Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, July 31, 2013

Makala: Serikali kuifumbia macho kashfa ya dawa za kulevya ni usaliti


M. M. Mwanakijiji
JESHI la Wananchi, Polisi, Uhamiaji na vyombo vingine vya usalama pamoja na baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara maarufu nchini wametajwa kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya ambayo imeharibu maisha ya maelfu ya vijana na kuvunja vunja familia. Taarifa za kuhusika huku kwa maofisa wa vyombo hivi vya usalama na watu mashuhuri zimekuja baada ya Mtanzania mmoja kukamatwa huko Hong Kong na kuandika barua ya kukiri kuhusika kwake na biashara hiyo pamoja na kuwataja watu waliomuingiza na kumwezesha kufanya biashara hiyo.

     Barua hiyo ilipostiwa katika mojawapo ya tovuti zinazofuatilia mambo ya dawa za kulevya na kubandikwa chini ya kichwa cha habari cha “Punda wa Madawa” kwenye mtandao wa waumini wa Kanisa Katoliki ambao umeundwa ili kuunga mkono mabadiliko na mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano. “Punda wa Madawa” ni jina linaloelezea watu wale wanaotumiwa na kutumika kusafirisha dawa za kulevya kutoka kwa wafanyabiashara wa jumla kwenda kwa wafanyabiashara wa reja reja. Watu hawa wanaweza kuwa ndani ya nchi au kati ya nchi na nchi. Mara nyingi – kama jina linavyoashiria – watu hawa ni vyombo tu vya vinara wa dawa za kulevya na lolote litakalowakuta huwa ni juu yao wenyewe. Hata hivyo, endapo wanafanikiwa kusafirisha ‘mzigo’ kutoka pointi moja kwenda nyingine basi huweza kulipwa vizuri na wengine huishi maisha ya kifahari kabisa kutokana na biashara hii.

    Kabla ya kuwataja watu ambao mwandishi anawatuhumu kujihusisha na biashara hii, anaelezea kwa kirefu jinsi alivyoingia katika mtego wa biashara hiyo na hatimaye kuangukia kwenye mikono mikali ya sheria ya polisi wa Hong Kong, China. Mwandishi anaelezea aliingia katika biashara hiyo baada ya shida za maisha kumzidia na kujikuta hana njia ya kupata kipato kingine halali ili kuisaidia familia yake. “Pamoja na misukosuko yote hiyo nilivumilia, lakini mtihani mkubwa ni pale kodi ya nyumba ilipoisha na mwenye nyumba akanipa ‘notice’ ya mwezi mmoja (nihame), au nimpe kodi ya miezi ya 360,000 tsh,” ameelezea mwandishi huyo ambaye hakuweka jina lake.

     Mwandishi huyo wa barua anadai kuwa baada ya kujitahidi kutafuta fedha hiyo na kushindwa, alijikuta ameomba msaada kwa marafiki zake ambao anawaita ‘wabaya’ kwani ni wao ndio walimchukua na kumpeleka kwa bosi wao ambaye alimlipia kodi ya miezi sita na kumpa fedha za ziada shilingi laki mbili. Tajiri huyo ni mtu anayeishi Magomeni Mwembechai jijini Dar es Salaam. Ni hapo ndipo alipoanza kupewa mazoezi ya kumeza vidonge vya heroine. Siku chache baadaye alipewa vidonge 93 vya dawa hizo ambavyo kila kimoja kina gram 15 kwa jumla ya gram 1,395 (sawa na paundi tatu hivi). Kutokana na kuanza kupata matatizo na kutoka vidonda, kijana huyo alijaribu kutaka kuacha biashara, lakini akakumbushwa kuwa ana deni la sh 560,000 na upande mwingine aliahidiwa kuwa endapo angefikisha mzigo ule salama basi angelipwa dola 5,000. Akapewa mpango wa safari kwenda Hong Kong akiwa katika hali ya udhaifu mkubwa wa mwili.

     Mwandishi alitarajia akamatwe uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam. Haikuwa hivyo na kwa maelezo yake kijana huyo anasema: “Ajabu pale airport kulikuwa na mtu ambaye aliandaliwa kunipitisha mimi mpaka boarding room.” Ilikuwa ni hali aliyokuwa nayo ndiyo iliwafanya maofisa wa Hong Kong kumtilia shaka na kumweka kizuizini. Kitu ambacho mwandishi inaonekana hakuwa anakijua ni kuwa Hong Kong hawana huruma na watu wanaojihusisha na dawa za kulevya kwani wana vifungo vikali kabisa na kwa maelezo yake kuwa hadi hivi sasa kuna vijana wa Kitanzania karibu 150 ambao wameshafungwa na wengine wakiendelea kusubiri kesi zao ziendelee. Alichoshukuru mwandishi ni kuwa angalau yeye na wenzake wamekamatwa Hong Kong kwani kama wangekamatwa China yenyewe basi wangenyongwa kwani tayari – kwa maelezo yake – wapo vijana wa Kitanzania walionyongwa huko.

    Kwa maelezo yake ambayo yanashabihiana kwa kiasi kikubwa na taarifa za vyombo vya usalama vya kimataifa vinavyofuatilia biashara hii haramu mizigo ya dawa za kulevya yanaingia nchini Tanzania yakitokea Pakistani na Afghanistan kupitia maeneo ya Tanga, Dar es Salaam, Mtwara na Bagamoyo ambazo huja kwa boti na kupokelewa na wahusika wakubwa nchini. Mwaka jana mtoto mmoja wa aliyekuwa afisa wa Benki Kuu ya Tanzania alikamatwa na wenzake huko Lindi akiwa na mzigo wa dawa za kulevya wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 9.

    “Mizigo hiyo huwa inasindikizwa na magari ya jeshi na polisi na hii siyo siri kwani hata wahusika wanajua,” anasema kijana huyo. Kuhusishwa kwa vyombo vya usalama na biashara hii haramu si jambo la kushangaza. Ipo mifano ya baadhi ya watumishi wa vyombo vya usalama waliokamatwa:
  • Mwaka 2011 – Mwanajeshi wa JWTZ alikamatwa mjini Morogoro akijaribu kusafirisha magunia 12 ya bangi kutoka Iringa kuja Dar es Salaam. Hii ilikuwa ni mwezi Desemba mwaka huo. Kijana huyo wa miaka 26 alikamatwa na askari polisi waliokuwa doria akiwa amevaa sare za jeshi hilo. Ni ofisa wa Kambi ya Lugalo mwenye namba MT86879.
  • Januari 2013 – Ofisa wa JWTZ mwenye namba MT 59503 Sajenti Aziz Athumani alikamatwa huko Arusha akiwa na pembe mbili za ndovu.
  • Aprili 2013 - Askari wa Magereza Brighton Octavian alikamatwa katika gereza la Keko akiwa na kete 732 ambazo inadaiwa alikuwa anazipitisha kwenda kwa wafungwa. Kuna ushahidi mkubwa wa uwepo wa mtandao wa kihalifu wa maofisa wa Magereza ambao wamekuwa wakitumiwa na wafungwa kupeleka habari nje au ndani kutoka kwa mabosi wa dawa za kulevya nchini.
  • Julai 2013 – Hivi majuzi tu mwanajeshi mwingine Seleman Chasama (50) katika hali ya kushangaza akili kabisa, amefikishwa mahakamani akishitakiwa makosa ya uhujumu uchumi na yale ya uhifadhi wa wanyama pori baada ya kukutwa na pembe 357 za ndovu zenye thamani ya dola milioni 2.6.
  • Julai 2013 – Maofisa waandamizi wa Jeshi la Magereza akiwemo Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP) Joseph Sauli, Warden Richard Barick na Koplo Silvester Bukha walikamatwa na twiga wawili, pundamilia wawili, swala palapala wawili na mbuni wawili, wote wakiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 55.
     Hiyo ni mifano michache tu ya kuhusishwa kwa maofisa wa usalama na mambo ya ujangili, dawa za kulevya na hapo hatujaangalia uhalifu mwingine. Na hapa izingatiwe hawa ni wale ambao walikamatwa tu na hatujaangalia wale wa polisi ambao kama watu wanakumbuka waliwahi kutuhumiwa kujaribu kumtegeshea mtoto wa Mzee Mengi dawa za kulevya pale Uwanja wa Ndege na barua hii inatupa mawazo tu jinsi gani hilo linaweza kutokea kweli. Ikumbukwe barua hii imekuja tayari kukiwa na habari za mabinti wawili wa Kitanzania wamekamatwa Afrika Kusini baada ya kutua nchini humo na mzigo wa dawa za kulevya wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 6; na hawa waliondokea Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam. Bila ya shaka kuna kuhusika kwa maofisa wa kikosi cha Uhamiaji ambao wana wajibu wa kusimamia watu wanaoingia na kutoka nchini.

      Vilevile, barua hii imekuja siku chache tu toka Mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere (CHADEMA) kuzungumza na waandishi wa habari kutaka serikali ijisafishe kwani inaonekana kuwaogopa vinara wa dawa za kulevya. Katika tamko lake la Julai 19 Nyerere ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani alisema kwa ukali kuwa; “Kupuuzia na kutochukua hatua kwa wahusika wa dawa za kulevya ni kuangamiza nguvu kazi ya taifa ambayo ikishaharibiwa na dawa za kulevya hatuna taifa tena. Hivyo serikali ifahamu kwamba kuendelea kulifumbia macho jambo hili kwa manufaa ya mafisadi wachache ni kulihujumu taifa na huo ni usaliti dhidi ya kiapo ilichokula cha kulitumikia taifa na kusimamia ustawi wa wananchi wa Tanzania.

    “Aidha, serikali itambue pia kwamba kuendelea kukaa kimya bila kuchukua hatua yoyote juu ya jambo hili kunatoa dalili kwamba yamkini na yenyewe inahusika na biashara hiyo.” Katika kuhitimisha barua yake, mwandishi wa barua hiyo alienda mbali na kuwataja baadhi ya watu ambao wanahusika na mtandao wa dawa za kulevya na namna ya ushiriki wao huku akisema kuwa wapo wengine ambao majina yao yakitajwa nchi itashituka kwani ni watendaji wa ngazi za juu serikalini. Barua yake hiyo ilitumwa kwa vyombo mbalimbali vya habari vya Tanzania. Kitu kimoja ambacho kiko wazi ni kuwa kijana huyo amefanya kile ambacho watu wengi wameshindwa kukifanya.

     Kukithiri kwa biashara hii nchini kunafichua tu kundi ambalo limejikita kwenye madaraka, ambalo licha ya kufanya vitendo vya ufisadi serikalini lipo pia kwenye mtandao wa uhalifu (organized crime) na limejipenyeza hadi kwenye vyombo vya dola. Barua ya kijana huyu kuhusisha vyombo vya usalama yaweza kuwa ni andiko la mwisho kwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuangalia utendaji wa vyombo vyake ambavyo anaonyesha kuwa anaviamini sana. Je, serikali itapokeaje taarifa hii? Je, kuna mtu mwenye ujasiri wa kupambana na kuufumua mtandao huu? Je, kama kijana huyu kawataja majina na mahali je, Serikali ya Tanzania ina maana kuwa miaka yote hii haikuwajua? Na Rais Kikwete anahalalisha vipi kuendelea kuwatumia watu wale wale walioshindwa kusimamia usalama? Kama yaliyomo kwenye barua hiyo ni kweli je, tunaweza kusema kweli nchi iko salama? Salama kwa nani?

Maswali mawili ya kujiuliza na kufikirisha:
  1. Kwa kila dawa zinazokamatwa na kwa kila watuhumiwa wanaokamatwa ni wangapi wanafanikiwa kupita na kuishia mitaani au nchi jirani?
  2. Je, majina ya hawa waliotajwa yamo kwenye ile orodha aliyopewa Rais Kikwete, au ile ya viongozi wa makanisa au ile ya Kikosi cha Kuzuia Dawa za Kulevya?

No comments: