Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnein Murji jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani hapa akituhumiwa na kosa la uchochezi. Baada ya kusomewa shtaka hilo, mbunge huyo alirudishwa rumande kutokana na kushindwa masharti. Sharti hilo lilikuwa ni kuwa na pasi ya kusafiria, ambayo alikuwa ameiacha Dar es Salaam alikokamatwa. Murji amepandishwa kizimbani ikiwa ni moja ya mkakati wa vyombo vya dola kuwasaka na kuwafungulia mashtaka watu inaowatuhumu kuhusika kuchochea vurugu ambazo chanzo chake ni kupinga ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Mwendesha Mashtaka ambaye ni Wakili wa Serikali, Zuberi Mkakatu aliieleza Mahakama kuwa mnamo Januari 19, mwaka huu, maeneo ya Ligula mkoani hapa mtuhumiwa alichochea watu kutenda makosa. Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mtwara, Dynes Lyimo alisema dhamana iko wazi kwa mshtakiwa kwa masharti matatu. Kuwasilisha hati ya kusafiria mahakamani na kuwa na mdhamini mmoja mkazi wa Mtwara ambaye atasaini mali isiyohamishika isiyopungua Sh20 milioni. Sharti la tatu lilikuwa mshtakiwa kutoruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara pasipo kibali cha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara.
Mbunge huyo anayewakilishwa na Wakili Chaula Msechu alifikishwa mahakamani hapo jana saa 3.15 asubuhi akiwa katika gari la polisi huku ulinzi ukiwa umeimarishwa. Polisi waliokuwa na silaha na wengine wakiwa na mbwa walikuwa wametanda mahakamani. Mbali ya mahakamani, polisi walikuwa wakipita katika barabara mbalimbali za Mtwara sambamba na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Licha ya matangazo mbalimbali ya polisi kwamba hakutakuwa na tishio la uvunjifu wa amani, baadhi ya wananchi waliogopa kufungua biashara zao na wengine wakikimbia mji.
Washtakiwa 91
Washtakiwa wengine 91 nao walifikishwa tena mahakamani hapo katika kesi inayowakabili ya uchochezi, uharibifu wa mali kwa makusudi pamoja na kufanya mkusanyiko usiokuwa halali. Kesi za washtakiwa hao ambao dhamana zao zilikuwa wazi kwa masharti tofauti, zimegawanywa kwa mahakimu watatu.
Source: Sanyiwa M. & Kimaro H. (June 2013). Mbunge wa CCM asota rumande. Mtwara. Retrieved from Mwananchi
No comments:
Post a Comment