Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Tuesday, March 26, 2013

Uharamia hautainusuru CCM


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimo katika wakati mgumu wa kutaka kurejesha ushawishi wake wa kisiasa kwa Watanzania na kuzima nyota ing’aayo ya chama kikuu cha upinzani nchini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho katika miaka ya karibuni kimejiimarisha na kugeuka kuwa mwiba mkali kwa CCM. Katika kuhakikisha wanarejesha uungwaji mkono wa Watanzania, CCM imekuwa ikijaribu mikakati na mbinu mbalimbali. Kwanza kilikuja na mkakati wa kuwataka wanachama wake wanaokabiliwa na tuhuma za ulaji rushwa na ufisadi kujivua uongozi wa chama hicho ili wasiendelee kukipaka matope chama chao, mkakati uliopata jina maarufu la “Kujivua gamba”. Hata hivyo, mkakati huo ulishindwa vibaya kwani wana-CCM wengi wanaotuhumiwa kwa rushwa na ufisadi waligoma kujivua uongozi, isipokuwa mtu mmoja tu, Rostam Aziz ambaye alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM taifa na pia Mbunge wa Igunga, aliyejivua nyadhifa hizo zote.


Baada ya kushindwa kwa mkakati huo, kiongozi mkuu wa chama hicho Rais Jakaya Kikwete alibadilisha mkakati kwa kuwataka wanachama wenzake wa CCM kuwaondoa madarakani Wana CCM wote wanaokabiliwa na tuhuma za rushwa na ufisadi kupitia uchaguzi mkuu wa chama hicho uliokamilika mwishoni mwa mwaka jana. Kuna ushahidi wa wazi kuwa pia mkakati huo umeshindwa vibaya kwani watuhumiwa wote wamerejea madarakani kwa kishindo, halmashauri kuu ya chama hicho inadhibitiwa na watuhumiwa wa rushwa na ufisadi na wapambe wao ni wazi matumaini ya Rais Kikwete na baadhi ya viongozi wa CCM kukiona chama chao kikizaliwa upya, kwa kuongozwa na watu wapya wasiokuwa na mawaa yameendelea kufifia. Hata hivyo, inaonekana Rais Kikwete hajakata tamaa ya kuleta mageuzi ndani ya chama chake ili kiweze kurejesha heshima yake ya zamani mbele ya Watanzania.

Na katika kuhakikisha hilo hivi karibuni rais ameunda kamati kuu mpya ambayo imewaweka kando watuhumiwa wa rushwa na wapambe wao, akiamini kuwa pengine hilo litakuwa jawabu la matatizo mengi yanayokikabili chama hicho na kukifanya kipoteze heshima na mvuto kwa umma. Lakini matarajio ya Rais Kikwete yanaonekana kukwama, Watanzania wengi bado hawakiamini chama chake, Watanzania wengi bado wanaamini CCM ni chama cha kifisadi, Watanzania wengi bado wanaamini CCM ni chama cha matajiri na kisichojali wanyonge, wengi wanaamini chama hicho bado kinaongozwa na wababaishaji na walaghai. Kutokana na kushindwa kufanikiwa inawezekana kabisa kwamba sasa CCM kimebuni mbinu mpya ya kupambana na CHADEMA. Ingawa haijathibitishwa, lakini wadadisi wa mambo ya siasa wanaamini CCM imeamua kutumia mbinu za kihalifu ambazo si tu kwamba zinahatarisha maisha ya baadhi ya watu nchini bali pia usalama wa taifa letu kwa ujumla.

Katika namna isiyo rasmi, chama hicho kinadaiwa kutumia baadhi ya watumishi wasio waaminifu wa vyombo vya dola kuwateka, kuwapiga, kuwatesa kuwajeruhi na hata kuwaua baadhi ya Watanzania wenye ushawishi katika jamii, kisha kukipakazia CHADEMA kuwa ndicho mhusika wa matukio hayo. Nasema hivi kutokana na kile kinachoendelea katika jamii yetu kwa waandishi wa habari kutekwa na kupigwa, lakini mbinu zimekuwa zikifanywa kuhusisha vurugu hizo na CHADEMA. Naamini CCM imekuja na mbinu hiyo kwa imani kuwa itasaidia kukichafua CHADEMA mbele ya macho ya Watanzania na kupoteza ushawishi na uungwaji mkono kinaoupata sasa. Tukio la karibuni la kutekwa, kupigwa, kuteswa na kung’olewa jicho kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa New Habari Corporation, Absalom Kibanda, na kufuatiwa na tukio la kukamatwa na kushitakiwa mahakamani kwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, kutokana na mkanda wa video uliosambazwa mtandaoni ukimuonesha Lwakatare akipanga kile kinachodaiwa na polisi kuwa mpango wa kumteka na kumdhuru Mhariri Mtendaji wa Mwananchi Communications, Denis Msacky, ni ushahidi wa wazi wa mchezo mchafu wa CCM na vyombo vyake dhidi ya CHADEMA.

Itakumbukwa kuwa mwanzo wa mwezi Januari, mwaka huu, Naibu Katibu Mkuu wa CCM upande wa Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba, aliutangazia umma wa Watanzania kuwa alikuwa na ushahidi wa mkanda wa video aliodai unaonesha viongozi wa CHADEMA wakipanga mipango ya kuua watu. Pamoja na kupewa changamoto na viongozi wa CHADEMA kwamba auwasilishe mkanda huo polisi ili wahusika washitakiwe, lakini tangu wakati huo mpaka leo Mwigulu hajasema kama mkanda huo aliupeleka polisi na polisi wenyewe hawajawahi kuueleza umma hatua waliyochukua dhidi ya Mwigulu. Ni kutokana na ukweli huo watu wengi tunaamini kwamba mkanda wa video uliosambazwa juzi mtandaoni na kusababisha Lwakatare kukamatwa na kushitakiwa, inawezekana ni sehemu ya mpango wa kuichafua CHADEMA. Wapo wanaoamini ni mkanda uliotengenezwa na baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola kwa niaba ya CCM na mkanda huo ni wa kupikwa kwa lengo moja tu la kuchafua taswira ya CHADEMA mbele ya umma. Kwa hiyo, mlengwa hapa si Lwakatare bali ni CHADEMA, Mwigulu na wenzake wanaamini kuwa CHADEMA itadhoofika na kupoteza ushawishi kwa wananchi ikiwa vyombo vya habari nchini vitaacha kuandika habari zake au vitaamua kukiandika vibaya, na vitafanya hivyo iwapo tu watafanikiwa kukichonganisha na wanahabari, iwapo watafanikiwa kuwaaminisha wanahabari kuwa CHADEMA ni adui wa wanahabari na watu wengine wenye kukikosoa.
Lakini mbinu hii nayo imeshindwa, Watanzania wengi sasa wana uelewa mkubwa wa mambo, wanaweza kufanya uchambuzi wa matukio ya kisiasa na kubaini mbivu na mbichi, wanaweza kuelewa propaganda chafu za watawala dhidi ya vyama vya upinzani vyenye nguvu, wengi wanakumbuka CCM na serikali zake mbili walivyoendesha mbinu kama hizi dhidi ya Chama cha Wananchi (CUF) miaka ya nyuma wakati chama hicho kilipokuwa na nguvu na tishio kwa chama tawala.

Wengi wanakumbuka tuhuma zilizowahi kutolewa mwaka 2000 na aliyekuwa mkuu wa Jeshi la Polisi nchini wakati huo, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Omar Mahita kwamba CUF kilikuwa kimeingiza nchini kontena la visu ili kivitumie siku ya uchaguzi na baada ya kutangazwa kwa matokeo ikiwa kitashindwa uchaguzi huo. Ukweli ni kwamba CCM kimeishiwa hoja, kwa sasa CCM hakiwezi kushindana kwa hoja na CHADEMA, hawana hoja ya kuwaambia Watanzania juu ya matatizo mbalimbali yanayoikabili nchi yetu, hata kama hoja wanayo lakini hakuna atakayewasikiliza kwasababu hawaaminiki kwa Watanzania, Watanzania wengi wanajua kuwa viongozi wengi wa CCM hunena wasichomaanisha, na humaanisha wasichokisema. CCM wanaelekea kufa kabisa kisiasa na ninawaonya kuwa njia waliyoamua kuifuata ya kutumia mbinu za kihalifu kupambana na CHADEMA ni kujimaliza zaidi, mbinu hiyo haina mwisho mwema kwao, uharamia hautawanusuru na kifo cha kisiasa, lazima watakufa tu ikiwa hawatarudi nyuma na kuangalia walipokosea. CCM wanapaswa kutafuta chanzo cha matatizo yanayokikabili leo chama chao, lazima watatafute chanzo cha kupoteza imani kwa wananchi walio wengi, hawana budi kutafuta chanzo cha kukataliwa na wananchi na kisha kutafuta majawabu madhubuti ya kukikwamua chama, si kutumia uharamia.

Source: Maziku G.(March 2013) Uharamia hautainusuru CCM. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: