WANAFUNZI 823 wa darasa la nne katika shule za msingi wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga, hawakufanya mtihani wa kujiunga darasa la tano mwaka jana, kutokana na utoro unaodaiwa kusababishwa na njaa. Kutokana na hali hiyo, Serikali wilayani hapa imepanga kugawa chakula cha msaada, tani 140 za mahindi mashuleni, badala ya kuwagawia wananchi walioko katika kaya mbalimbali. Taarifa hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mkata, Mussa Mwanyumbu, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo katika kikao cha baraza hilo. “Ili kunusuru utoro kwa wanafunzi, kamati imeshauri wanafunzi wapatiwe mlo japo mmoja wakiwa shuleni, ili kuongeza mahudhurio yao na kiwango cha ufaulu tuna imani kitaongezeka,” alisema Mwanyumbu.
Naye Diwani wa Kata ya Kang’ata, Naku Shartiel, alisema utoro huo siyo kwa wanafunzi peke yao, bali hata baadhi ya walimu ni watoro kazini. Kwa hiyo, aliitaka idara ya kazi ya wilaya kuwashughulikia walimu watoro ili kiwango cha taaluma kisishuke wilayani humo. Akizungumzia utoro huo, Ofisa Elimu wa Shule za Msingi wilayani Handeni, Mochiwa Mgaza, aliahidi kufuatilia na kusema kuwa watakaobainika watachukuliwa hatua zinazostahili. “Waheshimiwa madiwani, naomba tushirikiane kuwafichua na kuwabana walimu pamoja na wanafunzi watoro, naomba pia mnipatie taarifa za walimu watoro mashuleni ili tuwadhibiti mapema, kwani kwa kufanya hivyo kiwango cha taaluma kwa watoto wetu kitapanda,” alisema Mgaza. Kwa upande wake, Katibu Tawala, Wilaya ya Handeni, John Tike, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Muhingo Rweyemamu, alisema wamepanga kugawa chakula cha msaada tani 140 kwenye shule za msingi na sekondari ili kuwavutia watoto kwenda masomoni. “Utoro huo wa wanafunzi unatokana na njaa, sasa Kamati ya Maafa ya Wilaya tumekaa na kubaini kwamba, Handeni kuna watu zaidi ya 41,559 wenye njaa kali na tumeahidiwa kupatiwa tani 156 za chakula, tani 16 kati ya hizo zitagaiwa bure kwa makundi maalum yasiojiweza,” alisema Tiky.
Source:Omari A. (March 12, 2013). Njaa yakwamisha wanafunzi kufanya mitihani. Handeni. Retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment