Viongozi watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kata ya Ulemo wilayani Iramba, wamefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo ya
Kiomboi kujibu shitaka la kufanya fujo mkutanoni. Viongozi hao ni Mwenyekiti wa kata wa chama hicho, John Wilfred
(22), Katibu wa vijana wa kata, Kitila Gabriel (20), Mwenyekiti wa kata,
Emmanuel Reuben (27), Katibu mwenezi, Christopher Edso Shilla (33) na
mwanachama Kephasi Cyprian (35). Mlalamikaji katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa kijiji cha Ulemo,
Milton Nazael.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washtakiwa wanadaiwa kufanya
kosa hilo Machi 8, mwaka huu saa 5:15 asubuhi katika kijiji cha Ulemo wilayani
Iramba. Ilidaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja, wakati mkutano uliokuwa ukiongozwa na Mwenyekiti
huyo wa kijiji, bila halali na kwa makusudi, walifanya fujo na kusababisha
mkutano huo ushindwe kuendelea kama ulivyopangwa.
Hata hivyo, washtakiwa hao walikana mashitaka hayo na wapo nje
kwa dhamana ya Sh. 200,000 kila mmoja za maandishi hadi Aprili 4, mwaka huu
kesi hiyo itakapotajwa tena.
Source: Ismailly j. (March 2013). Viongozi watano wa Chadema washtakiwa kwa kufanya fujo. Retrieved from Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment