Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Saturday, March 23, 2013

Polisi wadai kumhoji "mtesaji" wa Ulimboka


NI RAMADHANI IGHONDU

JESHI la Polisi nchini limedai kumhoji mtu anayedaiwa kuwa Afisa Usalama wa Ikulu, Ramadhan Ighondu, anayetuhumiwa kuwa mhusika mkuu katika tukio la kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dk. Steven Ulimboka. Akizungumza na Tanzania Daima jana ofisini kwake, jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu, alisema kuwa tayari polisi ilishamhoji Ighondu kwa tuhuma hizo. Juni 26, mwaka jana, Dk. Ulimboka alitekwa na watu wasiojulikana na kupelekwa katika pori la Mabwepande ambako alipigwa na kuteswa vibaya kwa kunyofolewa kucha na kung’olewa meno na kisha kutelekezwa huko kabla ya kuokolewa na msamaria mwema na kukimbizwa hospitalini. Dk. Ulimboka alimtaja wazi wazi Ighondu kuwa ndiye alipanga na kuratibu njama za kutekwa kwake, na kusisitiza kauli yake hiyo kwa kula kiapo mbele ya wakili wake, Dk. Rugemezela Nshala, ambayo ilisomwa mbele ya waandishi wa habari. Mngulu alisema kuwa jeshi la polisi lilishamuita na kumhoji Ighondu kuhusiana na tuhuma za utekaji na kutesa zilizotolewa dhidi yake na Dk. Ulimboka na kwamba hawakubaini ushahidi wa kutosha kuweza kumfungulia mashtaka mahakamani. “Sisi tulishamhoji huyo Ramadhan Ighondu kuhusiana na tuhuma za Ulimboka dhidi yake, lakini hatukumfikisha mahakamani kwa sababu ushahidi haukujitosheleza. “Sisi tunapeleka mtuhumiwa mahakamani tunaporidhika kuwa ushahidi tulioupata una nguvu, na siyo kweli kwamba kila mtu anayehojiwa na polisi lazima afikishwe mahakamani,” alifafanua Mngulu. Aidha Mngulu alisema kuwa mbali ya kumhoji Ighondu, pia walimhoji wakili wa kujitegemea, Nyaronyo Kicheere, kuhusiana na suala hilohilo. Hata hivyo, Kicheere alikanusha kuhojiwa na polisi kuhusiana na suala la Dk. Ulimboka, bali aliitwa polisi kuwasilisha tamko la kisheria (hati ya kiapo) la Dk. Ulimboka ambamo anathibitisha kuwa Ramadhan Ighondu ndiye aliyepanga na kuratibu njama zote za kutekwa na kuteswa kwake.


“Siyo kweli kwamba nimewahi kuhojiwa na polisi kuhusu suala la Dk. Ulimboka, hawajanihoji, ila niliitwa makao makuu ya polisi na nilipofika pale hawakunihoji chochote bali waliomba niwape ile hati ya kiapo ya Dk. Ulimboka ambayo niliisoma mbele ya waandishi wa habari, na pia niliwapatia cheti cha kisheria cha kuniidhinisha kuisoma hati hiyo kwa waandishi wa habari,” alibainisha Kicheere na kuongeza: “Ila nimepata taarifa kwamba polisi wamepanga kuniita tena ili nikaandikishe maelezo, kwa hiyo nawasubiri waniite rasmi, lakini nasisitiza kuwa kwa sasa polisi hawajanihoji chochote kuhusu suala hilo,” alisisitiza. Hata hivyo, wakati polisi wakidai kumhoji Ighondu, hawajawahi kumuita wala kumhoji Dk. Ulimboka ambaye ndiye shahidi namba moja na mtu pekee anayewajua bila chembe ya shaka watekaji na watesi wake.

Source: Maziku G. (March 2013) Polisi wadai kumhoji "mtesaji" wa Ulimboka. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: