Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema mgogoro wa viongozi wake mkoani Kagera, hauna tija na badala yake, unarudisha nyuma jitihada za kujiimarisha. Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uendezi wa CCM, Nape Nnauye, ambaye aliwataka wakazi wa Manispaa ya Bukoba kuendelea na shughuli zao zikiwamo za miradi ya maendeleo. Alisema wananchi wanapaswa kufanya hivyo wakati wakisubiri majibu yatakayotolewa na tume itakayoundwa kuchunguza mgogoro huo. Mgogoro kati ya Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anathory Amani na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki, ulianza baada ya manispaa kuanza kutekeleza miradi mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa soko jipya na la kisasa, kituo cha mabasi na upimaji wa viwanja 5,000.
Katika mgogoro huo, Balozi Kagasheki alisema miradi iliyopangwa kutekelezwa na Manispaa ya Bukoba chini ya meya huyo haiko wazi, inaumiza wananchi na ina harufu ya ufisadi. "Chama kinasikitishwa na kinafedheheshwa na mgogoro huu, lakini hakiko tayari kuona shughuli za manispaa zinakwama kwa sababu ya mgogoro huo wa watu wawili ambao hauna manufaa kwa wananchi, chama na manispaa yenyewe," alisema Nnauye alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya vikao vya ndani na viongozi wa chama hicho na baadhi ya madiwani. Mkutano huo ulikuwa na lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
Alisema mgogoro huo unaowahusisha viongozi wanaotokana na chama kimoja cha CCM, umeathiri vikao vilivyopo kwa mujibu wa sheria na havikufanyika. "Lakini pia unaathiri shughuli nyingine za manispaa zisiendelee maana vikao vinavyopaswa kujadili na kupitisha bajeti visipokaa, ina maana utekelezaji wa ilani ya CCM unasimama na wanaoumia ni wananchi si viongozi wanaolumbana," alisema. Nnauye alisema kabla ya kutoa uamuzi wa kuruhusu shughuli za manispaa ziendelee, walikaa na madiwani wa CCM ambao ndiyo wengi na kukubaliana kuwa ziendelee kwa manufaa ya jamii ya wananchi. “Manispaa inaongozwa kwa kanuni na sheria za nchi, hivyo shughuli zote zitaendelea kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo, sisi chama hatuko juu ya sheria,” alisema.
Source:lugakingira L. (March 3, 2013). Mgogoro wa Kagasheki, Amani waikera CCM. Bukoba. Retrieved from Mwananchi
No comments:
Post a Comment