Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, March 27, 2013

Watanzania wapoteza imani na jeshi la polisi



INAELEWEKA kuwa Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kulinda raia pamoja na mali zao, lakini hivi sasa hali imekuwa tofauti. Polisi, ambao wanalipwa mishahara kutokana na kodi za walalahoi, hivi sasa wamegeuka na wakati mwingine huwanyanyasa wananchi kwa kuwaua ovyo bila hatia.  Tumeshuhudia matukio mengi mabaya ambayo polisi wetu wanayafanya bila hata chembe ya haya.  Polisi wa leo wako radhi kuwatetea wanasiasa kwa kuwalinda hata pale uhalifu wao unapoonekana hadharani. Wapo kwa ajili ya kuitumikia na kuilinda Serikali hata pale ambapo mambo ya ajabu yakionekana kufanywa na viongozi wetu waliopo serikalini. Siko kwa ajili ya kushabikia upande wowote, bali niko kwa ajili ya kueleza ukweli ambao unaonekana mbele ya macho ya wengi. Ikizingatiwa Watanzania wa leo wameamka si kama wale wa miaka ya 47, ambao hata kama wanaonewa wao wanakubaliana na hali hiyo tu pamoja na kile kinachosemwa na viongozi, hata kama kinahatarisha maisha yao.

Watanzania wa sasa wanajua kudai haki zao za msingi na wala hawaogopi tena. Tukiachana na hayo, hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alitangaza kumsimamisha kazi msaidizi mwandamizi wa polisi aliyekuwa anasimamia ajira katika jeshi hilo, Renatus Chalamila. Chalamila amepewa likizo ya mwezi mmoja, baada ya kutajwa mara kadhaa kuwatoza fedha vijana wanaoomba ajira za uaskari. Mbali na Chalamila, pia maofisa wengine watano wa jeshi hilo walisimamishwa kazi na wanatarajiwa kufunguliwa mashitaka ya kijeshi kutokana na tuhuma mbalimbali za ukiukwaji wa maadili na taratibu za jeshi hilo.  Ni dhahiri kuwa ndani ya Jeshi la Polisi kuna madudu yanayafanyika, ikiwemo rushwa na mambo mengine mengi ya ajabu na ya aibu. Tunashuhudia kwa macho yetu jinsi watu wanavyotekwa, kupigwa vibaya, kung’olewa viungo mbalimbali vya miili yao kama tulivyoona mwaka jana kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka. Pamoja na utekaji huo na utesaji aliofanyiwa Dk. Ulimboka, lakini mpaka leo tume iliyoundwa haijatoa majibu kuchunguza, hakuna aliyekamatwa kuhusika pamoja na tume iliyokuwa imeundwa ili kuchunguza waliohusika.

Lakini badala yake, Kamanda Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliutangazia umma kuwa mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni raia wa Kenya, amehusika katika tuhuma hizo na kwamba raia huyo alikwenda kutubu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Kawe. Baada ya Kamanda huyo kumtangaza raia huyo, Mchungaji wa Kanisa hilo, alikanusha vikali kuwa hakuna raia yeyote aliyefika katika kanisa hilo na kutubu kuwa alihusika katika tuhuma hizo. Pamoja na kwamba raia huyo kesi yake inaendelea mahakamani hadi leo hii, lakini bado Watanzania hawana imani na taarifa hiyo iliyotolewa na Kova na wanaona kama ilikuwa ni njia ya kuwanyamazisha watu ili wasiendelee kuwahofia baadhi ya watendaji wa serikalini ambao inadaiwa huenda wakawa walihusika. Wakati matokeo ya tume iliyoundwa kwa ajili ya Dk. Ulimboka hayajapatikana, lakini majuzi tulishuhudia tena tukio la aina hiyo alilofanyiwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, ambaye bado yuko kitandani akiendelea na matibabu.

Naye aliundiwa timu ya kuchunguza tukio hilo na mpaka leo hakuna aliyekamatwa hata mmoja, lakini polisi hao wamekuwa wepesi kumkamata Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, baada ya kuonekana kwenye video katika mitandao ya jamii akipanga kufanya vitendo vya kigaidi, ikiwa ni pamoja na kudhuru watu mbalimbali, wakiwemo waandishi wa habari. Watanzania wanahoji ni kwa nini huyo ofisa anayedaiwa kuwa ni wa serikalini, Ramadhani Ighondu, aliyewahi kutajwa na Dk. Ulimboka kuhusika katika tukio la kutekwa kwake na kuteswa, hajakamatwa na kufikishwa mahakamani? Pia wanahoji nguvu kubwa iliyotumika kuwasaka na kuwatia nguvuni waliotuhumiwa na mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Marehemu Liberatus Barlow, ambao walikamatwa ndani ya siku 12 tu baada ya kifo chake. Kwa mlolongo wote huo, Watanzania wamekata tama, hawana imani tena na jeshi lao na hata pale mtu anapoona anaonewa wanashindwa kupeleka malalamiko yao kwa polisi, wakidhani wanapoteza tu muda wao kwa sababu haki haiwezi kutendeka. Walalahoi wanalilia Jeshi lao la Polisi kwa kujiingiza kwenye siasa na rushwa, wamekata tamaa, hawana la kufanya.

Polisi jengeni heshima, imani imepotea.


Source: Hombo E. (March 2013). Watanzania wapoteza imani na jeshi la polisi. Retrieved from Mtanzania

No comments: