TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
BARAZA LA VIJANA CHADEMA WAANDAA
KONGAMANO KUBWA LA ELIMU
KUTOKANA na kutambua kuwa moja ya
matatizo makubwa yanayowakabili vijana wa Tanzania kwa muda mrefu sasa ni
ukosefu wa elimu bora inayokidhi viwango vya kutoa taaluma na utaalam kwa ajili
ya mahitaji halisi ya jamii yetu, Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (BAVICHA) limeandaa kongamano kubwa la kujadili elimu na mustakabali
wataifa la Tanzania litakalofanyika mjini Dodoma siku ya Jumapili, tarehe 9, 2013,
Ukumbi wa Kilimani.
Kongamano hilo ambalo litawakutanisha
wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, vyuo vikuu, walimu pamoja na
wahadhiri, litajadili hali ya elimu nchini na mstakabali wa nchi yetu kwa miaka
50 hadi 100 ijayo, likijikita katika kuchambua namna mfumo wa uendeshaji na
usimamizi unavyosababisha kuporomoka kwa sekta hiyo nyeti na kisha kujadili
njia mbadala za kusaidia kuondoka hapa tulipokwama kama taifa.
BAVICHA limeandaa kongamano hilo,
wakati ambapo tayari viashiria vya matatizo makubwa katika mfumo wa elimu yetu
nchini yameanza kuonekana wazi wazi kupitia matokeo mabovu ya vijana
wanaohitimu ngazi mbalimbali za elimu nchini.
Aidha, kongamano hilo linafanyika
wakati huu ambapo serikali ya CCM imeweza kuonesha pasi na shaka yoyote, kiwango
cha hali ya juu cha kushindwa kusimamia na kuendesha sekta ya elimu ambayo
ndiyo injini ya taifa lolote lile linalotaka kupigania ustawi na maendeleo ya
watu wake, kwa vizazi na vizazi.
Pia BAVICHA inaandaa kongamano hili
baada ya serikali kupitia bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
kushindwa kuonesha ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili sekta ya elimu na badala
yake imeendelea na ubabaishaji ambao umetufikisha hapa kwenye anguko na janga
kubwa la kizazi cha leo na kesho kutokana na kuporomoka kwa elimu yetu.
Baada ya uchambuzi wa hoja
zitakazoibuliwa wakati wa mjadala wa kongamano hilo, BAVICHA itawasilisha maoni
yake kwa chama ikiwa ni sehemu ya mchango wa vijana wa Tanzania, kuboresha sera
ya CHADEMA katika elimu.
Maoni hayo yatasaidia CHADEMA
kuendelea kusimamia na kusukuma agenda hii muhimu ya elimu katika nchi hii,
tukitambua kuwa chama kimeshaazimia kuifanya elimu kuwa ni kipaumbele namba
moja, namba mbili, kati ya sera kuu tulizonazo kwa ajili ya mawazo mbadala kwa
maendeleo ya taifa letu.
Imetolewa leo, Dar es salaam na;
Deogratias Munishi
Katibu
Mkuu BAVICHA
No comments:
Post a Comment