Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Sunday, June 9, 2013

Mgawanyiko mpya CCM:Watumia udini kupitisha bajeti



       Mgawanyiko umeibuka miongoni mwa wabunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ukihusishwa na masuala ya udini katika kupitisha bajeti za wizara zilizowasilishwa bungeni. 
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya kamati ya wabunge hao, vimeeleza kuwa, licha ya chama hicho kuwa katika makundi yanayopingika kwa misimamo, wameibuka wabunge wanaotumia mianya ya kidini kupenyeza ajenda zao. Hata hivyo, hali inaelezwa kuwa mbaya na inayohatarisha uhai wake, na kwamba jitihada za makusudi zinapaswa kufanyika kuwadhibiti ‘waasisi na watetezi ’ wa mgawanyo huo. Mbunge wa Mchinga, Saidi Mtanda, anatajwa kuwa nyuma ya mkakati unaojikita katika misingi ya kidini, hususani alipochangia hoja katika hotuba ya bajeti ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa.

         Moja ya hoja iliyojengwa na Mtanda katika kuichangia bajeti hiyo, ni kuhoji sababu za kutofautiana kwa alama za ufaulu wa kimadaraja, kati ya wanafunzi wanaosoma elimu ya dini ya kiislamu na ile ya kikristu. Kama vile haitoshi, Mtanda anaelezwa kukitumia kituo kimoja cha luninga kupitia moja ya vipindi vyake vya asubuhi, kujenga hoja zinazoashiria kuwapo ‘ubaguzi’ wa kidini katika wizara hiyo. Wakati bajeti ya wizara hiyo ikiendelea kujadiliwa bungeni, vyanzo vyetu vinaeleza kuwa, wakati kasi ya hoja zilizojikita katika udini ‘zikiwatafuna’ wabunge wa CCM, Waziri Mkuu ambaye ni kiongozi wa kamati ya wabunge wa chama hicho, hakuwepo mjini Dodoma. Hivyo, nafasi yake ilichukuliwa na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, aliyeongoza kikao kimoja kilichoitishwa ghafla kulijadili suala hilo.


        Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho, zilieleza kuwa Mtandao na wabunge wengine, waliungana kutaka suala ya ‘ubaguzi dhidi ya waislamu’ lishughulikiwe, hususani katika kuijadili bajeti ya Dk Kawambwa. “Tunapokwenda hapaonyeshi dalili nzuri kwa chama chetu,” alisema mbunge mmoja kutoka mikoa ya kanda ya ziwa, akitaka jina lake lisitajwe gazetini. Mbunge mwingine kupitia Viti Maalum, alisema mgawanyiko unaoachwa kukua miongoni mwa wabunge wa CCM, ukielekezwa katika misingi ya udini, utakiathiri chama hicho na kuigawa jamii ya Watanzania. “Inakuwaje Mbunge wa chama tawala, hata kama ni mawazo yake binafsi, anajielekeza katika kuchochea tofauti za kidini, anajenga hoja kumtetea Waziri kwa misingi ya dini, tunakwenda wapi,” alihoji

         Hata hivyo, inaelezwa kwamba kasi ya hoja zinazojikita katika udini, ‘ilizimwa’ na Sitta ambaye hakuongoza kutoa mapendekezo ama mwongozo wa kuchangia bajeti ya Dk Kawambwa, badala yake alisema kila mmoja awasilishe mawazo huru, ingawa yenye kuisaidia ipite. “Kama Sitta angeruhusu mjadala ule uendelee, ni wazi kwamba mambo yangekuwa mabaya zaidi…haistahili kuendekeza hoja hizi za kidini,” kilieleza chanzo chetu. Hata hivyo, akizungumza na mwandishi wa habari baada ya kuchangia hotuba ya Dk Kawambwa, Mtanda, alisema ni dhana potofu ‘kumhukumu’ kwamba anahusika na hoja za kidini.

     “Mimi ninazungumza hoja kwa vielelezo, sasa watu wasikimbilie kunihukumu kwa udini bali kuzijibu hoja kwa ufasaha,” alisema. Mtanda alitoa pia kauli kama hiyo kabla ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Dk Kawambwa, akijiweka kando na udini katika hoja zake. Sitta anayedaiwa kukabiliana na wakati mgumu wakati mjadala uliojikita kwa misingi ya udini alipotakiwa kulielezea suala hilo, hakuwa tayari.

Source: Ippmedia ( June 2013).Mgawanyiko mpya CCM:Watumia udini kupitisha bajeti . Retrieved from Ippmedia/ Nipashe

No comments: