Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Monday, March 4, 2013

CCM YAHAHA KUJINUSURU


NAPE AWAANGUKIA MADIWANI BUKOBA WASHIRIKI VIKAO


HATIMAYE Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeafiki msimamo wa madiwani wake mjini Bukoba, na kumwomba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuunda tume ya kumchunguza Meya wa Manispaa hiyo, Dk. Anatory Amani. Hatua hiyo inakuja kutokana na mvutano mkali uliopo kati ya madiwani na Meya Amani, wakitaka kumng’oa kutokana na tuhuma za ufisadi wa miradi mikubwa mitatu anayodaiwa kuitekeleza bila kuwashirikisha. Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) ya CCM, Nape Nnauye, alilazimika kwenda mjini Bukoba juzi na kufanya vikao vya ndani na madiwani hao pamoja na wanachama baada ya Meya Amani kupuuza maagizo ya awali ya Makamu Mwenyekiti, Philip Mangula aliyefika kutatua mgogoro huo mwezi uliopita. Mgogoro huo umefika pabaya baada ya hivi karibuni madiwani tisa wa CCM wakishirikiana na baadhi wa vyama vya CHADEMA na CUF kukwamisha vikao vya Baraza la Madiwani vilivyokuwa vijadili bajeti ya 2013/2014. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Nape alisema kuwa amefanya vikao na madiwani wao pamoja na wanachama, na kisha kuamua kuwa Meya Amani aundiwe tume ya kuchunguza tuhuma dhidi yake.


Alisema kuwa wamemwomba waziri mwenye dhamana na Tamisemi kuunda tume hiyo ili ichunguze tuhuma hizo za miradi ya uuzaji viwanja, ujenzi wa soko la kisasa na kituo kikubwa cha mabasi kwa sababu mikataba yake haikuwekwa wazi. Nape alisisitiza kuwa ikibainika alifanya udanganyifu, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Katibu huyo aliwaangukia madiwani tisa wa CCM waliokuwa wamegoma kushiriki vikao vya Baraza la Madiwani, akiwataka washiriki kwa manufaa ya wananchi wakati huu tume itakapokuwa ikifanya uchunguzi wake. Kuhusu vipeperushi vilivyosambazwa hivi karibuni mjini hapa vikiwakashifu na kuwatusi madiwani wanaompinga Meya Amani, Nape aliiomba serikali kufanya uchunguzi wa haraka ili kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua bila kujali nyadhifa zao.
Alisema kitendo hicho ni kibaya kwani kinachochea uhasama wa udini na ukabila. Madiwani 10 wa halmashauri hiyo akiwemo Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagesheki walitukanwa matusi ya nguoni kupitia vipeperushi hivyo vilivyosambazwa na watu wasiojulikana. Waliotukanwa ni madiwani nane wa CCM na wawili wa CUF waliosaini hati ya kumtaka Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Hamis Kaputa kuitisha kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani ili kumng’oa Meya Amani anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Halmashauri hiyo ina madiwani 24; watatu wa CUF, wanne wa CHADEMA na 17 wa CCM. Na ili kikao cha baraza kiweze kuendelea ni lazima akidi ya mahudhurio iwe na nusu ya wajumbe. Meya Amani ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kagondo, wiki iliyopita alipata wakati mgumu hadi kulazimika kukiahirisha kikao hicho baada ya akidi kutotimia.
Wakati wa kuanza kikao ukumbini walikuwemo wajumbe 11, yaani madiwani nane wa CCM, wawili wa CHADEMA na mmoja wa CUF, jambo lililomlazimu kuwapigia simu baadhi ya ambao walikuwa hawajafika na kuwashawishi bila mafanikio. Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Zipora Pangani naye aliingilia kati kumsaidia meya akiwapigia simu madiwani hao kila mmoja na kumbembeleza ataje mahali alipo ili amtumie gari imchukue au kitabu cha mahudhurio asaini huko aliko, lakini ilishindikana. Habari zaidi zinasema kuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera naye aliingilia kati kwa kumwagiza katibu wa wilaya awatafute madiwani wa chama hicho ambao hawakuwa ukumbini, lakini haikuwezekana kwani simu zao zilikuwa zimefungwa. Meya Amani ni kama alipuuza maagizo ya Mangula kwa kuamua kufungua kesi mahakamani kupinga kujadiliwa na kung’olewa na madiwani.

Mangula aliagiza madiwani nane wa CCM waliokuwa wamesaini hati hiyo, waondoe tuhuma hizo na kuzipeleka kwenye chama ili zipatiwe ufumbuzi. Madiwani waliosaini hati ya kutaka kuitishwa kikao cha kumng’oa meya huyo mbali na Kagasheki ni naibu wake, Alexander Ngalinda (Kata ya Buhende) na Yusuf Ngaiza (Kashai) ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Bukoba. Wengine ni Richard Gasper (Miembeni), Dauda Kalumuna (Ijuganyondo), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe) na Mulubi Kichwabuta (Viti Maalumu) na wale wa CUF ni Ibrahim Mabruk (Bilele) na Rabia Badru wa Viti Maalumu. Wiki iliyopita madiwani hao nane wa CCM walikabidhi barua kwa Katibu wa Wilaya wakipinga kushiriki vikao vyote vitakavyoongozwa na Meya Amani wakimtuhumu kuwa ndiye alihusika kusambaza vipeperushi vya kuwakashfu. Balozi Kagasheki ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na madiwani wenzake kadhaa wa CCM, waliwasilisha barua zao kwa mkurugenzi ili kuondoa tuhuma zao kwa muda asubuhi ya Januari 23 mwaka huu, lakini mchana wa siku hiyo, Amani akafungua kesi ya kupinga asijadiliwe.
Mangula aliwataka madiwani hao kuunda kamati ya kushughulikia mgogoro huo chini ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe ingawa naye pamoja na Pangani, Mwenyekiti na Katibu wa CCM mkoa wanadaiwa kumkingia kifua Amani.

Source: Tanzania Daima (March 4, 2013). CCM yahaha kujinusuru. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: