RUFAA DHIDI YA
UENDESHAJI WA BUNGE USIOKUWA WA HAKI NA UKIUKAJI WA KANUNI WA NAIBU SPIKA JOB
NDUGAI KATIKA KUONDOA HOJA BINAFSI YA MAJI
Tarehe 28 Februari
2013 nimewasilisha rasmi rufaa kwa mujibu wa Kanuni ya 5 (4) dhidi ya
uendeshaji wa Bunge usiokuwa wa haki wa Naibu Spika Job Ndugai kwa kukiuka
kanuni ya 58 (5) kwa kulihoji bunge kinyume na kanuni kufanya uamuzi badili wa
kuondoa hoja binafsi kuhusu hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa
majisafi na ushughulikiaji wa majitaka katika Jiji la Dar es salaam.
Nimefanya hivyo baada
ya kupata kumbukumbu rasmi ya Bunge (Hansard) za kikao cha tano cha tarehe 4
Februari 2013 cha mkutano wa kumi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika Mkutano huo
Naibu Spika Job Ndugai alisema na kufanya maamuzi kwamba: “Sasa ninahoji
wanaoafiki kwamba hoja hii iondolewe waseme ndiyo…..hoja imeondolewa.
Walioafiki Wameshinda”; wakati mtoa hoja sikuwa nimeomba idhini yoyote ya hoja
yangu kuondolewa.
Maamuzi hayo ni kinyume
na Kanuni ya 58 Fasili 5 ambayo inaelekeza kwamba “Endapo hoja imefikishwa
Bungeni, mtoa hoja anaweza tu kuiondoa hoja yake kwa kusimama mahali pake na
kusema ‘Ninaomba ruhusa kuondoa hoja’ na papo hapo Spika ataliuliza Bunge kama
linaafiki hoja hiyo kuondolewa na inapotokea Wabunge walio wengi watakubali,
Spika atasema ‘hoja hiyo inaondolewa kwa idhini ya Bunge’ na hoja hiyo itakuwa
imeondolewa na Bunge litaendelea na shughuli inayofuata”.
Ushahidi wa Kumbukumbu
Rasmi za Bunge (Hansard) za kikao tajwa unathibitisha ukiukwaji huo wa kanuni
kama ifuatavyo:
“……..WAZIRI WA MAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kuwa hoja iliyo mbele ya Bunge lako Tukufu ni kuitaka
Serikali kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi na uondoaji wa majitaka
Jijini Dar es Salaam, ambalo tayari linatekelezwa na mpango maalumu uliotengewa
fedha nyingi na Serikali, hivyo naomba kutoa hoja kwamba hoja hii iondolewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja……
………..MBUNGE FULANI:
Waziri amesema uongo,
amedanganya!
NAIBU SPIKA: Sasa ninahoji
wanaoafiki kwamba hoja hii iondolewe waseme
ndiyo.
WABUNGE FULANI: Sasa utaihoji vipi
wakati tuna majadiliano?
WABUNGE FULANI: Ndiyooooooooo!
NAIBU SPIKA: Wanaokataa waseme
siyo.
WABUNGE FULANI: Siyooo!
NAIBU SPIKA: Hoja imeondolewa.
Walioafiki wameshinda.
(Hoja ilitolewa
iamuliwe)
(Hoja iliamuliwa na
Kuafikiwa)
(Hoja Binafsi ya
Mheshimiwa John Mnyika
iliondolewa na Bunge)
MHE. TUNDU M. LISSU: Aaaaaa! Aaaaaaaaaaah!
Aibu!
NAIBU SPIKA: Hoja imeondolewa na
Bunge linaahirishwa hadi
kesho saa tatu kamili asubuhi…….”
Hivyo, pamoja na kuwa
Kanuni ya 8 inataka Spika kuendesha shughuli za Bunge na kutoa maamuzi kwa
haki, uadilifu na bila chuki wala upendeleo wowote kwa kuongozwa na Katiba ya
Nchi na Kanuni za Bunge, Naibu Spika wa Bunge alifanya maamuzi yenye kukiuka
kanuni ya 58 Fasili ya 5 kwa kuruhusu hoja yangu kuondolewa kwa hoja
iliyowasilishwa na Waziri wa Maji.
Kufuatia rufaa hii
Spika atataarifiwa kwa mujibu wa kanuni ya 5 (4) na kuitisha kikao cha kamati
ya kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 5 (5) ya kanuni za Kudumu za Bunge na
kulijulisha bunge kuhusu uamuzi utakaotolewa.
Wenu katika uwakilishi
wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
No comments:
Post a Comment