Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amezidi kuifyatukia Rasimu ya Katiba Mpya kwa maelezo kwamba mchakato wake umelenga kuvuruga Muungano na kuibebesha mzigo serikali. Amesema rasimu hiyo inahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa hasa katika kipengele cha Muungano. Alitoa kauli hiyo alipohojiwa na waandishi wa habari akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya tatu ya Chuo cha Ualimu Kibamba (KTC). “Sasa tuwe wazi tunampa nani kazi hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali anasema mchakato huo utaanza April mwakani, tutakuwa tumechelewa sana hivyo nadhani Tume ya Warioba (Jaji Mstaafu Joseph) ingewachukua wale Watanzania Bara wakakabidhiwa kwa namna fulani kisheria kushughulikia mambo yote ambayo yanahusu bara hapo ndio utaona sasa Muungano unakuwaje,” alisema Sitta.
“Utawapataje wabunge wa Bunge la Bara kwani lazima tuwe wazi fomula itakuwa ile ile au na kama ni ile ile ina maana kila jimbo litakuwa na wabunge wawili kwa jumla tutakuwa na wabunge kama 400 itakuwa ni mzigo kwa Tanzania. “ Je, viongozi wataitwa nani, tukiwa na Rais wa Tanganyika ina maana nchi itakuwa kiroja kwa kuwa na marais watatu, hivyo wananchi mnakubali kuwapo na mzigo wa namna hiyo na hata itifaki yake itakuwa ni tabu tu,” alisema Waziri Sitta. Alisema tatizo analoliona ni viongozi kuwa kama wanajitafutia ulaji ndani ya katiba mpya, haelewi ni kwanini Tume ya Jaji Warioba imependekeza mawaziri 15 wakati masuala ya muungano yapo saba.
“Kwa nini tuwe na mawaziri 15? Ni dhahiri kuwa Serikali ya Muungano itakuwa ndogo kabisa na masuala mengine sio lazima yawe yanashughulikiwa na wizara. Kwa mfano suala la uraia huwezi kuanzisha wizara ya uraia hivyo bado kuna kazi ya kufanya, isitoshe serikali za mtaa zitakuwa hizi hizi za sasa na hizi nazo zitakuwaje,” alihoji Sitta. Alisema anashindwa kuelewa viongozi wa Mkoa na wa Wilaya wataitwa akina nani yaani bado kuna kazi kubwa huwezi kumalizia Katiba ya Muungano kama hujui Tanganyika hatma yake ikoje. Sitta alisema angalau Zanzibar kuna katiba na hiyo nayo inahitaji mabadiliko kwa sababu haya mambo ya kila mtu kuitwa Rais hayana tija hata kidogo. Nchi kama ina shirikisho rais awepo mmoja na hata ikiahirisha sasa linapokuja suala la Afrika Mashariki tutakuwa na rais mmoja… “Tuanze kuzoea watu wengine kutoitwa rais,”
SERIKALI YA KIKWETE INAHUJUMIWA
Akizungumza wakati akihutubia katika mahafali hayo, Sitta alisema kuna tabaka lilolojengeka la wenye fedha ambalo linahujumu Serikali ya Rais Kikwete na hivyo kukwamisha juhudi zinazofanywa na Rais. Aidha, alisema kuna haja ya serikali kuwachukulia hatua kali wale wote ambao wanafanya ufisadi ili kurejesha maadili ya nchi. Aliongeza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakishirikiana na viongozi wa serikali katika kufanya masuala ya ufisadi jambo ambalo linahujumu nchi. Alitoa mfano wa nchi ya China ambapo kiongozi ama mtu yeyote ambaye atabainika ni fisadi huuliwa kwa risasi na kwamba hali hiyo kwa Tanzania imekuwa ikizuiliwa kwa madai ya haki za binadamu.
Alisema watu wanashuhudia vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano ambavyo vinatokana na kukosekana kwa huduma za afya kutokana na wananchi hao kuiba rasilimali za nchi. “Watu hawa ni wauaji hawana tofauti na yule anayeua kwa kisu hii ni hatari,” alisema. Alisema kuna baadhi ya viongozi badala ya kuwasaidia wananchi wamekuwa wakijilimbikizia mali pamoja na fedha huku wakihujumu serikali ya Rais Kikwete. Alisema watu hao wamekuwa wakiiwaibia wanyonge na kutorosha fedha nje ya nchi ambazo zingetumia kusaidia kufanya shughuli za maeneleo na kuboresha huduma kwa Watanzania.
MABILIONI YA USWISI
Alisema fedha sh.bilioni 300 ambazo zimehifadhiwa Uswisi hazina uhalali na kuhoji iweje hapa nchini ziwepo benki zaidi ya 50 halafu zikahifadhiwe fedha nje ya nchi. Aliongeza kuwa fedha hizo zingeweza kusaidia kutatua matatizo mbalimbali pamoja na kuboresha masuala ya kijamii. Waziri Sitta alisema kitendo cha kufichwa kwa mabilioni hayo ya fedha ndio jambo ambalo limeanza kuiumiza nchi na madhara yake kwa sasa yameanza kujionyesha kwa wananchi. “Hii ni hatari yaani wananchi wana shida halafu wenzetu wanakimbilia kuyafisha mahela yao nje ya nchi, hizo fedha zirudishwe ziweze kuwasaidia wananchi,” alisema Sitta. Alisema kuna haja ya viongozi wa serikali kutimiza mahitaji ya wananchi bila kujilimbikizia mali kwani inajengwa Taifa kwa ajili ya wote na sio kujinufaisha watu wachache.
Source: Shayo B. ( June 2013). RASIMU KATIBA MPYA:Sitta afyatuka. Retrieved from Ippmedia/ Nipashe
No comments:
Post a Comment