Wakati Watanzania wakilalamikia mwenendo usioridhisha wa uendeshaji wa vikao vya Bunge, Naibu Spika, Job Ndugai, ameibuka na kusema kuanzia sasa mbunge kutoka chama cha upinzani akifanya kitendo chochote cha utovu wa nidhamu bungeni hatachukuliwa hatua za kinidhamu. Akizungumza katika mahojiano maalum na kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One, alisema wabunge watakaokuwa wakichukuliwa hatua wanapofanya vitendo vya utovu wa nidhamu ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pekee.
Ndugai alisema uamuzi huo unatokana na kwamba yeye na wenzake kwa maana ya Spika Anne Makinda na wenyeviti wanapochukua hatua kwa wabunge watovu wa nidhamu cha kushangaza wao wanaonekana ndiyo tatizo huku waliofanya vitendo hivyo wakionekana mashujaa. “Kama unaweza kuchukua hatua kwa watovu wa nidhamu halafu huyo mtovu wa nidhamu akageuka kuwa shujaa basi ujue hiyo jamii ina matatizo makubwa sana na jamii yetu imefikia hapo, wapo wabunge wa vyama fulani fulani ambao hata wakifanya jambo la utovu wa nidhamu lakini mwisho wanaonekana mashujaa,” alisema Ndugai.
Ndugai alisema Watanzania lazima watambue kuwa suala la utovu wa nidhamu lazima likemewe kwa wabunge wote. “Kwa sasa hivi tunawaacha akifanya utovu wa nidhamu mbunge wa Chadema hatachukuliwa hatua ila akifanya wa CCM tutamdhibiti kwa sababu ‘media’ zinawabeba sana wabunge wa Chadema hata wafanye nini anayeonekana mbaya ni spika au mwenyekiti sasa nani atakubali aonekana ni mbaya,” alihoji Ndugai. Ndugai alisema yeye binafsi anapochukua hatua dhidi ya mbunge wa Chadema anapofanya vitendo vya utovu wa nidhamu amekuwa akilaumiwa, hivyo amenyoosha mkono na sasa atawaacha ili Watanzania wenyewe waamue kusuka au kunyoa.
Alisema kama Watanzania wanataka nidhamu iwapo bungeni hatua zinapochukuliwa kwa wahusika hakuna sababu ya kuwanyooshea vidole waliotoa maamuzi hayo. “Siku zote tunapochukua hatua tunaonekana matahira na mazezeta basi tunawaacha. Waisrael walipoulizwa mnamtaka Barnaba au nani wakasema Barnaba ili Yesu asulubiwe,” alisema Ndugai. Naibu Spika alisema wabunge waliochana nyaraka wakati wa mjadala wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa hawatatuchukuliwa hatua kwa sababu wakichukuliwa hatua kiongozi unayekuwa kwenye meza ndiye unaonekana mbaya.
Uamuzi wa Ndugai umekuja wakati ambao viongozi wa Bunge wakilaumiwa kuwakandamiza wabunge wa upinzani hususani wa Chadema, lakini pindi mbunge wa CCM anapokashifu au anapotumia lugha ya kuudhi ndani ya Bunge anaachwa. Kwa mara kadhaa, wabunge wa Chadema wametolewa nje na askari kwa madai ya kutumia lugha ya kuudhi, lakini haikuwahi kufanywa hivyo kwa wabunge wa CCM hata pale wanapokosea. Mathalani, wakati wa hoja ya mitalaa iliyowasilishwa na mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, kiti kilishindwa kumwagiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kuwasilisha nakala za mitalaa kama alivyokuwa ameomba mbunge jambo lililoibua mjadala usio wa lazima.
Hivi karibuni, mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiel Wenje, alilazimishwa kuomba radhi baada ya kusema kwamba baadhi ya vyama vinauhusiano na vyama vya kiliberali ambavyo vinaunga mkono ndoa za jinsia moja; na kiti kuruhusu mjadala ulioibua mvutano mkubwa bila sababu.
Source: Mwanakatwe T. (May 2013). Ndugai aridhia vurugu bungeni. Retrieved from Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment