katika hali kama hiyo, tusipochukua
hatua watahujumu mchakato wa katiba na hivyo Tanzania kupata katiba mpya
isiyokuwa bora.
Hali hii inathibitishwa na maudhui ya waraka huo ulioitwa "ufafanuzi..."
uliotolewa na CCM ambao kimsingi unapinga mambo mengi muhimu katika
rasimu ya katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa
na Jaji (Mstaafu) Joseph Warioba.
Kati ya mambo wanayoyapinga ni pamoja na uwepo wa Serikali Tatu; yaani
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Zanzibar na Serikali
ya Tanzania Bara. Msimamo wa CHADEMA umeeleza mambo muhimu ya
kuzingatiwa kuhusu muundo wa Muungano wa Serikali tatu kwa mustakabali
mwema wa taifa letu.
CCM hawataki hata Tunu ya " UWAZI" uwepo kwenye Katiba ya Jamhuri ya
Muungano katika hali ile ile ya kuruhusu mianya ya kulea “UFISADI”.
CHADEMA kupitia msimamo huu imeunga uwazi kuingia katika katiba na
kutoa maoni ya tunu nyingine muhimu za kuongezwa katika rasimu ya Katiba
sanjari na kusimamia kwamba maadili na miiko ya uongozi iwe sehemu ya
mambo ya Muungano.
CCM inakataa haki za msingi za watanzania zinazohusu masuala ya ardhi,
maliasili na rasilimali ziingie katika katiba ya Jamhuri ya Muungano.
CHADEMA kupitia msimamo huu imetoa maoni ya namna vifungu vya haki za
binadamu vilivyomo vinavyopaswa kuboreshwa na kusimamia kwamba haki
muhimu ikiwemo juu ya rasilimali za nchi na maisha ya wananchi ziwe sehemu
ya mambo ya Muungano.
Mambo hayo na mengine yapo katika kijitabu hiki chenye sehemu saba za
“Msimamo wa CHADEMA kuhusu rasimu ya katiba mpya ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania: Mambo Muhimu ya Kuzingatiwa”. Soma, chambua,
tafakari na chukua hatua. Ukishasoma sambaza msimamo huu kwa wengine ili
watoe maoni tupate katiba bora. Natanguliza shukrani za dhati.
Mabadiliko ya Kweli, Uhuru wa Kweli.
Dr Willibrod Peter Slaa
KATIBU MKUU
CHADEMA
Julai 2013
No comments:
Post a Comment