Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Thursday, March 21, 2013

Sakata la Lwakatare: Wanasheria CHADEMA ‘wafunguka’!



Kiongozi wa jopo la wanasheria watano (5) wanaomtetea Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, Wakili Tundu Lissu, akiwawakilisha wenzake, ameongea na vyombo vya Habari akiwa Makao Makuu ya CHADEMA na kuzungumzia masuala kadhaa kutokana na sakata hili. Lengo kuu la mkutano huo na wanahabari lilikuwa ni kuutarifu umma wa Watanzania kupitia kwa wanahabari juu ya hatua ambayo mawakili hao wameamua kuchukua kwa kupeleka ombi Mahakama Kuu ya Tanzania, chini ya hati ya dharura ili Mahakama hiyo ya juu iitishe mafaili yote mawili yaliyofunguliwa kuhusu kesi ya Lwakatare, yaani faili la kesi iliyofutwa na faili lililofunguliwa baada ya kesi ya awali kufutwa, wakiiomba mahakama iangalie na kujiridhisha…
Kupitia hati hiyo ya dharura, mawakili hao wanaiomba Mahakama Kuu:
- Ifute hati ya DPP iliyotolewa jana ikifuta mashtaka ya awali
- Ifute amri ya mahakama ya iliyotolewa kumaliza kesi iliyofunguliwa awali kabla ya kufutwa jana
- Ielekeze Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, itoe maamuzi kama ilivyokuwa imepanga kutoa kabla 'haijaingiliwa' kwa DPP kuifuta kesi mahakamani.
- Na pia wameiomba Mahakama Kuu, itamke kuwa hicho walichofanya waliomfungulia kesi Lwakatare ni matumizi mabaya ya;

1. Mamlaka ya DPP
2. Mfumo wa Mahakama na
3. Kuingilia uhuru wa Mahakama

Mbali ya maelezo hayo, Wakili Lissu pia amejibu maswali ya wanahabari, ambapo walitaka kujua masuala mbalimbali kuhusu kesi na mashtaka yanayomkabili Lwakatare, akisema: 
Mosi, Ili kosa liwe la kigaidi, ni lazima kuwepo maelezo yanayofafanua kuwa kuwa mtuhumiwa alikuwa na malengo au nia ya kigaidi; lakini hakuna maelezo ya namna hiyo kwenye hatia ya mashtaka kueleza ‘terrorism intention’. Alifafanua kuwa kwa maoni yake, Lwakatare amefunguliwa mashtaka ya kigaidi kwa nia tu ya kutaka asote gerezani, kwa sababu waliofungua mashtaka wametaka hivyo… ateseke!
Pili, Nolle prosequi iliyowasilishwa jana na DPP kufuta kesi iliyofunguliwa Jumatatu Machi 18, 2013 kwa ridhaa yake inazua maswali sana (questionable) sana kwasababu hakuna mahali mazingira yanaonesha iliwasilishwa kukidhi masuala mawili muhimu, maslahi ya umma na kuboresha utendekaji wa haki.
Amedai inazua maswali zaidi kwa sababu kadhaa; mbali ya kwamba ilitolewa wakati ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikuwa inakuja kutoa uamuzi kutokana na mabishano ya kisheria yaliyoibuka siku ya Jumatatu, hati mpya ya mashtaka haina kitu kipya isipokuwa hakimu na namba ya kesi. Vitu vingine vyote, ikiwemo aina, idadi ya mashtaka hadi nukta vimebaki vile vile kama vilivyokuwa kwenye hati ya mashtaka ya awali. Lissu alisema ndiyo maana jopo hilo linaiomba Mahakama Kuu ihoji dalili za uingiliwaji uhuru wa mahakama kwa DPP kuamua kutoa nolle prosequi, siku ambayo mahakama ilikuwa inakuja kutoa maamuzi juu ya mabishano ya kisheria.
"Ingawa mimi sijui mahakama ilitaka kusema nini… wenzetu wana taarifa za kiintelejensia, inawezekana wamejua hakimu angekuja kuamua nini kutokana na mabishano ya kisheria yaliyotokana na hoja za upande wa utetezi, hivyo wakaamua kuleta hiyo hati ya kufuta mashtaka. Kwa sababu haiingii akilini mawakili kama hawa wa serikali ambao wawili ni mawakili wakuu na mmoja wakili mwandamizi, walikosea waliyokosea," alisema Lissu na kuongeza;
"Ingawa watu wengi wanasema na kweli inaonekana hivyo kuwa mamlaka ya DPP kuingilia kesi yoyote na wakati wowote kabla haijatolewa hukumu ni makubwa sana, lakini ikumbukwe kuwa kuna kumbukumbu za maamuzi ya mahakama ambazo zinasema wazi kuwa mamlaka hayo ya DPP yana mipaka, hayawezi kufanyika isipokuwa iwe kwa ajili ya maslahi ya umma au kwa ajili ya kuboresha utendekaji wa haki, lakini kilichofanyika jana ni matumizi mabaya ya mamlaka ya DPP."
Kuhusu video
Wanahabari walitaka kujua maoni yake kuhusu video na namna kesi hiyo ilivyo, hasa kutokana na alivyoielezea ‘charge’ ilivyo ‘defective’, ambapo Wakili Lissu kwa maoni yake, alisema kuwa kuna masuala mengi yanatakiwa kuwekwa wazi kuhusu video yake, akihoji maswali kadhaa:

- Nani aliyemrekodi Lwakatare? Je, Lwakatare alijua kuwa anarekodiwa? Je, aliruhusu? Kama hakuruhusu, ilifanyika kihalali? Je, haivunji katiba ya nchi inayozungumzia privacy ya mtu? Je, baada ya kurekodiwa mkanda huo ulipelekwa wapi? Nani alikuwa nao? Je, umefanyiwa uhariri (editing) na nani? Je, aliyemrekodi alitumwa na nani?
Ushahidi mwingine
Ameongeza kuwa, video inaonekana imechukuliwa tarehe 28 Desemba, siku iliyofuata, Desemba 29, kwenye kipindi cha TV, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba akaanza kusema kuwa anayo video ya viongozi wakuu wa CHADEMA wakipanga mipango ya mauaji ya dhidi ya Watanzania.

Amezungumzia mawasiliano ya mtu anayeitwa Michuzi, kuwasiliana na watumishi wenzake wa OBR, akiwapongeza na kutoa kudos kwa TISS kwa kazi nzuri, akiwataka wenzake wapige sana kelele kwani hiyo ni kete muhimu kwa CCM. Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Usalama wa Taifa, hawaruhusiwi kufanya surveillance dhidi ya wapinzani wa kisiasa wa CCM, kwa sababu upinzani wa kisiasa ni suala lililoruhusiwa kisheria nchi hii. Aidha, Lissue ameongeza kusema wamepata mawasiliano ya simu yakionesha kuwa siku hiyo hiyo ambayo video imerekodiwa, majira ya saa 5.59, mtu aitwaye Ludovick alimpigia simu mtu aitwaye Mwigulu Nchemba.
Kwa mujibu wa Wakili Lissu, yamepatikana pia mawasiliano ya mtu aitwaye Dennis Msacky akimpigia simu Lwakatare, ambapo wamemuuliza Lwakatare iwapo ni kweli aliwasiliana na mtu mwenye jina hilo (ambaye kwenyecharge sheet ya pili, polisi wameonesha ndiye aliyekuwa akipangiwa kutekwa/kufanyiwa vitendo vya ugaidi), naye amekubali kuwa ni kweli alimpigia simu siku moja kabla ya tukio la kurekodiwa, akimuuliza kama amerudi Dar es Salaam, naye akamwambia alikuwa njiani kutoka Bukoba.
Amemaliza kwa kusema kuwa kesi hii ni kama kesi nyingine za kupikwa, ambazo polisi wamekuwa wakifungua dhidi ya CHADEMA na viongozi wa chama hicho, kwa nia ya kuiokoa CCM, kwasababu chama hicho kimekaliwa vibaya na hakiwezi tena kufanya siasa za ushindani dhidi ya wapinzani wao wakuu, CHADEMA.
"Ni mambo yale yale, walianza chama hiki cha familia ya Mtei na Mbowe, ikashindikana, chama hiki cha kikabila, cha Wachaga… ikashindikana, wakasema chama hiki cha kaskazini, imeshindikana, wamesema chama hiki cha wakatoliki, ikashindikana, wamesema chama hiki cha wakristo bado Watanzania wamekataa, iemshindikana pia… Sasa unafanyaje? Tengeneza hii kitu, sasa kiwe chama cha magaidi…ITASHINDIKANA pia," alisema Wakili Lissu.
Source: Fikira Pevu. (March).  Sakata la Lwakatare: Wanasheria CHADEMA " wafunguka". Retrieved from Fikira Pevu

No comments: